Alhamisi, 5 Mei 2016

Wabunge warushiana makonde Afrika Kusini


Wabunge nchini Afrika Kusini wamepigana bungeni baada ya spika kuamuru maafisa wa usalama kuwaondoa kwa lazima wabunge wa upinzani ambao walimbeza rais Jacob Zuma alipoingia bungeni tayari kulihutubia kikao.
Rais Zuma ambaye ameshindwa katika kesi mbili kuu zinazomhusisha na ubadhirifu wa mali ya umma na usimamizi mbaya alikuwa amefika bungeni kwa mara ya kwanza tangu kushindwa mahakamani.
Hata hivyo ujio wake uliwakera sana wabunge wa chama cha upinzani Economic Freedom Fighters (EFF).
Wabunge hao chini ya kiongozi wao Julius Malema walipiga mayowe na kumtupia matusi bw Zuma jambo lililomlazimu spika wa bunge kuamuru wabunge hao wa EFF kuondolewa nje.
Ijumaa iliyopita mahakama ya juu ya Afrika Kusini iliamua kuwa rais Zuma anapaswa kufikishwa kizimbani kufuatia kesi za ufisadi dhidi yake.
Kesi hiyo inahusiana na ufisadi uliotokea katika ununuzi wa silaha zenye thamani ya mabilioni ya dola mwaka wa 1999.
Zuma amekanusha madai yote dhidi yake, Anatarajiwa kukamilisha hatamu yake mwaka wa 2019.
Uamuzi huo wa mahakama ulikuwa msumari wa moto kwa kidonda cha Zuma ambaye mwezi uliopita alipatikana na hatia ya matumizi mabaya ya madaraka yake alipokaidi amri yakulipa pesa za umma zilizotumiwa kukarabati nyumba yake ya Nkandla.

