Uamuzi
wa Rais John Magufuli kukaa zaidi ya mwezi mmoja bila kuteua Baraza la
Mawaziri huenda ukawa umeisaidia Serikali kwa kuokoa takribani Sh683.3
milioni za walipa kodi, bila kuhusisha gharama za ununuzi wa
‘mashangingi’.
Kiasi
hicho cha fedha kimetokana na hesabu inayokadiriwa kuwa matumizi ya
waziri iwapo Rais Dk Magufuli angeendelea na ukubwa wa Baraza la
Mawaziri la mwisho la Rais Jakaya Kikwete la mawaziri 55, kati ya hao 24
wakiwa manaibu waziri.
Hata
hivyo, Dk Magufuli ameshatangaza kuwa na baraza dogo la mawaziri,
ingawa hajaweka bayana litakuwa na jumla ya mawaziri wangapi.
Kwa
mujibu wa aliyekuwa Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya
Makazi, Goodluck Ole-Medeye, Waziri hulipwa mshahara wa kati ya
Sh3.8milioni mpaka Sh 5milioni kwa mwezi ambazo ni sawa na mshahara
wanaolipwa wabunge.
Kwa
mantiki hiyo, kwa mawaziri 55, Serikali ilitakiwa ilipe Sh209 milioni
kwa ajili ya mishahara ya Novemba, lakini hazikulipwa kwa kuwa bado
kiongozi huyo hajawateua.
Kanuni
za kudumu za utumishi wa umma toleo la mwaka 2009, zinaitaka Serikali
kumpatia nyumba mtumishi anayetakiwa kupatiwa huduma hiyo kwa aidha
kumpa nyumba ya Serikali au kumkodishia nyingine yenye hadhi ili aweze
kutimiza wajibu wake ipasavyo.
Kanuni
hizo zinamtaka Wakala wa Majengo (TBA) kufanikisha zoezi hilo la kutoa
huduma za nyumba au kusimamia ukodishaji wa nyumba husika ya mtumishi.
Mawaziri
ni miongoni mwa watumishi wanaopatiwa nyumba za Serikali ambazo nyingi
zinapatikana katika maeneo ya vigogo ya Masaki, Oysterbay au Mikocheni
jijini Dar es Salaam.
Kwa
mujibu wa tovuti ya uuzaji na ukodishaji nyumba na viwanja ya Lamudi,
nyumba za bei ya wastani ambayo inaweza kwenda na hadhi ya waziri
inakodishwa kwa kiasi kisichopungua Sh5 milioni kwa mwezi.
Hivyo
basi, kama nyumba za mawaziri hao ambazo hukarabatiwa na kuhudumiwa na
TBA, zingekuwa zimekodishwa kutoka kwa watu binafsi kwa kipindi cha
mwezi mzima basi Serikali ingelipa Sh275 milioni.
Ili
kutimiza majukumu yao vyema wakiwa bungeni mjini Dodoma, mawaziri pia
hupatiwa nyumba za kuishi tofauti na zile za Dar es Salaam ambazo zipo
chini ya TBA.
Hata
hivyo, Ole-Medeye alisema Serikali huwalipa mawaziri Sh800, 000 kwa
mwezi kwa ajili ya huduma za nyumba za Dar es Salaam, mawasiliano na
ankara nyingine za kumsaidia kimaisha.
Iwapo
kiwango hicho cha Sh800, 000 kwa mwezi kingetumika kumlipa kila waziri
kama sehemu ya fedha za makazi, bado Serikali ingehitajika kutoa Sh44
milioni kwa ajili ya gharama za kuhudumia nyumba na mawasiliano.
“Hivi
Sh800, 000 utapata wapi nyumba ya kukodi akaishi waziri? Kwa bei ya
sasa nyumba za kiwango hicho ni Dola za Marekani 3,000 (Sh6 milioni) au
zaidi.
