Jumanne, 4 Oktoba 2016

Hakuna Msanii Bongo Mwenye Vigezo vya Mwanaume Ninayemtaka – Shilole


Kwa mujibu wa Shilole, hakuna msanii Bongo aliye na vigezo vya mwanaume anayemhitaji kwa sasa.

“Hakuna hata mmoja,” Shilole alimjibu mtangazaji wa Kings FM, Prince Ramalove aliyemuuliza kama kuna msanii wa Bongo kwenye vigezo anavyovitaka.

Awali alitaja vigezo hivyo kuwa ni, “Upate mtu ambaye anakupenda kwa dhati, mchapakazi, ambaye anajua kwamba maisha ni nini,” alisema Shishi.

Kingine alisema kuwa mwanaume huyo awe mrefu. Shilole alikuwa na uhusiano maarufu na Nuh Mziwanda kabla ya kuachana na kuwafanya wawe maadui kwa muda. Kwa sasa wameamua kuziweka tofauti zao pembeni.

Baada ya Kuachana na Mbunge wa Donge,Wastara Arudiana na Mpenzi Wake wa Zamani


Mwigizaji Wastara aliwahi kuingia kwenye vichwa vya habari Tanzania kutokana na ndoa yake kuvunjika ndani ya siku 80 akiwa kaolewa na Mbunge wa Zanzibar.

Kabla ya ndoa hiyo Wastara alikuwa kwenye uhusiano na mshikaji ambaye ni staa wa Bongo Movie pia ambaye anaitwa Bondi, sasa basi baada ya taarifa kuenea katika mitandao mbalimbali kwamba amerudiana na Bondi leo ameyazungumza haya juu ya taarifa hizo.

‘Unajua watu hawajui tulipotoka yule ni mtu wangu wa muda mrefu ni makosa yake tu alinikosea ndio sababu ya mimi kuachana naye na ndipo nikaamua kwenda Zanzibar kuolewa yakatokea yaliyotokea na sasa niko na Bondi yaani nimerudiana naye nimesamehe yaliyopita kwasasa tuna kama miezi miwili tangu turudiana katika uhusiano wetu’

Mastaa 10 Wadaiwa Kuanika Miili Yao Kunasa Wanaume!


Hali ngumu na raha ya ubuyu usimung’unye mwenyewe! Ishu inayotrendi kwa sasa kwenye ulimwengu wa ubuyu wa mjini ni aibu ya baadhi ya mastaa wa kike Bongo kudaiwa kuwanasa wanaume mtandaoni kwa njia ya picha zinazoonesha sehemu kubwa ya miili yao.


Kufuatia ishu hiyo, kumeibuka malalamiko kwamba, picha hizo haziishii tu mitandaoni bali zinawafikia hata watoto wao na kumomonyoa maadili ya Kitanzania kwani baadhi ya watu, wakishavutiwa nazo, huzichukua na kutumiana kwenye simu hivyo kusambaa kwa watu wengi zaidi.

Chanzo makini ambacho ni mfuatiliaji wa karibu wa ishu za mastaa kimeeleza kwamba, baadhi ya mastaa hao wamekuwa wakisingizia kuwa wanatangaza nguo hasa za ndani ndiyo maana huvaa kihasara.



UGUMU WA MAISHA?
Lakini nyuma ya pazia, inadaiwa kuwa kutokana na ugumu wa maisha kwa sasa, ndiyo mbinu mpya ya kujipiga promo kwa ajili ya kujiuza kwa wanaume ambao huwatafuta baada ya kuona picha hizo. “Ninyi hamjui tu! Kama hamuamini, chunguzeni, wasichana kibao wa mjini pamoja na baadhi ya mastaa wamebuni njia rahisi ya kujiuza mitandaoni. “Wanachokifanya ni kwenda studio na kupiga picha kali zinazoonesha maungo yao kisha wanatupia mitandaoni.

WAWILI WATANGAZA MAFANIKIO
“Kuna wawili (mastaa) ambao ni marafiki zangu, wanasema wamefanikiwa kupata dau kubwa kwa siku kutoka kwa wanaume kwa sababu tu ya kujipigia promo wenyewe,” kilimwaga ubuyu chanzo hicho.


