MAPYAA!
Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrati (DP), Abdul Juma Mluya
ameibuka na kusema mazingira ya kifo cha aliyekuwa mwenyekiti wa chama
hicho, Mchungaji Christopher Mtikila yamejaa utata huku akiweka wazi
kwamba, inavyoonekana aliuawa kabla ya ajali yenyewe.
Mtikila
alifariki dunia katika ajali ya gari aina ya Toyota Corolla namba T189
ARG, Oktoba 4, 2015 iliyotokea kwenye Kijiji cha Msolwa, Bagamoyo,
Pwani. Wengine watatu walijeruhiwa.
Mti ambao gari liliugonga kwa juu kabla ya kupinduka.
Akizungumza na Uwazi mwishoni
mwa wiki iliyopita kwenye ofisi ndogo ya chama hicho nyumbani kwa
marehemu, Mikocheni B jijini Dar, Mluya alisema hata watu waongee vipi,
lakini uchunguzi wao umeonesha kwamba, kiongozi wao aliuawa tofauti na
eneo la ajali na mwili kwenda kutupwa pale.
ROHO YAKE ILIWINDWA KWA SIKU 40
Mluya alisema:
“Ndugu mwandishi, Mchungaji Mtikila kama kufa alikuwa afe muda mrefu
sana pengine siku arobaini zilizopita (mpaka siku ya kifo cha kweli),
kwa sababu amewindwa na watu ambao hatujajua lengo lao kubwa lilikuwa
nini!
“Kila alikokwenda kwa shughuli za kichama kulikuwa na timu ya watu inayomfuatilia.”
...Baada ya Kupinduka
MARA YA KWANZA
“Tarehe
siikumbuki, lakini ni Septemba mwanzoni. Tulikuwa Bunda, Mara kwenye
shughuli za chama, kuna watu ambao walikuwa hawaeleweki walitufuata
mpaka hotelini.
“Baada ya kubaini hilo, nilimuuliza mwenyekiti kuhusu ratiba aliyokuwa nayo ya kuzungumza kwenye runinga ya Staa TV.
“Alinipa
ratiba. Baada ya kumaliza kuzungumza, nilimwambia Bunda si mahali pa
kulala hivyo nilimshauri aondoke, aende Mwanza. Na nilimwambia dereva
wake aondoke bila kuaga.”
WAKIWA NJIANI
“Lakini cha
ajabu, wakiwa njiani wakielekea Mwanza kuna gari liliwafuata kwa nyuma
kwa mwendo ambao waliutulia shaka. Dereva wa mwenyekiti alipokuwa
akiongeza mwendo, naye anaongeza, akipunguza naye anapunguza.
“Ilibidi dereva amwambie mwenyekiti naye akamtaka dereva aongeze kasi hadi Mwanza.”
“Katika ratiba
yetu tulitaka kufanya ziara za kichama kuanzia Oktoba 18, mwaka huu
kwa kuanzia mkoa wa Kigoma na kwingineko. Pamoja na kufuatiliwa kote
kule mwenyekiti hakuwa na roho ya uoga hata kidogo. Alimtanguliza sana
Mungu.
“Kwa hiyo wasiwasi mkubwa wa kufuatiliwa na watu hao ulianza Mara na Mwanza kwa nyakati tofauti.
“Septemba 11,
mwaka huu ndiyo tarehe ambayo sasa nilianza kukariri matukio hayo hatua
kwa hatua. Siku hiyo tulikwenda kwenye Kijiji cha Usangu mkoani Pwani
kwa ajili ya kufanya kampeni ya mgombea udiwani. Baada ya kumaliza
tuliamua kurudi Dar lakini njiani dereva akasema kuna watu hawajui
wanakuja nyuma yetu.”
WAPOTEA NJIA KWA KUFUATILIWA
“Tulijikuta
tukipotea njia na kutokea mjini Kisarawe (Pwani). Pale tulifika kituo
cha mafuta ambapo tulikuta gari aina Toyota Land Cruiser VX limepaki
kama vile ni watu pia walikuwa wakitufuatilia.
“Lengo la
kusimama pale lilikuwa kupata chakula lakini hatukufanya hivyo kulingana
na mazingira. Tukaanza safari ya kurudi Dar. Tulipofika Pugu Sekondari,
gari lile lilitupita kwa kasi na kupotea.
