Wakati Baraza la Usuluhishi la Benki ya Dunia likitoa hukumu ya kutaka
Tanesco kuilipa Benki ya Standard Chartered-Hong Kong (SCB-HK) Sh320
bilioni, wanasiasa wawili walioibua sakata hilo bungeni wamechachamaa
wakimtaka Rais John Magufuli awafikishe mahakamani wote waliohusika
katika sakata la escrow.
Katika hukumu hiyo, Baraza hilo limeitaka Tanesco kulipa mamilioni hayo
ya fedha baada ya mgogoro wa muda mrefu kati yake na Kampuni ya
Independent Power Tanzania Ltd (IPTL).
Uamuzi huo umekuja wakati Serikali ilisharuhusu kufanyika kwa malipo ya
Sh306 bilioni kutoka katika akaunti ya Tegeta Escrow iliyokuwa
imefunguliwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwa ajili ya sakata hilo kwenda
kwa kampuni ya Pan Africa Power Solutions (T) Ltd (PAP).
Kaimu Meneja Uhusiano wa Tanesco, Leila Muhaji alisema katika shauri
hilo, shirika hilo liliwakilishwa na mawakili binafsi kutoka kampuni ya
uwakili ya Rweyongeza na ndiyo itakayotoa taarifa kuhusu hukumu hiyo.
Maoni ya
Zitto
Akizungumzia hukumu hiyo, Mbunge wa Kigoma Mjini,
Zitto
Kabwe alisema: “Rais Magufuli awachukulie hatua wote waliohusika kuitia
hasara Serikali kwa kuruhusu kufanyika kwa malipo ya Tegeta Escrow.”
Alisema benki iliyotumika kupitisha fedha za Tegeta Escrow ndiyo ilipe deni hilo ambalo linatakiwa kulipwa na Tanesco.
Mbunge huyo aliyeongoza kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC)
kuchunguza sakata hilo, alisema Rais Magufuli aitwae mitambo ya IPTL
kisheria na kuimilikisha kwa Tanesco kama ilivyopitishwa katika maazimio
ya Bunge.
“Pia wamkamate Harbinder Singh Seth, mmiliki wa PAP na wafuasi wake wote
na kuwafikisha mahakamani kujibu tuhuma zinazohusiana na sakata hilo,”
alisema.
Zitto alisema: “Rais Magufuli aamue ama kusimama upande wa Watanzania au Tegeta Escrow.”
Alisema haiwezekani Tanesco ikaingia hasara kwa sababu ya uchotaji wa
fedha za escrow na Rais akaacha kuwachukulia hatua waliohusika.
Kiongozi huyo wa Chama cha ACT – Wazalendo alisema, “Inasikitisha
kuwalipa watu fedha zilizokuwa kwenye akaunti hiyo na kuwapa mitambo ya
kuzalisha umeme huku mkiendelea kuwalipa gharama za uwekezaji.”
Aliongeza, “Sasa mnawalipa Standard Chartered Bank fedha zao kwa mtambo
ambao siyo wenu kwa fedha ambazo mngezitoa kwenye akaunti hiyo, lakini
sasa mnazitoa Hazina, inasikitisha.”
Kauli ya Kafulila
Aliyeibua sakata hilo, David Kafulila alisema hukumu iliyotolewa wiki
iliyopita ilitarajiwa kwa kuwa walishaeleza kuwa aliyelipwa fedha za
escrow hakuwa mwenye fedha hizo.
“Leo vinara waliokuwa wakitetea IPTL bado ni vinara katika Serikali ya
Magufuli, fedha za escrow hazikuwa za IPTL sasa tunaingia gharama
nyingine, Sh300 bilioni ni lazima tufahamu nani yuko nyuma ya mzimu huu
wa escrow,” alisema mbunge huyo wa zamani wa Kigoma Kusini.
Kafulila aliungana na
Zitto
kumuomba Rais Magufuli kuwakamata wahusika wote na kuwafikisha
mahakamani. “Bunge liombe ripoti ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na
Rushwa (Takukuru) iwekwe wazi kuhusu Akaunti ya Tegeta Escrow,” alisema.
Alitaka maazimio yote ya Bunge yatekelezwe kwa kuwa bado mengi hayajatekelezwa.
“Hii ni hasara kubwa na inatufunga kisheria, lazima tulipe kama
ilivyokuwa Dowans walipotushinda tukalipa Dola za Marekani 94 milioni
sawa na Sh200 bilioni na hizi tutazilipa iwe kwa uwazi au kwa siri.
“Inaumiza sana kwa sababu kodi ya wananchi italipa fedha ambazo
zingetumika kutatua matatizo ya wananchi katika kilimo, maji, elimu na
maeneo mengine.”
Alisema Serikali ililipa fedha hizo Novemba 2013 wakati ikijua bado kuna
mgogoro. “Kulikuwa na haraka gani kutoa fedha hizo badala ya kusubiri
uamuzi wa Baraza hilo,” alisema.
Kafulila aliwaomba wabunge kuendelea kupambana bila woga ili waliohusika na ufisadi huo wachukuliwe hatua za kisheria.