Ijumaa, 11 Desemba 2015

Namba za Simu za Kuripoti Kero TRA na taarifa za siri za Watumishi Wabadhirifu

Dk Mpango ametaja namba za simu na kuomba wananchi waripoti taarifa zinazohusu watumishi wa ofisi ya Mamlaka na Mapato Tanzania (TRA), wanaojilimbikizia mali kinyume na kanuni za utumishi wa umma.

Pia ameomba namba hizo zitumike kutoa taarifa kuhusu kero wanazokumbana nazo wananchi katika ofisi za TPA.
Piga simu 0689 122 515
Tuma ujumbe mfupi wa maneno (sms) 0689 122 516
Pia ametoa namba yake kuwa ni 0787 570 714 na ya Naibu wake kuwa ni 0784 228 095

Profesa Lipumba, Lissu wapinga uteuzi wa Muhongo na Mwakyembe

Saa chache baada ya rais Magufuli kutangaza baraza lake la Mawaziri ambalo limekuwa baraza dogo kama alivyoahidi, aliyekuwa mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF) na mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu wamekosoa uteuzi wa Profesa Sospeter Muhongo na Dk. Harison Mwakyembe.

Dk. Mwakyembe alikuwa waziri wa Uchukuzi katika serikali ya awamu ya nne na hivi sasa ameteuliwa kuwa waziri wa Katiba na Sheria. Profesa Muhongo ambaye alijiuzulu kwa kashfa ya Escrow katika serikali ya awamu ya nne, amerudishwa katika wizara ya Nishati na Madini.

Profesa Lipumba amekosoa uteuzi wa profesa Muhongo kwa madai kuwa uteuzi wake umelitia doa baraza hilo.

“Kwa kitendo kama hiki, Rais Magufuli amejiwekea dosari kutokana na uteuzi huu. Maana yake ni kuwa katika kashfa ile Profesa Muhongo hakuwa na hatia,” Profesa Lipumba aliliambia gazeti la Mwananchi.

Profesa Lipumba aliongeza kuwa wananchi watapata ugumu kumuelewa Rais kutokana na ahadi zake kuwa atapambana na rushwa na ufisadi.

Naye Tundu Lissu aliliambia gazeti hilo kuwa uteuzi wa Dk. Harison Mwakyembe hakuwa sahihi kwa kuwa ndiye aliyekuwa waziri wa Uchukuzi na punde baada ya rais Magufuli kuingia ikulu, Mamlaka ya Bandari ikabainika kukumbwa na kashfa ya upotevu wa makontena.

“Juzi Rais Magufuli aliufumua uongozi wa Bandari ya Dar es Salaam kutokana na kashfa, miongoni mwa waziri waliokuwa wakisimamia sekta hiyo ni Dk. Harrison Mwakyembe, eti leo amemrudhisha kundini?” Lissu ananukuliwa.

Lissu aliongeza kuwa Muhongo pia hakufaa kuwa miongoni mwa mawaziri kwa kuwa alifukuzwa na Bunge kutokana na sakata la Escrow.

Hata hivyo, Profesa Lipumba alimpongeza rais kwa kutekeleza ahadi yake ya kuunda baraza dogo kwa lengo la kubana matumizi.

Home Shoppinga Center Yajitokeza Kujibu Tuhuma Za Kukwepa Kodi

Baada ya kusambaa kwa taarifa kwenye mitandao zikieleza kuwa kampuni ya Home Shopping Centre imefunga maduka yake kutokana na kukwepa kodi na kuhusika kwenye sakata la makontena yaliyopotea bandarini, uongozi wa kampuni hiyo umejitokeza na kupinga taarifa hizo.

Kupitia taarifa yake kwa vyombo vya habari, kampuni hiyo imeeleza kuwa habari hizo sio za kweli na kueleza kuwa haijawahi kukwepa kodi na haihusiki kwa namna yoyote na makontena yaliyopotea bandarini.