“Tulipofika
Tazara gari lile lilionekana na wakati huo yalikuwa mawili.
Kilichotushangaza ni upya wa magari lakini eti namba zinaanzia na A.
Mimi nilifikiria kwamba, pengine ni za idara ya usalama wa taifa
zilikuwa doria mbalimbali hasa kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi.
“Ndugu mwandishi, mimi ninafanya kazi ya siasa, niko makini sana. Niliwaambia wenzangu kuwa tunafuatiliwa.
“Ndani ya gari
sisi tulikuwa na viongozi wa kuwapeleka Temeke. Lakini baada ya kufika
huko lile VX tulikutana nalo. Tulipomuacha yule tuliyempeleka kule,
tukawa tunampeleka mchungaji nyumbani kwake (Mikocheni) lakini bado lile
gari lilikuwa likitufuatilia.”
WAPIGA CHENGA
“Tulipofika
maeneo ya Msasani kwa Mwalimu (Julius Nyerere) dereva alikunja kona
kuelekea kwa mchungaji na lile gari likakunja kona na kurudi
lilikotoka.”
SIKU NYINGINE
“Siku
iliyofuata tulipanga mipango yote ambapo sasa tulisema Oktoba 18, mwezi
huu tuanze ziara ya mkoa wa Kigoma na maeneo mengine ya Kanda ya Ziwa.
“Mimi
niliondoka kuelekea Shinyanga, yeye (Mchungaji) aliandaa safari ya
kwenda Njombe kwenye kampeni ya mgombea Ubunge Jimbo la Njombe.”
OKTOBA 2, 3, 2015
“Mwenyekiti
aliondoka Dar Oktoba 2, kuelekea Njombe. Oktoba 3, alinipigia simu
asubuhi na kunijulisha kuwa jana yake walipata ajali maeneo ya
Makambako wakati wanakwenda.
“Nilimuuliza alipata matibabu, akajibu kuna viongozi wa Njombe walifika na kumchukua hivyo yuko sawasawa.”
TAARIFA YA AJALI
“Siku hiyo
hiyo walifanya kampeni na jioni yake walianza safari ya kurejea Dar.
Walipofika Mkoa wa Pwani, saa kumi na moja alfajiri, Mchungaji Mgaya
alinipigia simu na kuniambia walikuwa njiani wanarudi Dar, wamepata
ajali mbaya sana. Lakini hakuniambia kama mchungaji amefariki dunia.
“Nilianza
kufuatilia tukio hilo na kuuliza kama kuna msaada wowote wameupata,
akasema mpaka muda huo polisi walikuwa hawajafika. Mimi napenda sana
kufungua mitandao ya kijamii, nilipofungua nikakuta picha zilishasambaa
kwenye mitandao kitu ambacho nilijiuliza usiku huo huyo mpigapicha
alikuwa wapi?”
SHAKA KUBWA YA DP
“Sisi DP,
mashaka yetu makubwa ni mazingira mazima ya namna kiongozi huyo
alivyofariki dunia. Hata mtoto hawezi kudanganywa kwa namna hiyo. DP ina
taasisi ya kufanya uchunguzi iitwayo Liberty International Foundation
iliyokuwa ikisimamiwa na marehemu. Ipo kazini kwa sasa ili kubaini
ukweli wa kifo cha mwenyekiti na tutaweka wazi kila kitu.”
“Laini pia tunaitaka serikali kufanya uchunguzi na kutoa taarifa hadharani.”
MWENYEKITI KIJIJI AIBUKA NA YAKE
Uwazi pia lilifika aneo la ajali na kujionea kwa macho mazingira yake na kupata maelezo kutoka kwa baadhi ya mashuhuda.
Joshua Mohamed
Msigala ni Mwenyekiti wa Kijiji cha Msolwa, Chalinze, Pwani palipotokea
ajali. Yeye anasimulia mambo aliyoelezwa na mmoja wa majeruhi,
Mchungaji Patrick Mgaya siku ya tukio.
“Kwanza kabisa
waandishi wa habari mmefanya vizuri kufika eneo la tukio na kujionea
hali halisi. Nawaeleza hali halisi ilivyokuwa mpaka mimi kufika eneo la
ajali.
