Namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijaalia siha njema na pia kwa kunipa mwangaza wa kuandika hiki ninachokusudia.
Pia niwashukuru wapenzi wasomaji wa safu hii ambao tumekuwa
tukiwasiliana na kushauriana hili na lile katika tasnia hii adhimu ya
mapenzi. Nawakaribisha sana!
Labda kwa wale wasiofahamu niwaambie tu kwamba dhana ya mapenzi ni dhana
yenye wigo mpana sana na ndiyo maana hutasikia hata siku moja
tumepumzika kuizungumzia.
Hata hivyo, tunachofanya siku zote ni kukumbushana kwa yale
tunayoyafahamu na kushauriana kwa pale tunapohisi wengi hufanya makosa.
Baada ya kusema hayo sasa nigeukie mada yangu ya leo ambayo kwa kiasi
kikubwa inawahusu wale walio kwenye ndoa na kikubwa nazungumzia yale
ambayo wawili waliotokea kupendana kwa dhati wanatakiwa kuyafanya mara
baada ya kumaliza kufanya tendo la ndoa.
Nalazimika kuandika makala haya baada ya kubaini kuwa wengi wamekuwa
wakifanya makosa na kujikuta wakishamaliza kufanya tendo hilo takatifu,
kila mmoja anageukie kwake kisha kuuchapa usingizi.
Sisemi kwamba ni lazima kuyafanya haya nitakayoyaeleza leo ila
yakifanywa huwa na manufaa yake na mara nyingi yanaboresha uhusiano.
Kuoga pamoja
Mtakuwa ni watu wa ajabu kama mtamaliza kufanya tendo hilo kisha kila mmoja kulala na majasho yake. Wapo
wasiojali katika hili na kuona kuoga au kutooga ni uamuzi wa mtu. Elewa
linapokuja suala la usafi inashauriwa mkimaliza lazima muoge.
Wapo wanawake ambao wakishamaliza hukimbilia kuwaandalia maji wenza wao,
wakishaoga ndipo nawo huenda kuoga. Hivi unaona ugumu gani kwenda kuoga
na mwenza wako? Unaijua raha ya kuoga na huyo wako wa maisha?
Wanaofanya hivyo wanajua raha yake na wewe ambaye hujawahi, anza leo.
Mmemaliza mambo yenu, chukuaneni kimahaba, elekeeni bafuni kisha
ogeshaneni kimahaba.
Baada ya hapo rudini chumbani, mkishajifuta maji pandeni kitandani mkiwa wapesi.
Kusifiana
Hakuna muda maalum uliotengwa kwa ajili ya wanandoa kusifiana. Hilo
linaweza kufanyika wakati wowote lakini pale mnapomaliza kufanya tendo
la ndoa ni lazima utakuwa na jambo zuri la kumuambia mwenza wako.
Msifie kwa utundu na ubunifu wake. Msifie pia kwa mapenzi matamu
anayokupa na ikibidi mpe sifa ya uzuri wake kiasi cha kukufanya kila
unapokuwa karibu yake ujisikie amani ya kupitiliza.
Wapo ambao hawana kabisa kasumba ya kuwasifia wala kuwashukuru wenza wao
kwa mazuri wanayofanyiwa. Yaani wao wanachukulia kila kitu poa tu bila
kujali kwamba kusifiana kunanogesha mambo.
Kuelekezana
Kwenye kale kamchezo, wapo ambao wanakosea, kuelekezana na kukosoana kwa
wapenzi ni jambo la kawaida. Yawezekana mwenza wako alifanya kitu
ambacho hakikukufurahisha wakati mkiendelea na burudani yenu,
mnapomaliza mwambie lakini kwa lugha ya kimahaba na ya upole. Naamini
kwa kufanya hivyo atakuelewa na kubadilika.
Zungumzieni maisha
Huu ni wakati muafaka wa kujadili changamoto na malengo katika maisha
yenu. Hapa akili zinakuwa zimetulia na kila mmoja anakuwa na mawazo
chanya kwa mwenza wake. Jadilini mambo yenu, wekeni mikakati ya
kuliboresha penzi na maisha yenu kwa ujumla.
Hayo ni baadhi ya mambo ambayo mnashauriwa kuyafanya pale mnapomaliza kufanya tendo la ndoa.
Yapo mnayotakiwa kuyaepuka ili kutotibua furaha iliyopatikana. Hayo
nitakuja kuyaeleza katika makala zinazokuja kupitia ukurasa huu.