Ijumaa, 6 Mei 2016

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Singida Asimamishwa Kazi Baada ya Kutoa Taarifa za Uongo Kuhusu Watumishi HEWA

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Singida, Simion Mumbee amesimamishwa kazi baada ya kudaiwa kutoa taarifa za uongo kuhusu watumishi hewa.
Katika taarifa hiyo, Mumbee anadai watumishi hewa 19 waliogundulika kwenye halmashauri hiyo hawajaisababishia hasara Serikali jambo linalodaiwa kuwa si kweli.
Akizungumza jana kwenye ufunguzi wa kikao cha maendeleo mkoani humo, Mkuu wa Mkoa wa Singida, Mathew Mtigumwe alisema anamsimamisha kazi mkurugenzi huyo ili kupisha uchunguzi.
“Nilipotuma tume kufuatilia suala la watumishi hewa katika Halmashauri ya Wilaya ya Singida, ilibaini wapo na wameisababishia Serikali hasara ya zaidi ya Sh125 milioni,” alisema Mtigumwe.
Alisema taarifa ya Mumbee ililenga kuidanganya Serikali. Mtigumwe alimuagiza Katibu Tawala wa Mkoa, Dk Angela Lutambi kumuandikia barua ya kumsimamisha kazi mara moja.
Mtigumwe alisema hana nafasi ya kufanya kazi na watumishi wa aina ya Mumbee.
Wakati huo huo; Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Said Mwambungu amemsimamisha kazi Ofisa Utumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea, Philbert Mtweve kwa tuhuma za kuwalipa mishahara watumishi hewa wanane na kuisababishia Serikali hasara ya Sh27 milioni.


PICHA: Jionee kaburi atakalozikwa Papa Wemba

Picha hii inasemekana ndilo kaburi atakapozikwa mwanamziki Maarufu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo maarufu kwa jina la Papa Wemba.
Huu ni zaidi ya ufahari, lakini mimi naona hauna maana..


CHADEMA na Katibu Mkuu mfu..Ukimya Wake ni Hatari kwa Mustakabari wa Chama

Kiukweli huyu katibu mkuu hajui hata pa kuanzia Chama kinaonesha dalili za kuifuata TLP na UDP sioni harakati zake ki ukweli CHADEMA ilikosea sana Dr. Mashinji ni unpopular figure hata akitembea kwa miguu Karikoo hakuna wa kumshitukia kuwa ni kiongozi.
Ukimya wake ni hatari kwa mustakabari wa chama kwani watu wasiokuwa na vyeo kama akina Lowassa ndo wamekuwa msaada mkubwa kukisemea chama kwa sasa. Anaonekana kabisa ni uteuzi ambao ulikosewa na ni mtu asiyekua na ushawishi ndani ya chama.
Kutoka kwenye nchi ya viwanda mpaka nchi ya majipu alikuwa ana mengi ya kuongea lakini yupo kimyaa wakisubiri kuzungusha mikono mwaka 2020.
Huku serikali ya Magufuli ikijisafishia njia inaonekana haitapata upinzani mwaka 2020 kutokana na uchakavu wa CHADEMA.


Nuh Mziwanda Afunguka Kuhusu Kurudiana na Shilole

Msanii Nuh Mziwanda ambaye kwa sasa anafanya poa na wimbo wake mpya ambao amemshirikisha Alikiba amefunguka na kusema kuwa hata kama ikitokea mpenzi wake huyo wa zamani akitaka kurudiana na yeye ni kitu kisichowezekana kwa sasa.
Akizungumza kwenye kipindi cha 5SELEKT kinachorushwa na ting’a namba moja kwa vijana Nuh Mziwanda amesema kuwa kwa sasa yeye amefunga ukurasa wa mapenzi na Shilole hivyo hata ikitokea akataka kurudiana na yeye hawezi kufanya hivyo kwani ameshaanza maisha mapya ambayo anaona ni ya furaha zaidi.
Mbali na hilo Nuh Mziwanda ameeleza kuwa kwa sasa hataki tena maisha ya kiki na skendo alizoita kuwa ni za ajabu ajabu bali anataka kujenga jina lake kutokana na kazi zake kwenye muziki pamoja na kutengeneza muziki kama ‘Producer’


