MWANANCHI
Mbio za urais ndani ya CCM sasa
zimefikia pabaya baada ya kuibuka hofu ya kuwapo kwa mpango wa kuivuruga
Kamati Kuu kabla ya haijakutana kuchuja majina ya makada watakaotakiwa
kupigiwa kura na Halmashuri Kuu ili kumpata mgombea atakayepeperusha
bendera ya chama hicho kwenye Uchaguzi Mkuu.
Hadi sasa CCM haijatangaza ratiba yake
kwa ajili ya kuongoza wanachama wanaotaka kuwania uongozi wa ngazi
mbalimbali kwa tiketi ya chama hicho.
Hata hivyo, Kamati Kuu ya CCM itakutana
Mei 20 na kufuatiwa na vikao vya siku mbili vya Halmashauri Kuu Mei 21
na 22 kwa ajili ya kupitisha ratiba, ilani na taratibu nyingine za
uchaguzi, ikiwa ni kuashiria kuanza rasmi kwa mchakato wa uchaguzi ndani
ya chama hicho kikongwe.
Wakati chama kikitafakari kuanzisha
rasmi mchakato wa uchaguzi, tayari kuna habari kuwa moja ya makundi ya
makada wanaowania urais limeonyesha kutokuwa na imani na mwenendo wa
Kamati Kuu ambayo ina jukumu la kuchuja wanaowania urais na kupeleka
majina Halmashauri Kuu kwa ajili ya kupigiwa kura.
Taarifa zinaeleza kuwa kundi hilo
linashawishi wanachama ili wakubali kuomba kupiga kura ya kutokuwa na
imani na Kamati Kuu kwa madai kuwa inaonekana kupendelea baadhi ya
waliojitokeza na kubana wagombea wengine.
“Kuna
mkakati wa kuweka CC itakayowasaidia kwa kuwa ukishapita hapo,
umeshakuwa Rais wa nchi hii. Uzuri ukishinda ndani ya chama na
kutangazwa kuwa mgombea wao, basi makundi yote hurudi kukipigania chama
na wengine kujipendekeza ili wapewe nafasi katika serikali ijayo,”.
MWANANCHI
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadiki ameteua timu ya wahandisi kutoka Wilaya za Temeke, Ilala na Kinondoni kwa kushirikiana na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS),
kufanya tathmini ya uharibifu wa miundombinu kutokana na mvua
zinazoendelea kunyesha pamoja na kujua gharama stahiki kulirudisha jiji
katika hali yake.
Sadiki alisema kuwa baada ya kufanya
tathmini hiyo, itatoa mwanga ni kiasi gani kinahitajika ili kurudisha
miundombinu iliyoharibika katika hali yake ya kawaida.
“Siwezi
nikasema leo (jana) kuwa miundombinu iliyoharibikia itafanyiwa
matengenezo kwa kiasi hiki au kile, subirini. Nimeitisha wahandisi na
wanaendelea na kazi,” Sadiki
“ Hiki
kitu siyo cha kukurupuka kina taratibu na sheria zake inabidi zifuatwe,
hayo yote yakishakamilika wananchi wa mkoa huu watafahamishwa lini
ukarabati unaanza na kwa kiasi gani, kwani hapa hakuna siri,”.
Alisema mvua zimelivuruga jiji na kusababisha uharibifu mkubwa wa miundombinu.
Aliyataja maeneo yaliyoathirika zaidi kutokana na mvua hizo ni pamoja na Keko,
Chang’ombe Maduka Mawili, Yombo Vituka, Vingunguti, Africana, Msasani
Bonde la Mpunga, Jangwani, Manzese, Kigogo, Mburahati, Boko na Basihaya.
Licha ya kuathirika na mafuriko
yaliyotokana na mvua zilizoonyesha mfululizo kwa siku kadhaa, wakazi wa
maeneo yaliyopatwa na adha hiyo wamesisitiza kuwa hawatahama katika
makazi yao kwa sababu mafuriko yamewafuata.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na
gazeti hili walidai kuwa wameishi maeneo hayo kwa miaka mingi, wakipata
huduma zote, ikiwamo maji, umeme lakini hakukuwa na adha hiyo, huku
wakiitupia lawama Serikali kwa kushindwa kutafuta jinsi ya kuwasaidia.
MWANANCHI
Wakati viongozi wa vyama vya upinzani wakieleza hofu ya Uchaguzi Mkuu kuahirishwa, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imesitisha mchakato wa kuandikisha wapigakura mkoani Mbeya uliopangwa kufanyika kuanzia Mei 5 hadi itakapotangazwa tena.
Tayari kazi hiyo inaendelea kwenye mikoa
ya Lindi, Mtwara, Ruvuma na Iringa ambako kazi hiyo pia ilianza kwa
kusuasua, na NEC ilitarajiwa kuongeza kasi ya uandikishaji kwa kuingia
mikoa ya Dodoma, Katavi na Mbeya ambako mpango huo umesitishwa kwa muda
usiojulikana.