Kampuni yatozwa Sh118 Bilioni Poda yake Kusababisha Saratani

Poda ya Johnson, iliyodhaniwa kuwa ni kipodozi na tiba mujarabu kwa watoto na watu wazima duniani kote imebainika kusababisha saratani.
Jana, Mahakama ya St Louis ya Marekani, iliiamuru kampuni inayotengeneza poda hizo, Johnson & Johnson kumlipa Deane Berg wa Sioux Falls, South Dakota, Dola za Marekani 55 milioni (Sh118 bilioni ) baada ya kujiridhisha kuwa kipodozi hicho kilimsababishia saratani ya mayai ya uzazi (ovarian cancer).
Mpaka sasa, zaidi ya wanawake 1,000 wameshafungua kesi kuishtaki kampuni hiyo kwa madai ya kuwasababishia saratani hiyo baada ya kutumia poda ya Johnson kwa miaka mingi.
Ofisa Uhusiano wa Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania, (TFDA), Gaudensia Simwanza alisema wanazo taarifa juu ya madhara ya poda hizo ingawa bado hawajathibitisha kitaalamu kwa poda zilizopo nchini.
Alisema TFDA ilishafanya uchunguzi wa kimaabara kuhusu poda hizo lakini haikuona madhara yoyote.
Simwanza alisema FDA ilitakiwa pia kuwapa taarifa watumiaji wa bidhaa hizo duniani kuhusu madhara ya poda hizo.
Mwaka 2013, Berg alikuwa mwanamke wa kwanza kuishtaki kampuni hiyo baada ya kugundulika na saratani.
Baada ya kuridhishwa na malalamiko ya Berg, Mahakama iliamuru kampuni ya Johnson & Johnson kutoa onyo kuwa poda hizo, Johnson Baby Powder na sabuni ya Shower to Shower, zinasababisha saratani. Hata hivyo, kampuni hiyo haikufanya hivyo.
Baada ya mwaka mmoja, Berg alifungua tena kesi hiyo na Mahakama iliamuru alipwe kiasi hicho cha fedha.
Daktari wa Hospitali ya Wanawake, Brigham, Daniel Cramer alitoa ushahidi mbele ya Mahakama na kueleza kuwa zaidi ya wanawake 10,000 wamegundulika kuwa na saratani ya mayai ya uzazi kwenye hospitali hiyo.
Kadhalika, wanawake hao walibainika kuwa na chembechembe za ‘talcum’ kwenye kizazi.
Daktari wa Saratani wa Taasisi ya Saratani ya Ocean Road, Herry Tungaraza alisema kuna uwezekano wa kemikali ya ‘talcum’ kupenya kwenye ngozi, hadi kwenye damu na kuingia kwenye mayai ya uzazi na kisha kusababisha saratani.
Alisema si lazima poda hizi zimuathiri mtu kwa kuzitumia sehemu za siri tu, hata kama akizitumia kwa kupaka usoni, zinaweza kusafiri na kuathiri mayai ya uzazi. “Kama ingekuwa zinadhuru kwa kuzipaka sehemu za siri tu, basi zingeathiri zaidi shingo ya kizazi au nyumba ya uzazi, lakini mayai yapo mbali na ndiyo yaliyoathiriwa na saratani,” alisema.
Shahidi mwingine wa katika kesi ya Berg alithibitisha kuwa aliona chembechembe za ‘talcum kwenye uvimbe ulioko kwenye mayai ya Berg.
Mwathirika mwingine
Mei mwaka jana, Gloria Ristesund (62), alifungua kesi dhidi ya Johnson & Johnson kwa kushindwa kuwaonya wateja wake kuhusu poda hiyo kusababisha saratani.
Ristesund aligundulika na saratani, mwaka 2011 baada ya kutumia poda hiyo kwa kuipaka sehemu za siri kwa miaka kadhaa hasa. Mahakama iliamuru Ristesund pia kulipwa Dola 55 milioni.
Tovuti ya CNN inaeleza kuwa utafiti kuhusu kemikali za ‘talcum’ kusababisha saratani ulitolewa miaka mingi nyuma lakini Johnson & Johnson hawakutaka kuweka wazi ukweli huo kwa wateja wao.
“Ni kama kampuni zinazotengeneza sigara, wanajua kuwa imeshathibitishwa kuwa uvutaji wa sigara unasababisha saratani ya mapafu lakini wanauficha umma kuhusu hili,” ilisema taarifa ya CNN.


P Diddy Aongoza Orodha ya Forbes ya Wana Hip Hop Watano Wenye Mkwanja zaidi


Forbes wametoa orodha mpya ya wasanii wa hip hop wenye fedha zaidi, The Forbes Five.
Diddy ameongoza orodha hiyo mwaka huu kwa kuwa na utajiri ufikao dola milioni 750. Nafasi ya pili imekamatwa na Dr Dre mwenye dola milioni 710 huku Jay Z akifuatia kwa dola milioni 610.
Mwanzilishi wa Cash Money, Birdman amefuatia katika nafasi ya nne akiwa na dola milioni 110. Drake amechukua nafasi ya 50 Cent na kukamata nafasi ya tano kwa utajiri wa dola milioni 60.


Majibu ya Snura baada ya Chura wake Kupigwa Nyundo na Serikali

Baada ya wizara ya habari, utamaduni, sanaa na michezo kuufungia wimbo wa Snura, Chura jana, muimbaji huyo anaonesha kutoshtushwa na hatua hiyo hasa kutokana na support anaiyopata kutoka kwa mashabiki wake.
Kwa ufupi haoneshi stress, walau kwa kile alichokiandika kwenye Instagram. “Ingekua ndio hela leo ningekua bilionea lo!!! Nawapenda sana kwakweli na nawatakia usiku mwema,” aliandika Snura kwenye Instagram.
Aliongeza hashtag: #utaipenda2_ndimuimekolea_malimao_kama__210_habarizetuwanazo_ilazaohatuna.”
Pamoja na wimbo huo kufungiwa kuchezwa kwenye redio na TV, Snura aliagizwa kuhakikisha amefuta video zake zote mtandaoni.