Hayo yote nayasema kuhusu nyota wa Bongo Fleva, Nasibu Adul Juma au
maarufu zaidi kwa jina la Diamond. Siku za hivi karibuni, Diamond
ameanzisha zoezi la kuwachukua wanamuziki na kuwaingiza kwenye kundi
lake maarufu sana la Wasafi Classic Baby ‘WCB’ ambalo limetokea kupata
jina kubwa katika Muziki wa Kizazi Kipya Bongo.
Lebo hii ya Wasafi kwa sasa inaundwa na watu wanne, Queen Darleen,
Rayvanny, Rich Mavoko na Harmonize. Awali, alianza na akina Harmonize,
Rayvanny, Rich Mavoko na mwisho ni Queen Darleen. Harmonize na Rayvanny
walikuwa hawakutamba sana kabla ya kwenda Wasafi. Mimi kwa hao, naona ni
sawa kabisa na wala sina tatizo nao.
ANAINUA VIPAJI
Katika mahojiano yake na vyombo mbalimbali vya habari hapa Bongo,
Diamond amekuwa akisema kwamba, anafanya hivyo ili kukuza muziki na
kuinua vipaji vya wanamuziki wachanga wa Tanzania. Mimi kwa hilo pia
sina tatizo naye. Pia, watu au wadau mbalimbali wa muziki huo wakawa
wanampongeza Diamond kwa kuwa, zoezi lake la kuwabeba akina Harmonize
linaongeza ushindani mkubwa katika Muziki wa Kizazi Kipya, kwamba kama
yeye anawainua hawa, wengine wakainuliwa kule, muziki utapaa. Na kwa
hili pia mimi sina tatizo nalo hata kidogo.
NI HOJA ZA MSINGI SANA
Kuna hoja za msingi kwamba, kama si Diamond, hawa akina Rayvanny
wasingekuwa hivi walivyo leo. Wasingejulikana kama wanavyojulikana
wakiwa kwa Diamond. Hiyo ni hoja ya msingi sana, tena sana. Na kwa hilo
mimi sina tatizo na hoja husika.
KUHUSU RICH MAVOKO
Katika zoezi lake la kuendelea kuchukua wasanii, Diamond akamchukua
Mbongo Fleva, Rich Mavoko ndani ya kundi lake la Wasafi. Hapa kidogo
baadhi ya watu wakahoji uhalali wa usahihi wake. Wengi waliamini kuwa,
Diamond kumchukua msanii huyo ambaye alishajenga jina kubwa katika
muziki huo ni sawa na kumpoteza njia kwani Rich Mavoko kuwa chini ya
Wasafi kunaweza kumfanya afifie kama siyo kufa kabisa kisanii.
NINACHOKIONA
Sasa ninachokiona mimi ni kwamba, nia ya Diamond inaweza kuwa nzuri sana
lakini kukatokea makosa madogomadogo kwenye kuchukua aina ya wasanii.
Yapo madai ya chini kwa chini kwamba, pia ana mpango wa kumchukua msanii
anayevuma sana kwa sasa, Darassa ambaye kibao chake cha Muziki
kimeishika nchi kwa kupigwa maeneo mbalimbali. Kama kuna ukweli wa madai
haya, naamini kuna siku tutakuja kusikia, hata Ali Kiba, Ommy Dimpoz
nani sijui, wote wana mpango wa kujiunga Wasafi. Katika hili, ninatia
shaka kwamba, lengo la Diamond kuwakusanya wasanii niliowataja na
kumchukua pia Rich Mavoko ni njia moja kwake ya kuelekea kwenye
kuudidimiza muziki wa Bongo Fleva.
Wasafi linajiimarisha kuwa kundi kubwa la muziki huo nchini. Sasa je,
ikitokea hivyo, upinzani utatoka wapi? Ninavyojua mimi siku zote, palipo
na ushindani ndipo panapokuza kitu. Ni sawa na timu za mpira wa miguu
wa Tanzani, piga mahesabu kwamba, kuna siku Simba itashuka daraja. Je,
Yanga atabaki na mshidani gani? Na kilele cha raha ya mpira wa Tanzania
ni kucheza kwa Simba na Yanga.
Ndiyo maana, makocha wa timu hizo bora wafungwe na timu nyingine zote,
lakini siyo Simba au Yanga. Hata shule wanazosoma watoto wetu siku hizi,
ubora wake inatokana na kuwepo kwa shule bora nyingine. Kama ingekuwa
shule moja tu ndiyo bora sifa yake isingekuwa na maana. Sifa ya mtu
mrefu duniani kote inatokana na kuwepo kwa mtu mfupi. Kama watu wote
wangekuwa na kimo sawa isingejulikana kama urefu ni bora.
Kuwepo kwa Wasafi kusiwe sababu ya kuwakusanya wanamuziki wengine hawa
wenye majina makubwa kwani na wao uwepo wao ndiyo changamoto ya kuwepo
kwa Wasafi. Inawezekana nia ya Diamond ikawa nzuri sana lakini mimi
naamini anakokwenda, kunaweza kuwa ndiyo kaburi la muziki wenyewe.