Mheshimiwa Rais Wanaodhani Wako Juu ya Sheria ni Wengi Sana...Soma Kisa Hichi

MIAKA michache iliyopita, wakati wa Serikali ya Awamu ya Nne ambayo imeshapita, kuna jambo moja lilinishangaza sana. Jambo hili lilimhusu Waziri wa Serikali hiyo na mlinzi wa benki.
Kilichotokea ni kwamba Mheshimiwa Waziri alikwenda kwenye mashine ya kutolea fedha, maarufu kama ATM, huenda kwa ajili ya kutoa fedha. Akiwa ndani ya kile chumba akaanza kuzungumza na simu. Akazungumza na simu kwa muda mrefu, hali iliyosababisha wateja waliokuwa wakiisubiri huduma hiyo kuanza kulalamika na kumlazimu mlinzi kumuomba Waziri awapishe wateja wengine waweze kupata huduma.
Hilo halikumfurahisha Waziri yule na badala yake akaanza kumwuliza mlinzi kama anajua yeye ni nani, kwa kuwa yeye kama Waziri ana mambo mengi ya maana na alikuwa akizungumza na simu muhimu. Kwa huyo Waziri, suala la kuzungumza kwenye chumba cha ATM na kuwanyima fursa wateja wengine kama yeye kuipata huduma waliyokuwa wakiihitaji kwa wakati, halikuwa tatizo kabisa.
Sakata la Mheshimiwa Waziri na mlinzi wa benki liliripotiwa kwenye vyombo vya habari na bahati mbaya mwisho wake ulikuwa wa kusikitisha, kwani mlinzi alifukuzwa kazi kutokana na kutimiza majukumu yake. Baadhi ya watu walipiga kelele, lakini hakuna kilichotokea. Sana sana, baba wa watu akabaki bila kazi, huku akiwaza ataitunzaje familia yake iliyokuwa ikimtegemea.
Sasa juzi hapa hali hiyo imejirudia tena.  Safari hii, hata hivyo, imemhusisha Mke wa Mheshimiwa Waziri mwingine, ambaye alibishana na askari wa usalama barabarani aliyekuwa akitimiza majukumu yake ya kazi kwa kumweleza makosa ya barabarani aliyoyatenda. Badala ya kusikiliza makosa yake na kuadhibiwa kwa kadiri ya matendo yake, mke huyu aliitumia karata yake ya kupitia mgongo wa mumewe na kutoa kauli za kuudhi zisizofaa kwa yule askari.
Kwa mara ya kwanza katika kipindi kirefu sana, mambo yanaelekea kubadilika na wale waliokuwa wakidhani wapo juu ya sheria, wanakumbushwa tena kwamba Tanzania sio ya kwao peke yao.
Taarifa zinasema kwamba Rais John Pombe Magufuli ameamuru askari wa usalama barabarani aliyekuwa akifanya kazi yake na kuishia kutolewa maneno yasiyofaa na Mke wa Waziri, apandishwe cheo.  Vilevile, ameshamuonya Waziri na Mke wake kuhusiana na tukio hilo, kwani hakuna mtu aliye juu ya sheria.
Binafsi, taarifa hiyo imenifurahisha sana. Tuseme tu ukweli kwamba Tanzania ilikuwa nchi ya ajabu sana. Ilikuwa na matabaka makubwa sana kiasi cha watu kuzungumzia kutaka hata kukimbilia kuishi nje ya nchi, kutokana na kujiona hawathaminiwi, huku wengine wakitamba mitaani na kufukuzisha watu kazi kana kwamba wao ndio wamiliki halali wa nchi hii.
Tanzania ilifika mahali ambapo huyu askari wa usalama barabarani ambaye Rais ameamua kumpandisha cheo, angekuwa katika hali ngumu sana. Kwanza angetafutiwa zengwe, kisha angehamishwa kituo cha kazi na kupelekwa kijijini huko kwenye kitengo cha kawaida kabisa. Wale aliowaudhi, wangehakikisha kwamba jamaa harudi tena mjini, na anasahaulika kabisa.
Lakini yote hii ni kutokana na ulimbukeni wa kada fulani kudhani wako juu ya sheria na hawatakiwi kuguswa, huku sie akina yakhe tukiendelea kulipa faini halali na wakati mwingine kuadhibiwa na askari mwenye hasira za kutendwa na watu wa aina ya Mke wa Waziri.
