Maafisa wa polisi nchini Uganda wameimarisha
usalama katika maeneo mengi ya uma katika mji mkuu wa Kampala kufuatia
kukamatwa kwa washukiwa kadhaa wa makundi ya kigaidi na vilipuzi.
Msemaji wa polisi ameiambia BBC kwamba jaribio la kutekeleza mashambulizi limetibuliwa. Awali
,ubalozi wa Marekani mjini Kampala ulisema kuwa mamlaka ilitibua
shambulizi la kigaidi lilokuwa limepangwa na washukiwa wa kundi la
Alshabaab. Ubalozi wa Marekani umewataka raia wake nchini Uganda kuendelea kukaa majumbani mwao. Ubalozi
huo tayari ulikuwa umeonya kuhusu shambulizi la kulipiza kisasi dhidi
ya maeneo ya Marekani na kundi la Alshabaab ili kujibu shambulizi la
angani la Marekani lililomuua kiongozi wa kundi hilo mapema mwezi huu.
Jeshi la Nigeria linasema kuwa limewaua zaidi
ya wanamgambo 100 wa kundi la Boko Haram kufuatia shambulizi la
wapiganaji hao siku ya ijumaa kazkazini mashariki mwa jimbo la Borno.
Vikosi
vya serikali vimeripotiwa kuyakamata magari na risasi wakati vilipokuwa
vikiimarisha usalama katika mji wa Konduga,yapata kilomita 35 kutoka
mji mkuu wa jimbo hilo, Maiduguri. Wapiganaji wa Boko Haram wameiteka miji kadhaa na vijiji katika majuma ya hivi karibuni wakikaribia kuelekea Maiduguri.