Kaimu Mkurugenzi wa Jiji, Dk Lazaro Samweli alisema walipewa taarifa za kusitisha uandikishaji hadi hapo watapotaarifiwa tena licha ya Tume hiyo kupeleka vifaa vya BVR.
Mwezi uliopita, Nec ilitangaza kwamba
ingeanza kazi hiyo ya kuboresha Daftari la Wapigakura mkoani hapa Mei 5,
jambo ambalo lilisababisha uongozi wa jiji utangaze nafasi za kazi ya
kuandikisha kwa wenye ujuzi wa kompyuta.
“Kabla
ya Mei 4, ofisa kutoka Tume ya Uchaguzi alikuja akatuambia tusimamishe
mchakato wa kuwapata watu wa kusimamia hadi hapo tutakapotaarifiwa,
lakini vifaa tulishavipokea, hivyo tunawasubiri wao watakavyotuelekeza
taratibu zao kwa mara nyingine tena,”Dk Samweli.
Alisema walipokea mashine 86 za BVR
kutoka NEC na kwamba mashine 15 kati ya hizo ni kwa ajili ya mafunzo ya
waandikishaji na 71 zinazosalia zitakuwa maalumu kwa kazi yenyewe ya
kuandikishia.
Viongozi wa vyama vya upinzani wamekuwa
wakituhumu kuwa kusuasua huko kwa kazi ya kuboresha Daftari la
Wapigakura ni mpango wa kutaka Serikali ya Awamu ya Nne iongezewa muda
kwa kuwa haijajiandaa kukabidhi madaraka.
Mwenyekiti wa NEC, Jaji Damian Lubuva
alisema hakuwa na taarifa za kusitishwa kwa uandikishaji mkoani Mbeya,
lakini akaongeza kuwa wananchi wanatakiwa kuwa wavumilivu kwani
uandikishaji utafanyika kama ulilovyopangwa.
“Unajua
sikuwa na taarifa hizo kwa sababu nilikuwa katika kikao na wenyeviti
wenzangu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki
(EAC). Kama kweli limesitishwa, itakuwa ni mchakato mdogo wa maandalizi
haujakamilika. Ila niwatoe hofu wakazi wa mkoa huo uandikishaji
utafanyika kama ulivyopangwa,” Jaji Lubuva.
MWANANCHI
Siku moja baada ya Ikulu kutangaza kuwasafisha mawaziri watano na Katibu Mkuu, Eliackim Maswi, wabunge wamejiweka pembeni na suala hilo wakisema Bunge lilishatimiza wajibu wake.
Juzi, Ikulu iliwasafisha mawaziri wanne
walioshinikizwa kuachia ngazi na Bunge kutokana na kuhusishwa na sakata
la Operesheni Tokomeza Ujangili na mmoja aliyejiuzulu kutokana na kashfa
ya uchotwaji wa Sh306 bilioni kutoka Akaunti ya Tegeta Escrow, pamoja
na katibu mkuu wa wizara.
Waliotangazwa na Ikulu kuwa safi ni Emmanuel Nchimbi, aliyekuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa na Shamsi Vuai Nahodha,
aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani. Wawili hao wanatajwa kwenye
kinyang’anyiro cha urais kwa tiketi ya CCM ingawa hawajatangaza nia.
Wengine ni aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Hamis Kagasheki na aliyekuwa Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, David Mathayo.
Hali kadhalika, Profesa Sopster Muhongo
aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini ambaye alijiuzulu kutokana na
kashfa ya escrow, pamoja na katibu mkuu wa wizara hiyo, Eliackim Maswi
aliyesimamishwa kutokana na sakata hilo, wametangazwa kuwa safi.
Waziri Kivuli wa Maliasili na Utalii, Mchungaji Peter Msigwa
alisema kitendo cha Serikali kutangaza kuwa mawaziri hao hawakuhusika
katika kutekeleza makosa yaliyotokana na Operesheni Tokomeza,
kinaonyesha nia ya kuendeleza tabia ya viongozi kutopenda matatizo
yaliyotokea wakiwa madarakani.
“Kilichofanyika
ni kuionyesha dunia kuwa hakuna kuwajibika, unapopewa jukumu lazima
uwajibike. Sijui Taifa hili linakwenda wapi? Nakosa hata maneno ya
kuzungumza,” Msigwa.
Mbunge wa viti maalumu (CCM), Esther Bulaya alisema kuwa katika taarifa hakuna kipya kwani haina tofauti na ile ya Kamati ya Bunge iliyoundwa kuchunguza suala hilo.
“Jana
(juzi) nilimsikiliza kwa makini sana (Katibu Mkuu Kiongozi) Balozi Sefue
wakati akitoa taarifa hiyo kwa waandishi wa habari ila kichwani
lilinijia swali moja tu; hivi madai yaliyotolewa na wananchi katika tume
iliyoundwa kuchunguza jambo hili ya kweli au si kweli?” Bulaya.