Lakini pamoja na taarifa njema hizi tulizozisikia mwishoni mwa wiki, bado tuna safari ndefu sana.  Bado wapo watu wanaodhani wako juu ya sheria, hawatakiwi kuguswa na wanaruhusiwa kufanya chochote wanachojisikia kukifanya kwa kuwa wao ni wao na hawawezi kulinganishwa na Watanzania wengine.
Katika hili, naomba nizungumze na Mheshimiwa Rais na kumweleza maajabu ya Tanzania, ambayo bado hayajaandikwa kwenye Kitabu cha Guinness Book of Records.
Mheshimiwa Rais, hivi unafahamu kwamba kwenye nchi hii mtu akiwa na gari lenye nembo za Serikali, kama vile STK, huwa anavunja tu sheria za barabarani na haulizwi chochote? Ataona watu wote tupo barabarani, tumesimama kwenye foleni, tunasubiri nafasi yetu ifike ili tuendelee na safari, lakini yupo radhi kupita hata njia za pembeni za watembea kwa miguu na hataguswa. Eti ile nembo tu ya STK inamfanya awe juu ya sheria.
Mheshimiwa Rais, wapo pia hawa wengine ambao wanadhani kwamba kutokana na vyeo walivyonavyo, vyeo ambavyo aidha wewe ama watangulizi wao mmewapa, basi hata wakifika maeneo ya huduma za umma, kama vile hospitali, hawahitaji kufuata utaratibu wa kusimama kwenye foleni kama sisi wengine tufanyavyo.  Watafika, watawaona mmesimama, watapitiliza bila kuwasemesha huku wakiwa wamekunja nyuso zao kwa hasira na ukijaribu kuhoji, watakuuliza “unajua mimi ni nani?” Hawa pia wanadhani wako juu ya sheria.
Mheshimiwa Rais, wapo pia wale ambao wanajiona wapo ‘grade’ ya juu zaidi. Hawa hufikia mahala pa kutumia magari ya umma, magari ambayo sisi tunayalipia kodi ili yanunuliwe, yakarabatiwe na yajazwe mafuta, lakini wao kuamua kuyatumia kwa mambo yao binafsi. Magari haya yatakwenda sokoni kununua mchicha na vitunguu, yatapaki saluni kumsubiri ‘mama’ ajiweke vizuri na yatapaki baa kusubiri bosi apate mapumziko ya kutosha, hata kama ni hadi usiku wa manane. Yaani sisi tunakatwa kodi ili wao watumbue maisha, kwani wanadhani kwamba wako juu ya sheria.
Mheshimiwa Rais, wapo na wale ambao hata tukiwa kwenye foleni za benki, basi wao wataingia na kupitiliza ili wahudumiwe kwanza, kana kwamba wengine tuliosimama pale ni milingoti ya TANESCO na hatuna mambo mengine ya kufanya. Ukihoji, utasikia: “kwani wewe hujui mimi ni nani?  Nina mambo muhimu ya kitaifa ya kufanya.” Unabaki unajiuliza, hivi kumbe kuna watu na WATU. Kwa kila kitu, wao wapo juu ya sheria.
Naomba tu niseme kwamba hali hii ilikera kiasi kwamba tukaizoea na ndio maana hata Mke wa Waziri alipotoa maneno yasiyofaa kwa askari wa usalama barabarani, hakuna aliyejua kwamba askari yule angepandishwa cheo na Waziri kuonywa. Sana sana, tulikuwa na uhakika kwamba hili litasambazwa sana kwenye mitandao ya jamii, huku wale wanaotukana askari kwamba wanachokitaka ni rushwa tu, wakiendeleza kauli hizo za kuudhi.
Watu walijiona kwamba wao ndio Watanzania halisi na wengine ni wa kusingiziwa.  Watu walijiona kwamba wao ndiyo pekee wenye haki miliki ya nchi.  Watu walijiona kwamba wao wako juu ya sheria. Mheshimiwa Rais, naomba nikuhakikishie kwamba watu hao bado wapo wengi…