“Siku hiyo
asubuhi ya saa kumi na moja na nusu kama sikosei, nikiwa nyumbani
nilipigiwa simu na dereva mmoja wa lori anayenijua. Akasema ameona ajali
maeneo yangu lakini hajui kama kuna waliokufa au la!”
MWENYEKITI AWAHI NA BODABODA
“Kusikia
hivyo, nilichukua bodaboda ili niwahi. Nilifika ndani ya dakika kama
kumi tangu kutokea kwa ajali. Nilikuta mwili wa Mtikila umelala pembeni
ya gari huku wengine watatu waliodai walikuwa ndani ya gari wakiwa
wamesimama tu.
“Ila kati ya hao watatu, mmoja alijitambulisha kuwa ni Mchungaji Mgaya, yeye wakati nafika alikuwa akiongea kwa simu.”
ALICHOAMBIWA NA MCHUNGAJI
“Nilimuuliza
mchungaji ilikuwaje? Akasema wakati wanapata ajali hiyo, marehemu
Mtikila na wengine wawili walichomoka ndani ya gari hali iliyosababisha
kifo cha Mtikila. Hata hivyo, kwa upande wangu sikuamini kama wote
walichomoka kutoka kwenye gari bali mazingira yalionesha walitoka
wenyewe.
“Mchungaji
alizidi kuniambia kuwa, gari lilipaa juu zaidi ya futi kumi na kugonga
mti kisha likapinduka na kulalia paa (kwenye Uwazi siku ya tukio,
mchungaji alisema gari lilibiringika).
“Lakini pia
siamini, kwani pamoja na kuona alama katika mti sikubali kama
zilisababishwa na ajali kwani kama ni hivyo gari lingekuwa limepondeka
zaidi juu lilikoangukia tofauti na lilivyokuwa likionekana.”
KILICHOMSHANGAZA ZAIDI MWENYEKITI
Mwenyekiti
huyo alizidi kusimulia kushangaa kwake: “Kitu kingine kinachonishangaza
ni kwamba, kwa maelezo yao gari liliacha barabara likawa linaendeshwa
pembeni kwa umbali wa meta mia moja (urefu wa uwanja wa mpira). Kwa nini
dereva asipunguze mwendo ambapo angefanya hivyo gari lisingefika kwenye
mti.”
“Kinachoshangaza
kingine ni kwamba, hakuna majeraha yaliyoonekana kwa macho kwa
walionusurika hata kuonesha kwamba walikatwa na vioo wakati wakirushwa
nje kutoka ndani ya gari. Hata viti vya mbele vilikuwa vilevile,
havikuharibika na kama majeruhi walirushwa nje walipitia wapi?”
WALIOFIKA AWALI
Mwenyekiti
huyo alisema anawashukuru askari wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania
(JWTZ) wa Kambi ya Kizuka na Sangasanga waliokuwa wakipita ambapo
walifika kutoa msaada.
“Baadaye mimi
nilifanya mawasiliano na Polisi wa Kituo cha Chalinze (Bagamoyo) ambapo
walifika eneo la tukio. Pia polisi wa mkoa nao walifika na saa 12:30
asubuhi majeruhi na mwili wa marehemu walipelekwa Hospitali Teule ya
Rufaa Tumbi.”
Naye Ofisa
Mtendaji wa Kijiji cha Msolwa, Joseph Hamad kwa upande wake alisema
alipokea taarifa saa 3 asubuhi na alipowasiliana na mwenyekiti
alimwambia yupo katika eneo la tukio.
Baadhi ya
wananchi wa kijiji hicho waliohojiwa na Uwazi walisema wameshangazwa na
ajali hiyo iliyosababisha kifo cha Mchungaji Mtikila na kuitaka serikali
kufanya uchunguzi wa kina.
SIMU YA MTIKILA YAZUA UTATA
Mpaka
tunakwenda mitamboni, familia ya Mtikila ilisema, jana ilitarajia
kufuatilia simu ya marehemu kwani haijulikani ilipo na pia kujua walipo
dereva (George Ponella) na msaidizi wake (Ally Mohamed) ambapo awali,
dereva alishikiliwa na jeshi la polisi.
Habari imekusanywa na Makongoro Going, Haruni Sanchawa na Issa Mnali.
Source:GPL
0 comments:
Chapisha Maoni