Ijumaa, 25 Julai 2014

KAMPENI YA UGAWAJI WA VYANDARAU VYA HATI PUNGUZO

imagesWizara ya Afya na Ustawi wa Jamii imeandaa kampeni kwa ajili ya ugawaji wa vyandarua vya hati punguzo katika kaya nchini, inayotarajiwa kuanza mwezi Aprili mwaka 2015.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Naibu Waziri wa Wizara hiyo Mhe.Dkt Kebwe Stephen, amesema kampeni hiyo imeanzishwa ili kuziba pengo kutokana na kusitishwa kwa huduma ya hati punguzo iliyokuwa ikifadhiliwa na Mennonite Economic Development Associates (MEDA) mapema mwezi Juni 2014 .

Dkt. Kebwe aliongeza kuwa  jamii pamoja na wakina akinamama wajawazito watanufaika na kampeni hiyo, ikiwemo ile ya  ugawaji wa vyandarua kwa wanafunzi shuleni ambayo imeanza kutekelezwa tangu mwaka 2013 kwa mikoa ya Lindi,Ruvuma na Mtwara.

“kampeni hii ni muhimu na ni mojawapo ya njia mbadala ya kuendelea kuwasaidia akinamama wajawazito na watoto wachanga kujikinga na ugonjwa wa malaria ikiwa ni mkakati wa kupunguza vifo vya akinamama na watoto”alisema Mhe.Dkt. Kebwe

Aidha, jumla ya vyandarua milioni 13 vimesambazwa kupitia mpango huo, ambapo imechangia katika kuongeza matumizi ya vyandarua kwa akinamama wajawazito  kutoka 16%  mwaka 2004 hadi 75% mwaka 2012 na kutoka 16% hadi 76% kwa upande wa watoto.

Pia alifafanua kuwa elimu kuhusu matumizi sahihi ya vyandarua itaendelea kutolewa Kwa watumiaji wa vyandarua hivyo, kwani baadhi ya watu wamekuwa wakitumia tofauti kwa kufugia kuku na hata wengine kuweka katika bustani ili kukinga ndege waharibifu badala ya kujikinga na mbu.

Mpango huu wa hati punguzo ni mkakati ulioendelevu kuhakikisha kuwa makundi ya akinamama wajawazito na watoto wachanga wanaendela kupata vyandarua ili kujikinga dhidi ya ugonjwa wa malaria na umekuwa ukitekelezwa kupitia ufadhili wa Mfuko wa Dunia wa Kupambana dhidi ya ugonjwa wa Ukimwi, Kifua kikuu na Malaria, Shirika la Maendeleo la Serikali ya Watu wa Marekani (USAID), Shirika la Maendeleo la Uswisi (SDC) na Idara ya Maendelao ya nchi ya Uingereza