Mfanyabiashara Dangote Atajwa Kutumbuliwa kwa Juliet Kairuki TIC

Wakati aliyekuwa Mkurugenzi wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), ametajwa kutenguliwa uteuzi wake kwa kukataa kuchukua mshahara wa Serikali kwa miaka mitatu mfululizo, uchunguzi umebaini kuwa jipu la kusamehe kodi Kampuni ya Saruji ya Dangote ndilo lililomwondoa.
Uchunguzi uliofanywa umebaini kuwa mbali na Juliet Kairuki kutochukua mshahara wa Sh 5,000,000 kila mwezi aliopangiwa na Serikali kwa miaka mitatu, kwa maana kuwa ameacha kuchukua wastani wa Sh milioni 180 kwa muda huo, anatuhumiwa kusamehe Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwa wawakezaji bila kufuata utaratibu au sheria za nchi.
“Hili la mshahara ni cha mtoto. Amewadanganya wawekezaji wengi kuwa anaweza kuwapa msamaha wa kodi ya VAT, na sasa Serikali hii ilipoingia madarakani ikasema hana mamlaka hayo. Mwekezaji wa kwanza aliyedanganywa ni Dangote,” anasema mtoa taarifa wetu.
Uchunguzi uliofanywa umebaini kuwa Novemba, 2015 Kampuni ya Dangote iliingiza nchini makaa ya mawe tani 35,000 kutoka Afrika Kusini na kutaka makaa haya yasamehewe kodi zote.
“Kwa kweli tulishangaa sana. Kwanza, makaa ya mawe si bidhaa za mtaji (capital) bali ni za matumizi tu (consumables). Vifaa vinavyosamehewa kodi ni zile zinazotumika kuzalisha bidhaa nyingine leo, kesho, mwakani au miaka mitano ijayo na kuendelea, ila makaa ya mawe ukiyachoma yanaisha siku hiyo hiyo, hivyo hii si mtaji.
“Ukiacha hilo, hawa watu wa Dangote wameambiwa wanunue makaa ya mawe kutoka Kiwira au Ngaka, lakini hawataki,” kinasema chanzo chetu na kuongeza kuwa kwa mwaka uliopita, waliagiza tani 2,000 tu za makaa ya mawe kutoka Tancoal kinyume cha makubaliano ya kuongeza ajira nchini.
Afisa kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) amefichua katika uchunguzi huu kuwa kinachoendelea kwenye Kampuni ya Dangote ni balaa. “Hii kampuni tulidhani imekuja hapa kukomboa wananchi, lakini uhalisia siyo.
“Kampuni hii inafanya malipo bila kutoa kodi ya zuio, bidhaa inazoingiza nchini pamoja na nyingine kupata misamaha ya kodi bado inaongeza bei zinakuwa ghali mno kwa maana ya kuongeza gharama za uzalishaji na hivyo kupunguza kiasi cha kodi kinachostahili kulipwa… ni shida,” anasema afisa huyo kwa uchungu.
Kutokana na mkanganyiko huo, Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Alphayo Kidata, ameunda timu ya kufanya ukaguzi maalumu kwa Kampuni ya Dangote ambayo imewakuta na hatia.
“Hiyo bilioni 20 ni uchunguzi wa awali, tunaweza kupata kiasi kikubwa zaidi. Tunawashukuru kwa kuandika habari za ukwepaji kodi, na nakuhakikishia sisi tunafuatilia kila mnachochapisha,” anasema mtoa habari wetu.
Afisa mwingine wa TRA anasema mbinu kubwa inayotumiwa na Dangote na kampuni nyingine ambazo tayari TRA imekwishaibaini mbinu wanazotumia kupunguza faida (Tax Base Erosion), kwa kuingia mikataba yenye gharama kubwa na kampuni walizo na uhusiano nazo kibiashara, kuonesha wametumia gharama kubwa wakati uhalisia wanafanya mbinu za kukwepa kodi.
Akizungumzia sakata hili, Mejena Mkuu Mwandamizi wa Kampuni ya Dangote, Vidya Dixit, amekiri kupokea ankara ya malipo kutoka TRA yenye thamani ya bilioni 20 na akasema: “Wakaguzi wa TRA wako hapa, wamefanya uchunguzi wao, wametuletea madai yao, na sisi tunawasiliana na mshauri wetu wa masuala ya kodi, ikithibitika kuwa tunadaiwa kiasi hicho Dangote ni kampuni kubwa, tutalipa.”
Dixit amesema TRA wamekagua mikataba mbalimbali wanayotumia akina Dangote kuagiza bidhaa na huduma, na wakaja na kiasi hicho, hivyo kwake halioni kama ni tatizo, washauri wao wa masuala ya kodi wakikuta ni kweli watalipa tu. Chanzo chetu kimetueleza kuwa mshauri wao ni Kampuni ya PriceWaterhouseCoopers (PWC) ya Afrika Kusini.