WALIOTAJWA HAWA HAPA
Baadhi ya mastaa wanaotajwa kujipigia promo kwa wanaume ni pamoja na Isabela Mpanda ‘Bella’, Hamisa Mobeto, Gift Stanford ‘Gigy Money’, Lulu Auggen ‘Amber Lulu’, Elizabeth Michael ‘Lulu’, Husna Maulid, Faiza Ally Lulu Semagongo ‘Aunt Lulu’, Mwanaisha Said ‘Dyna’ na Tunda Sebastian.
.

UBUYU YABAINI KITU
Kufuatia sakata hilo, Kona ya Ubuyu Ulionyooka ilizungumza na baadhi ya mastaa waliotajwa ambapo wapo waliokiri kuwa, biashara hiyo inalipa zaidi kwani haina gharama lakini pia walidai kuwa kila mtu ana maisha yake na anajua anapopatia mkate wake wa siku bila kujali kujiondolea utu.



MSIKIE GIGY:

“Kama inalipa, haimhusu mtu, ninachojua ni kweli wapo wanawake wengi wanaojiuza, cha muhimu ni kujua dau lako na siyo kufuatilia maisha ya wengine, mimi naishi maisha yangu.

” HUYU HAPA BELLA
Kwa upande wake Bella alifunguka kuwa, yeye si wale waliopo kwenye kundi hilo ila anapenda tu kupiga picha hizo kwa sababu ya mwili alionao na pia ikumbukwe kuwa aliwahi kuwa miss na kazi yake ya muziki na uigizaji vinamruhusu.


TUNDA ANAFUNGUKA:
“Mimi napenda kufanya nitakacho, siangalii watu wanataka nini ILIMRADI ni ukurasa wangu, siwezi kuzuiwa kufanya lolote. Kuhusu wanaume, hata wakija wengi huwa nawapotezea tu na wala hawajakosea kwa sababu wapo wanaodhani tunapiga picha kwa ajili hiyo na kutuma komenti kibao.” Hao ni baadhi ya mastaa waliopatikana na kupewa nafasi ya kujitetea lakini katika uchunguzi wa Wikienda, ilibainika kuwa wengi wanaoweka picha hizo, lengo lao huwa ni kutangaza nguo kama walivyowahi kujitetea Hamisa Mobeto, Lulu na wengineo.

NENO LA MHARIRI
Siyo hukumu ya Wikienda wala msomaji wake kuwa mastaa wanaotajwa ni kweli kwamba wanajiuza kwa njia hiyo lakini kama kweli wanafanya hivyo, wanapaswa kujiheshimu kabla ya kuumbuliwa kwani kila mmoja anajua kwamba tukimvalia njuga tutamuumbua.

Kama ni suala la matangazo ya nguo, basi wafanye matangazo kwa wakati kisha kujiweka kiheshima na siyo kila nukta kutupia picha za nusu utupu. Pia kama ishu ni kukosa wachumba, wakumbuke kuwa ndani ya mitandao hiyohiyo kuna uwezekano wa kuwepo kwa wachumba na wakwe hivyo ni rahisi kupoteza sifa za mke bora.

Polisi yamtia mbaroni askari aliyechukua rushwa kutoka kwa raia wa kigeni Zanzibar.


Jeshi la Polisi Zanzibar limemkamata askari wake anayetuhumiwa kupokea rushwa kutoka kwa raia wa kigeni baada ya kumkamata kwa kosa la barabarani na kumuachia huku akimuahidi kumlinda.

Uamuzi huo wa jeshi la polisi Zanzibar umetolewa na kamishna mkuu wa jeshi hilo hapa Zanziabr CP Hamdan Omar Makame wakati akiongea na waandishi wa habari katika makao makuu ya polisi ambapo amesema jeshi la polisi limesikitishwa sana na kulani kitendo hicho cha askari huyo akipokea rushwa kwa kosa la raia huyo kutovaa mkanda na kitendo hicho kusambazwa kwenye mitandao ambapo amemtaja askari huyo ni sajeti Talib Hamad na siyo jina la Ali huku pia akisema kitendo hicho kilifanyika Mkokotoni na sio Mahonda kama alivyokaririwa askari huyo kwenye mahojiano ya mtandao.

