Alhamisi, 12 Mei 2016

Mpinzani wa Museveni , Dr Kiiza Besigye Akamatwa Baada ya Kujiapisha Kuwa Rais

Mpinzani mkuu wa Rais wa Uganda, Yoweri Museveni, Dk. Kizza Besigye ambaye amekuwa akipinga ushindi wa Rais huyo, amekamatwa na polisi wa nchi hiyo baada ya jana kujiapisha kuwa Rais ikiwa ni siku moja tu (leo) kabla ya Museven kuapishwa.
Haijulikani ni vipi Dr Kiiza Besigye alikwepa vizuizi  vya polisi na kuibukia mjini Kampala ambapo alikutana na wandani wa chama chake na ''kula kiapo cha urais wa taifa hilo''.
Katika video inayosambaa kwenye mitandao ya kijamii Dr Besigye anaonekana ''akila kiapo'' mbele ya mtu aliyevalia mavazi sawa na ya ''jaji wa mahakama ya juu''.
Video hiyo ilisambazwa kwa kasi kwenye mitandao ya kijamii na kusababisha mamlaka inayosimamia mawasiliano nchini Uganda kuamrisha kampuni zinazotoa huduma za simu nchini humo kufunga huduma za mitandao ya kijamii
Tume ya Taifa ya Uchaguzi ilimtangaza Yoweri Museveni kuwa mshindi katika uchaguzi mkuu uliopita akiwaacha kwa mbali wapinzani wake wakuu, Kizza Besigye na Amama Mbabazi.
Kadhalika, Mahakama Kuu nchini humo ilihalalisha ushindi wa Museveni baada ya kutupilia mbali shauri la pingamizi la ushindi huo lililowasilishwa na Amama Mbabazi.


Viongozi Wakuu Wote wa Taifa Wako nje ya Nchi ..Nani Anaongoza Nchi Kwa Sasa?

Viongozi wakuu wote wa Taifa wako nje ya nchi katika ziara za kiserikali kwenye mataifa tofauti.
Rais John Magufuli aliwasili Uganda jana asubuhi kuhudhuria sherehe za kuapishwa kwa Rais mteule wa nchi hiyo, Yoweri Museveni zinazofanyika leo na Makamu wake, Samia Suluhu Hassan alikuwa Kigali, Rwanda kuhudhuria mkutano wa dunia wa uchumi.
Taarifa zilizopatikana na kuthibitishwa na Mwandishi wa Makamu wa Rais, Penzi Nyamngumi zimesema, Makamu wa Rais aliondoka nchini Jumanne akitokea Dodoma na angerejea kesho baada ya mkutano huo.
Kiongozi anayefuatia kwa wadhifa, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alisafiri juzi kwenda London, Uingereza kumwakilisha Rais Magufuli katika mkutano wa wakuu wa nchi kujadili mapambano dhidi ya rushwa.
Majaliwa katika ziara hiyo ameongozana na Jaji Mkuu, Mohamed Chande Othman.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju alipotakiwa kutoa ufafanuzi juu ya anayepaswa kukaimu urais, alisema Makamu wa Rais amekwisha rejea nchini na yuko Mwanza.
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya 37 (3), inaeleza kuwa endapo Rais atakuwa hayupo katika Jamhuri ya Muungano, kazi na shughuli za Rais zitatekelezwa na Makamu wa Rais, kama naye hayupo, yatatekelezwa na Waziri Mkuu.
Hata hivyo, Ibara ya 37 (6) (b) inasema Rais hatahesabiwa kwamba hayupo iwapo atakuwa nje ya Jamhuri ya Muungano kwa kipindi cha saa 24.