Meneja huyo alijibu pia swali kuwa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TRA) inawadai dola 2,867,400 za Marekani (sawa na Sh bilioni 6.3), kwa kusema: “Mimi sisimamii idara ya uhasibu. Madeni hayo yanaweza kuwapo, ila Dangote ni kampuni kubwa, kama kuna madeni ya aina yoyote tutalipa tu baada ya kujiridhisha kuwa ni madeni halali.”
Kuhusu suala la tani 35,000 za makaa ya mawe kutoka Afrika Kusini, alisema wao kama Dangote hawapaswi kulaumiwa kwani walifuata taratibu zote: “TIC walitupa sisi msamaha wa kodi, sasa tumezungumza na Waziri wa Fedha akasema TIC hawana mamlaka ya kutoa msamaha wa kodi bila kutangaza kwenye Gazeti la Serikali (GN) na kweli hakukuwapo GN yoyote.
“Sasa hapa tunapata tabu kidogo, idara moja ya Serikali inasema hivi na idara nyingine inasema vile, tunapata shida kidogo,” anasema Dixit. Katika makaa hayo ya mawe pekee ambayo wanatakiwa kuyanunua kutoka nchini, Dangote wanadaiwa wastani wa Sh bilioni 1.1.
Kuhusu tuhuma zinazoelekezwa kwa kiwanda hicho kuwa kimewageuka wafanyabiashara wadogo na kupendelea wafanyabiashara wakubwa kwa njia ya kuwauzia saruji nyingi na kutowajali wadogo, Dixit anasema wao hawana ubaguzi na ucheleweshaji unaweza kutokea kunapotokea dharura.
Anasema kuna wakati wanaangalia nani ana ghala kubwa la kuhifadhia saruji kiasi gani, ila hiyo haiondoi ukweli kwamba hawabagui yeyote anayetaka kununua na kuuza saruji ya Dangote.
“Ukisema kuna walioshindwa kupata saruji kwa wiki moja au mbili, hilo naweza kukuelewa, lakini miezi miwili, wala asikudanganye mtu. Hilo haliwezekani. Ni kweli kule Lindi tunakotoa chokaa, machimbo yote kwa siku tatu zilizopita yalijaa maji, tukashindwa kupata chokaa, lakini zaidi ya hapo kila mtu anapewa fursa sawa ya kununua saruji bila ubaguzi,” anasema Dixit.
Awali, baadhi ya wafanyabiashara waliilalamikia Kampuni ya Dangote kuwa inauza saruji kwa upendeleo, hali inayowafanya wakose mapato kwani wamekopa mikopo benki na wanaishia kutopata saruji kwa wakati hivyo wanashindwa kulipa hiyo mikopo.
“Kuna mfanyabiashara ameweka kwenye akaunti ya Dangote Sh bilioni 2.5, huyu ndiye anayepewa saruji sisi wengine tunapuuzwa. Watanzania wengi wamekopa benki wastani wa Sh milioni 20, 30 au 50 wanaziweka kwenye kampuni ya Dangote na hawapati hiyo saruji. Hii inatutia hasara mno. Tunataka usawa katika biashara hii,” anasema mmoja wa wafanyabiashara anayedai ameweka Sh milioni 25 kwenye Kampuni ya Dangote, lakini hapatiwi saruji.
Pia, wanalalamikia bei kubwa ya saruji ya Dangote kwani wakati kiwanda kinaanza kujengwa Watanzania walitangaziwa kuwa mfuko mmoja wa saruji ungeuzwa kwa Sh 8,000, lakini sasa bei inafikia Sh 16,000 kwa mikoa kama Mwanza na kwa Dar es Salaam inauzwa kati ya Sh 10,800 na 12,500.
Kamishna Mkuu wa TRA, Kidata, hakuwa tayari kulizungumzia kwa undani suala la Dangote zaidi ya kusema: “Hili suala lipo, tunalifanyia kazi, ni mapema mno kulizungumzia kwa sasa.”
Hata hivyo, afisa mwingine mwandamizi alishangaa kusikia kuwa Dangote bado wanatafuta ushauri wa kisheria kama walipe kodi hiyo au la: “Hawa waliishakwenda hadi kwa Bwana Mkubwa wakakubali kulipa, sasa leo inakuwaje wanatafuta ushauri?” Alihoji afisa huyo.
Alichosema ni kuwa kila mfanyabiashara mkubwa kwa mdogo ajiandae kulipa kodi. “TRA haitaingilia mapato halali ya mfanyabiashara yeyote, ila kwa yeyote anayekwepa kodi hili halitavumiliki. Serikali ya sasa inasema hapa ni kazi tu, hakuna habari ya jina kubwa au dogo. Jipu ni jipu tu, bila kujali ni kubwa au dogo, yote yatakamuliwa tu.”


