WAKATI wapinzani wakipinga uteuzi wa Waziri wa Nishati na
Madini, Profesa Sospeter Muhongo, waziri huyo amewasihi wananchi
kumvumilia kidogo, ili baada ya muda mfupi atoe mpango wa maendeleo ya
wizara hiyo, ambao pamoja na mambo mengine, utaelezea bei ya nishati
hiyo itakavyoshuka.
Akizungumza na waandishi wa habari muda mfupi baada ya
kuapishwa kushika wadhifa huo jana Ikulu jijini Dar es Salaam, Profesa
Muhongo alisema mbali na mkakati wa kushusha bei ya umeme, kasi ya
kusambaza umeme vijijini kupitia miradi ya Wakala wa Nishati Vijijini
(REA), itarejea palepale.
“Nimepokea uteuzi huo, kinachofuata ni kuwatumikia
wananchi, niwaombe tu wanivumilie kidogo nitawapa mpango wangu wa
maendeleo wa muda mfupi na mrefu, lakini nisisitize tu nishati sio
siasa, ni suala la utaalamu, liachwe lifanywe kitaalamu,” alisema Profesa Muhongo.
Akizungumzia bei ya umeme na upatikanaji wake, Profesa
Muhongo alisema kupunguza bei hiyo ni ajenda muhimu itakayozingatiwa na
kusema ili umeme uwe wa uhakika, ni lazima kuwe na mipango ya kuwa na
nishati hiyo ya uhakika ifikapo mwaka 2025.
“Umeme wa uhakika utapatikana na matarajio yetu ni
Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025 ambapo
tunatarajia uzalishaji wa nishati hiyo ufike Megawati 10,000 hadi
15,000,”alisema Profesa Muhongo.
Alisisitiza kwamba wizara yake haitategemea chanzo kimoja
cha nishati bali wataangalia vyanzo vingine ikiwemo nishati jadidifu,
upepo, gesi, makaa ya mawe, maji huku akisema vyanzo hivyo vikitumika
kuzalisha nishati, ni wazi bei ya umeme itashuka na kushusha gharama
nyingine za maisha na za uwekezaji.
Aliongeza katika kuendeleza sekta ya nishati suala la
uwekezaji ni muhimu hivyo wizara yake inakaribisha wawekezaji wenye
sifa, watakaowekeza kwenye sekta hiyo ili kuja na matokeo bora zaidi,
wananchi wanufaike na rasilimali za nchi yao.
Pamoja na nia yake hiyo kwa wananchi, Profesa Muhongo
anakabiliwa na pingamizi kutoka kwa wanasiasa wa vyama vya upinzani,
akiwemo Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema) na aliyekuwa
Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba.
Lissu na Profesa Lipumba, wamekaririwa wakikosoa uteuzi wa
Profesa Muhongo kwa madai kuwa wizara aliyopewa kuiongoza, ilikumbwa na
kashfa ya Akaunti ya Tegeta Escrow wakati wa uongozi wake, ikasababisha
ajiuzulu.
Hata hivyo, Profesa Lipumba na Lissu katika kukosoa huko,
hawakutaka kutumia kumbukumbu zilizo wazi kuwa uchunguzi dhidi ya
Profesa Muhongo, ulibaini kuwa hakukiuka maadili yoyote katika sakata la
utoaji wa karibu Sh bilioni 300 zilizokuwa katika akaunti ya Tegeta
Escrow, iliyokuwa Benki Kuu (BoT).
Matokeo ya uchunguzi huo yalitangazwa Mei mwaka huu na
Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, ambapo alisema Tume ya
Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, ndiyo ilifanya uchunguzi
kama Profesa Muhongo alistahili kwenda kwenye Baraza la Maadili kujibu
mashitaka, lakini hawakuona tatizo lake na kufunga shauri lake.
Balozi Sefue aliweka wazi kuwa Profesa Muhongo alijiuzulu
kwa sababu za kisiasa, lakini kimaadili hakuhusika kwa namna yoyote,
kutokana na uchunguzi wa Sekretarieti ndiyo sababu hakufikishwa katika
Baraza la Maadili.
Kitu kingine ambacho Lissu na Profesa Lipumba, hawakutaka
kuzungumzia ni utendaji wa Profesa Muhongo alipokuwa katika wizara
wakati wa uongozi wa Serikali ya Awamu ya Nne, chini ya Rais mstaafu
Jakaya Kikwete.
Kumbukumbu zinaonesha kuwa katika miaka miwili ya uongozi
wake katika Wizara ya Nishati na Madini, Profesa Muhongo alisimamia kwa
umahiri usambazaji wa umeme vijijini.
Kabla ya kuteuliwa kwa Profesa Muhongo, Watanzania asilimia
14 tu ndio waliokuwa wakitumia nishati ya umeme, kati yao asilimia 12
walikuwa watumiaji wa mijini na asilimia mbili ndio walikuwa watumiaji
wa vijijini.
Kwa mujibu wa takwimu za Serikali, kati ya mwaka 2007 na
mwaka 2010, kulikuwa na ongezeko la asilimia nne la watumiaji wa umeme,
hali iliyoonesha kuwa ongezeko la Watanzania waliokuwa wakipata umeme,
lilikuwa asilimia moja kwa mwaka.
Lakini baada ya kuteuliwa kwa Profesa Muhongo katika nafasi
hiyo, katika muda mfupi wa uongozi wake, idadi ya Watanzania wanaotumia
umeme iliongezeka na kufikia asilimia 36 katikati ya mwaka jana.
Kwa hatua hiyo, uongozi wa Profesa Muhongo ulivuka malengo
ya Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambayo ndio msingi wa utekelezaji
wa malengo ya Serikali, iliyotaka Serikali kuhakikisha ifikapo mwaka
2015, asilimia 30 ya Watanzania wawe wanapata umeme.
Katika kutimiza malengo ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya
2010, uongozi wa Profesa Muhongo, ulitangaza punguzo la gharama za
kuunganisha umeme majumbani kutoka Sh 177,000 za awali hadi Sh 27,000
vijijini.
Awali, punguzo hilo lilitolewa kwa mikoa ya Lindi na
Mtwara, ambako bomba la kusafirisha gesi kwenda Dar es Salaam limeanzia
na limepita, lakini baada ya muda gharama hizo zilishushwa kwa vijiji
vyote nchi nzima.
Profesa Muhongo mwenyewe alikaririwa akisema gharama hizo
zitahusu miradi inayosimamiwa na Wakala wa Umeme Vijijini (REA), katika
kipindi ambacho makandarasi watakuwa wakiendelea na awamu ya pili ya
miradi iliyoanza Machi mwaka huu na kutarajiwa kukamilika katikati ya
mwakani.