“Home Shopping Centre Co. Limited haihusiki kabisa kwa njia yoyote ile na wizi, ukwepaji kodi, au potevu wa makontena 349 na yale zaidi ya 2431 yaliyoibuliwa na Mheshimiwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na kamwe haijawahi kujihusisha na uhalifu huo wa kuiba makontena na kukwepa kodi,” ilieleza taarifa hiyo iliyosainiwa na Mfilisi wa kampuni hiyo, Yusufu Mohamed.

Mohamed alieleza kuwa kampuni hiyo ilifunga maduka yake kama ambavyo makampuni mengine hufanya na sio vinginevyo.

Wema Sepetu Kortini Kwa Uwizi wa Umeme..Tanesco Waeleza Makubwa

KIMENUKA! Baada ya Miss Tanzania 2006 aliye pia nyota wa sinema za Bongo, Wema Sepetu ‘Madam’ kunaswa na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) akidaiwa kutumia umeme wa shirika hilo kinyemela, kuna madai atapandishwa kortini.
Taarifa kutoka chanzo makini zinasema kuwa, mrembo huyo alifanya ‘manuva’ hayo katika nyumba anayoishi, Kijitonyama, Dar hivyo kuweza kuliingizia hasara shirika hilo hali ambayo shirika hilo haliwezi kumvumilia.


“Amefanya ile michezo ya kuchezea mita. Mita inakuwa inasoma umeme mdogo lakini mzigo unaotumika ndani mkubwa, haufanani na malipo halisi ambayo alistahili kulipia,” kilisema chanzo chetu na kuongeza:
“Maofisa wa Tanesco juzikati ndiyo wakampitia. Inasemekana Wema alikuwa ndani na Idris (yule mshindi wa Big Brother Africa). Idris ndiye alitoka lakini Madam hakuinua miguu yake kwenda nje, wakamng’olea mita na kuondoka nayo.”

Baada ya chanzo hicho kuvujisha ubuyu huo sambamba na picha zilizosemekana ni za siku ya tukio wakati maofisa hao walipofika nyumbani hapo na kufanya ‘ambushi’, paparazi wetu alimpigia simu Wema kwa muda mrefu lakini hakupatikana, akampigia mtu wa karibu na Madam, Ahmed Hasheem ‘Petit Man’ ambapo alipatikana na kusema:

“Unajua kaka mimi si msemaji wa Wema. Mimi ni msemaji wa wasanii walio kwenye lebo ya Wema ya Endless Fame. Kama unataka msemaji wake, cheki na Martin Kadinda.”
Alipotafutwa Martin, alijibu kwa kifupi: “Kaka hata mimi nazisikia hizo habari lakini sipo Dar, nikirudi nitakwenda kucheki halafu nitakupa taarifa kamili.”
Juzi Jumanne, paparazi wetu alifika nyumbani kwa Wema ili kujionea sakata hilo lakini hakufanikiwa kuingia getini baada ya kugonga geti kwa muda mrefu bila majibu.
Mmoja wa majirani wa mrembo huyo aliyeomba hifadhi ya jina, alipoulizwa kuhusu kufahamu sakata hilo, alisema:

“Kiukweli sisi wenyewe tulishangaa. Tunaamini Madam si mtu kuchezea mita. Ni mtu anayejiweza, anayejitambua sasa tumeshtuka kuona mita inatolewa.”
Paparazi wetu alifika Ofisi za Tanesco Mkoa wa Kinondoni Kaskazini (Mikocheni) ili kuzungumza na wahusika lakini akakosa ushirikiano.

Hata hivyo, mfanyakazi mmoja wa Kitengo cha Emergency (Dharura) aliyeomba kufichwa jina lake, alisema ni kweli zoezi hilo lilifanyika nyumbani kwa Wema, Jumatatu iliyopita na kukutana na kadhia hiyo ambapo alisema madam huyo atapandishwa mahakamani kujibu mashitaka ya kuiibia Tanesco.
GPL