Kamishna mkuu huyo wa polisi Zanzibar amesema kwa sasa askari huyo atachukuliwa hatua za kinidhamu kwa mujibu wa taratibu za kipolisi na ikithibitika kuwepo kosa la jinai atapelekwa kwenye vyombo vya sheria vya dola huku na akisisitiza wananchi waendelea kutoa ushirikiano.

Kwa mujibu wa tukio hilo lilivyoonekana kwenye mtandao huo raia huyo alikamtwa kwa kosa la kutovaa mkanda wa gari na askari huyo aliamua kuchukua leseni ya barabara na kumuhakikishia kuwa aendele na safari na atamlinda huku akionekana akipokea fedha taslimu.

Profesa Lipumba Apata Pigo, Baraza la Wadhamini CUF Lagoma Kumtambua, Lapanga Kufunga Jengo la Chama


TAMKO LA BODI YA WADHAMINI YA THE CIVIC UNITED FRONT (CUF – CHAMA CHA WANANCHI) KUFUATIA KIKAO CHAKE KILICHOFANYIKA JANA, TAREHE 2 OKTOBA, 2016

Kwa kuzingatia hali iliojitokeza katika chama chetu cha THE CIVIC UNITED FRONT (CUF – Chama Cha Wananchi) kufuatia hatua ya makusudi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi, kutupandikizia vurugu na fujo kwa kujipa mamlaka asiyokuwa nayo ya kutuamulia nani awe Mwenyekiti wa Chama, hatua ambayo imesababisha mtu anayeitwa Ibrahim Haruna Lipumba na genge lake tarehe 24 Septemba, 2016 kuvamia na kuhodhi jengo la Ofisi Kuu ya Chama iliyopo Buguruni, Dar es Salaam, Bodi ya Wadhamini ya Chama iliona kuna haja ya kukutana na kuchukua hatua za kukabiliana na matukio hayo.

Bodi ya Wadhamini ya The Civic United Front (CUF – Chama Cha Wananchi) imefanya kikao chake, tarehe 2 Oktoba, 2016 katika Makao Makuu ya Chama, mjini Zanzibar chini ya Mwenyekiti wake, Mhe. Abdallah Said Khatau.

Tumefanya hivyo kwa kutambua wajibu wetu kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Siasa, Sura 258 ya Sheria za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (Political Parties Act, Cap 258) na Katiba ya CUF ya 1992 (Toleo la 2014).

Ni vyema ieleweke kwamba kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Siasa, kila chama cha siasa chenye usajili wa kudumu kinapaswa kuunda Bodi ya Wadhamini ambayo ndiyo inayokuwa mmiliki na msimamizi wa mali zote za chama cha siasa husika. Kifungu cha 21 cha Sheria ya Vyama vya Siasa kinalieleza hilo kama ifuatavyo:

“21. —(1) Every political party which has obtained a certificate of full registration shall appoint a board of trustees to manage the properties and any business or investment of the party.

(2) Every board of trustees shall be duly incorporated under the Trustees Incorporation Act and every party shall, not later than sixty days from the date of full registration, submit to the Registrar—
a) the names and addresses of the members of ther board of trustees; and
b) a copy of the certificate of incorporation.”

CUF kilitimiza masharti hayo ya kisheria kwa kuunda Bodi ya Wadhamini, na Katiba ya Chama ya 1992 (Toleo la 2014), Ibara ya 98 ikafafanua zaidi namna inavyopatikana, pamoja na nguvu na uwezo wake kichama, kama ifuatavyo:

“98._ (1) Kutakuwa na Bodi ya Wadhamini ya Chama itakayoteuliwa na Baraza Kuu la Uongozi la Taifa kwa mujibu wa sheria za nchi kwa kipindi cha miaka mitano (5) na mjumbe anaweza kuteuliwa tena baada ya muda wake kumalizika.

(2) Bodi itakuwa na wajumbe wasiozidi tisa (9), watano (5) kutoka Bara angalau wawili (2) wakiwa ni wanawake na wanne (4) kutoka Zanzibar angalau mmoja (1) akiwa ni mwanamke ambao watateuliwa kwa masharti yanayohitajika ya Sheria ya Bodi ya Wadhamini na utaratibu uliowekwa na Baraza Kuu la Uongozi la Taifa.