“Sasa
fedha hiyo umlipe mtumishi wa ndani, gharama za umeme, mawasiliano na
maji ndiyo maana nasema uwaziri ni kazi ya kuhudumia jamii,” alisema
Ole-Medeye akieleza kuwa waziri hupatiwa posho ya Sh80, 000 kwa siku
akiwa mikoani kwenye ziara.
Gharama
za posho za mawaziri hao zingetegemea na siku ambazo wangekaa mikoani
kwa kipindi hicho cha siku 31, na hivyo si rahisi kujua kiwango chake.
Gharama za samani
Miongoni
mwa mambo ambayo Serikali hugharamia kwa mawaziri wake ni samani za
ndani ya nyumba, ambazo pia huongezeka au kupungua kulingana na ukubwa
wa baraza.
Katibu
Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dk Adelhelm Meru alisema ununuzi
wa samani za ndani ya nyumba za waziri husimamiwa na Mamlaka ya
Udhibiti wa Manunuzi ya Umma (PPRA) kwa wizara zote na hununuliwa kila
baada ya miaka mitano.
Hata hivyo, Dk Meru alitoa angalizo kuwa matumizi ya waziri husika huchangiwa pia na ukubwa wa wizara na kiwango cha bajeti.
“Mawaziri wengine wanaishi kwenye makazi yao na siyo wote wamepewa makazi ya Serikali.
“Lakini wanapewa huduma ya umeme, maji, posho ya majukumu na gari,” alisema Dk Meru.
Mashangingi
Mawaziri
pia hupatiwa magari kwa ajili ya usafiri na mara nyingi huwa na ama
Toyota Land Cruiser VX V8 au GX V8 ambayo hujulikana kama “mashangingi.”
Ili
kufanikisha shughuli zao, kila waziri hupatiwa lita 1,000 kwa mwezi za
mafuta. Kwa bei elekezi ya sasa ya Mamlaka ya Udhibiti wa huduma za
Nishati na Maji (Ewura), iliyoanza kutumika Desemba 2, bei ya dizeli
jijini Dar es Salaam ni Sh1,823 kwa lita.
Gari
moja la waziri mmoja iwapo lingetumia lita zote 1,000 Serikali
ilitakiwa kulipa Sh1.823 milioni ambazo kwa baraza zima ingekuwa jumla
ya Sh100.3 milioni.
Pia, magari hayo huitaji kufanyiwa matengenezo kwa kila baada ya kilomita zinazoshauriwa na mtengenezaji.
Dk
Meru alisema kwa kawaida kila gari hufanyiwa matengenezo baada ya
kilomita 5,000 kwa kiasi cha wastani Sh1.8 milioni kila moja.
Kwa
maana hiyo, katika Serikali ya “hapa kazi tu” inayohimiza viongozi wa
kutoka maofisini kwenda kusikiliza shida za wananchi vijijini, hapana
shaka kuwa mawaziri hao wangekuwa ama wameshatimiza kilomita
zinazohitaji matengenezo au wanakaribia.
Serikali kufanikisha matengenezo hayo, ingeweza kulipa kampuni husika ya matengenezo Sh99 milioni kwa mwezi.
Gharama
hizo ni mbali na fedha za kununua magari hayo ambayo kila moja
linakadiriwa kugharimu Sh250 milioni, hivyo mawaziri 55 wangetafuna
Sh13.75 bilioni.
Unafuu
wa gharama katika eneo la ununuzi wa mashangingi hayo utakuwa dhahiri
iwapo Rais Magufuli atatekeleza ahadi yake ya kuteua baraza dogo,
mathalan, akiteua mawaziri 20 atakuwa ameokoa mashangi ya mawaziri 35,
sawa na Sh8.75 bilioni.
Ukimya
wa Rais Magufuli kutoteua Baraza la Mawaziri kwa kipindi cha mwezi
kumeibua mtizamo tofauti miongoni mwa wachambuzi wa masuala ya Siasa na
utawala, wengi wakisema kuna faida nyingi kuliko hasara.
0 comments:
Chapisha Maoni