Wabunge wa UKAWA Wamzomea Profesa Tibaijuka huku Wakimwita Mwizi.......Ni Baada Ya Kupingana na Hoja za Tundu Lissu Aliyedai Zanzibar Ni Koloni La Tanganyika

Mbunge wa Muleba Kusini (CCM), Profesa Anna Tibaijuka jana alikuwa mkali bungeni akisema yeye si mwizi na kuwabeza wanaomuita hivyo kuwa wataisoma namba.
Profesa Tibaijuka alifikia hatua hiyo baada ya kuhamaki kutokana na baadhi ya wabunge wa upinzani kupaza sauti na kumuita mwizi wakati akichangia hotuba ya bajeti ya Wizara ya Katiba na Sheria.
Profesa Tibaijuka alianza kwa kuwataka wabunge wamuunge mkono Rais John Magufuli kwa kuwa amechaguliwa na wananchi.
“Wenzetu ambao kazi yao ni kuja kutusimamia sisi (upinzani) wana haki ya kusema wanayoyasema, lakini hata sisi tuna haki ya kuyaweka vizuri ili yaeleweke kwa wananchi,” alisema.
Profesa Tibaijuka alisema upinzani ukifilisika utabaki kukemea kwa sababu ni lazima tu useme kitu, Bunge linageuka kijiwe na bungeni si mahali pa kupeleka hoja za vijiweni.
Kauli hiyo iliwakera wabunge wa upinzani ambao walianza kupaza sauti zao dhidi yake, hali iliyoonekana kumchanganya.
Akirejea hotuba ya msemaji wa kambi ya upinzani bungeni, Tundu Lissu kuwa Tanganyika inainyonya Zanzibar na kuifanya koloni lake, Profesa Tibaijuka alihoji: “Tanganyika inainyonya Zanzibar katika lipi? Hili ni jambo la kujiuliza. Nimejiuliza mimi kama mchumi. Kazi yangu ya kwanza nyinyi mnanijua nilikuwa kwenye shirika la makazi duniani, hamjui kwamba nilikuwa kwenye Shirika la Biashara la Dunia?” alihoji.
Kutokana na zomeazomea kuendelea, Spika wa Bunge, Job Ndugai aliingilia kati: “Waheshimiwa wabunge namlinda mzungumzaji, naomba muwe wavumilivu. Mheshimiwa Profesa endelea."
“Kwa wale wanaosema nimeiba mtaisoma namba, mimi si mtu wa kutishwa na vitu vya ovyoovyo.
"Mimi sitishwi na hoja za ovyoovyo, huyo (mtu) akaisome namba. Nasimama hapa kwa sababu nataka nitetee vitu. Mtu anapopotosha anaweza kuleta hatari. Tanganyika kwa mtizamo wa kiuchumi haiwezi kuinyonya Zanzibar.
“Katika Dunia ya ustaarabu unasikia hoja. Lissu hapa angeweza kuzomewa, lakini wastaarabu wakamsikiliza wamekomaa kisiasa,” alisema huku baadhi ya wabunge wakiendelea kumzomea.
Tibaijuka aliwahi kuwa waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi wakati wa utawala wa Rais Jakaya Kikwete na aliondolewa baada ya kutuhumiwa kupata mgawo wa fedha za Tegeta Escrow.