(3) Bodi ya Wadhamini itakuwa ndiyo mdhamini pekee wa fedha na mali za Chama pamoja na madeni na itafanya shughuli zake kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizowekwa na sheria ya nchi inayohusu Wadhamini.

(4) Bodi inaweza kushitaki au kushitakiwa kwa niaba ya Chama.

(5) Bodi itawajibika kwa Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la Chama ambalo linaweza kuweka utaratibu unaofaa wa kuendesha shughuli za Bodi hiyo, na itafanya vikao vyake angalau mara mbili kwa mwaka.

(6) Mwenyekiti na Naibu Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini watachaguliwa na Wajumbe wa Bodi kutoka miongoni mwao, kwa sharti kwamba Mwenyekiti akitoka upande mmoja wa Jamhuri ya Muungano, Naibu Mwenyekiti atatoka upande mwengine wa Jamhuri ya Muungano.”

MAAMUZI YA BODI YA WADHAMINI:
Kufuatana na uwezo wake uliotajwa hapo juu na kwa kuzingatia nafasi yake kama mdhamini pekee wa fedha na mali za Chama (rejea Ibara ya 98(3) iliyotajwa hapo juu, Bodi ya Wadhamini imefikia maamuzi yafuatayo:

1. Imepuuza wito wa mtu anayeitwa Ibrahim Haruna Lipumba alioutangaza jana kwamba eti amemtaka mtu mwengine anayeitwa Thomas Malima kuitisha kikao cha Bodi ya Wadhamini. Lipumba kwa sasa si Mwenyekiti tena wa CUF na pia si mwanachama wa CUF baada ya kufukuzwa uanachama na Baraza Kuu la Uongozi la Taifa.

2. Itaendelea kuwajibika kwa Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la Chama kama inavyotakiwa na Ibara ya 98(5) ambalo ndilo linaloiteua Bodi na litaheshimu maamuzi yote ya Baraza Kuu la Uongozi la Taifa likiwa ndiyo chombo chenye dhamana ya kusimamia uongozi na uendeshaji wa Chama.

3. Itachukua hatua za kisheria chini ya uwezo wake iliopewa na Ibara ya 98(3) na 98(4) kurejesha chini ya dhamana yake mali zote za Chama zilizovamiwa, kuporwa na kuhodhiwa na Ibrahim Lipumba na genge lake ikiwemo jengo la Ofisi Kuu ya Chama iliopo Buguruni, Dar es Salaam.

4. Itachukua hatua za kisheria chini ya uwezo wake iliopewa na Ibara ya 98(4) dhidi ya Ibrahim Lipumba kumtaka alipe gharama na hasara zote alizozisababisha kwa kuvamia Mkutano Mkuu Maalum wa Taifa wa Chama, tarehe 21 Agosti, 2016 katika Ukumbi wa Blue Pearl, Ubungo Plaza na genge lake kufanya vurugu, ghasia na uharibifu wa mali za hoteli na hatimaye kuvuruga Mkutano Mkuu jambo lililosababisha hasara ya takriban Sh. 600 milioni; na kisha kuvamia Ofisi Kuu ya Chama, Buguruni, Dar es Salaam, tarehe 24 Septemba, 2016 ambapo alisababisha hasara ya takriban Sh. 50 milioni.

5. Itachukua hatua za kisheria chini ya uwezo wake iliopewa na Ibara ya 98(4) kwa kumshtaki Msajili wa Vyama vya Siasa kwa kuingilia maamuzi halali ya vikao halali vya Chama na kulazimisha kukichagulia Chama chetu Mwenyekiti kinyume na onyo lililowahi kutolewa na Mahakama Kuu dhidi ya Ofisi yake kutokuwa na mamlaka ya aina hiyo.

6. Inawahakikishia wanachama wote wa CUF wa Tanzania Bara na Zanzibar kwamba Bodi yao ya Wadhamini iko makini na itasimama pamoja nao kulinda mali zote za Chama.

7. Inaionya Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa iwache kuingilia mambo ya ndani ya uongozi na uendeshaji wa Chama cha CUF.

HAKI SAWA KWA WOTE

Abdallah Said Khatau
MWENYEKITI WA BODI

Joran Lwehabura Bashange
KATIBU WA BODI