Mwita Waitara Azusha Tafrani Bungeni.......Ni Baada ya Kutaka Kumchapa Ngumi Mbunge wa Kasulu Aliyedai Tundu Lissu na Mnyika Ni Vichaa

Mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara (Chadema) ametolewa nje ya Bunge baada ya kutaka kumkwida Mbunge wa Kasulu Vijijini, Agustine Holle (CCM) aliyedai kuwa Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu na Mbunge wa Kibamba, John Mnyika wote wa Chadema kuwa wanaugua kichaa.
Waitara alionesha kukerwa na kauli hiyo hasa pale Holle alipokataa kufuta kauli yake, licha ya kutakiwa kufanya hivyo na Naibu Spika, Dk Tulia Akson.
Wakati Holle akichangia, Waitara alinyanyuka kwenye kiti chake na alipofika alipo mbunge huyo alimzungumzisha maneno ambayo hayakusikika na kuonesha kama kutaka kumpiga kabla ya kukaa kwenye kiti kilicho mbele yake ndipo, Holle alisikika akisema “wewe unataka nini” ndipo Naibu Spika alipogundua kuwa Waitara anataka kumpiga Holle na kumuamuru atoke nje lakini hakutii amri hiyo.
Kutokana na kutotii, Naibu Spika aliamuru askari wamtoe ndipo walipoingia zaidi ya askari watano na kutoka naye hadi nje ya geti kubwa la kuingilia bungeni.
Holle wakati anachangia bajeti ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa mwaka wa fedha 2016/2017, alimtaja Lissu ambaye ni Waziri Kivuli wa Wizara hiyo kuwa ana taarifa kuwa Lissu amewahi kuugua ugonjwa wa kichaa na hadi sasa ana faili kwenye Hospitali ya Vichaa ya Mirembe iliyopo mkoani Dodoma.
Hata hivyo, alipopewa nafasi na Naibu Spika kufuta kauli yake akasema “nafuta kauli yangu lakini kwa taarifa zilizozagaa nimeamini ni kweli na mbona kwao(Chadema) wapo wengi hata Mnyika sasa hivi yupo Muhimbili anatibiwa kichaa”.
Kutokana na kauli hiyo, Lissu alisema licha ya kuifahamu Hospitali ya Mirembe, hajawahi hata kuingia kwenye geti la hospitali hiyo wala kuugua ugonjwa huo na kutaka kiti cha Naibu Spika kimtake Holle athibitishe ; na akishindwa kanuni zielekeze hatua za kuchukua kama zilivyowekwa.