Wakati
Watanzania wakisubiri kufahamu sura zitakazoingia kwenye baraza jipya
la mawaziri katika Serikali ya Rais John Magufuli, baadhi ya mawaziri wa
awamu iliyopita ya Jakaya Kikwete hawajaziachia nyumba za Serikali
walizokuwa wanaishi.
Kwa
mujibu wa Kanuni za Utumishi wa Umma, mawaziri wanastahili kuishi
kwenye nyumba za Serikali kuanzia pale uteuzi wao unapotangazwa ili
kuanza kutekeleza majukumu yao wakiwa katika mazingira salama, wao na
familia zao. Haki hiyo hukoma mara moja; pale wanapovuliwa wadhifa huo
au baraza husika linapovunjwa baada ya kukamilisha muhula wake au sababu
nyingine yoyote.
Maandalizi
ya Rais Magufuli katika uteuzi yanakwenda sambamba na taasisi
zinazohusika kutekeleza wajibu wao wa kuandaa makazi ya wateule
wanaotarajiwa, lakini zinakwamishwa na mawaziri ambao hawajahama.
“Tumepata
fedha za kutosha kukarabati nyumba zenye uhitaji huo kutoka wizarani.
Nyumba 15 zipo katika utekelezaji. Kuna baadhi tunasubiri waliomo wahame
ili tuweze kuendelea,” alisema Mhandisi Edwin Nnunduma, kaimu
mkurugenzi wa ushauri wa Wakala wa Nyumba za Serikali Tanzania (TBA).
Nnunduma
alisema kila kitu kipo tayari na mapokezi ya viongozi hao
hautacheleweshwa kwa namna yoyote ile kwa kuwa nyumba zipo za kutosha
kuwahifadhi ili walitumikie Taifa kwa viwango vinavyohitajika.
Takwimu
zinaonyesha kuwa wakala huyo anasimamia jumla ya nyumba 93 na kati ya
hizo 29 zilikuwa zinakaliwa na mawaziri wa Serikali iliyopita ya Rais
Jakaya Kikwete ambao, kwa mujibu wa kanuni walistahili kuziachia mara tu
baada ya Rais Magufuli kuapishwa, Novemba 5.
Kwa
mujibu wa Nnunduma, ukarabati huo unahusisha nyumba 35 ambazo
zinajumuisha 29 za mawaziri na sita wanazoishi baadhi ya makatibu wakuu
wa wizara.
Taarifa
zilizolifikia Mwananchi zinaeleza kuwa wapo baadhi ya mawaziri ambao
wamekaidi kuondoka kwenye nyumba hizo, licha ya kanuni na sheria
kuwataka kufanya hivyo na agizo la Katibu Mkuu Kiongozi lilikwishatolewa
likiwataka kurudisha magari na nyumba za Serikali.
Alipoulizwa
kuhusu suala hilo, Mnunduma alisema, “Kuna waraka wa Katibu Mkuu
Kiongozi uliowataka wahame kwenye nyumba hizo ndani ya siku 30 baada ya
kuapishwa kwa Rais mpya. Muda huo uliisha jana (juzi), naamini bado
baadhi hawajahama mpaka sasa. Nilikuwa safarini hivyo sina uhakika ni
nani na nani hawajafanya hivyo.”
Novemba
5, mara baada ya kuapishwa kwa Rais Magufuli, Katibu Mkuu Kiongozi,
Ombeni Sefue, aliwaagiza mawaziri na manaibu waziri kurudisha magari ya
Serikali ikiwa ni siku yao ya ukomo wa uongozi. Katika agizo hilo,
alisema baada ya bendera ya Rais anayemaliza muda wake kuteremshwa na
kabla ya ile ya Rais mpya kupandishwa, magari hayo yanatakiwa
yabadilishwe namba kwa kuondoa herufi ya cheo na kuwekwa zile za
Serikali.
Wakati
urejeshaji wa magari ulifanywa mara moja, uhamaji kwenye nyumba za
Serikali ulipewa muda wa siku hizo 30, ili kutoa fursa kwa familia
husika kuandaa mazingira hayo ikiwa ni pamoja na kusafirisha mali husika
za viongozi hao na walio nao.
Kukawia
huko kwa baadhi ya mawaziri kunaelezwa kuwa huenda kukawa na sababu
mbili; ama uhakika wa kurudi kwenye baraza jipya au kutokana na ukosefu
wa mahali pa kuhamia baada ya utumishi kukamilika na muda wa kutafuta
mahali pengine penye hadhi sawa na yao kuwa changamoto.
“Wapo
baadhi ya mawaziri ambao walichaguliwa siku za mwisho ambao kabla ya
hapo walikuwa wanaishi majimboni kwao. Mwezi mmoja uliotolewa unaweza
usitoshe kwa wao kutafuta nyumba nyingine hapa mjini itakayowafaa
kulingana na mahitaji yao,” kilisema chanzo ambacho hakikutaka kutajwa.
Uchunguzi
wa gazeti hili katika mitaa Mikocheni, Masaki na Kijitonyama ziliko
nyumba za mawaziri ulibaini baadhi zikifanyiwa ukarabati na baadhi ya
walinzi waliohojiwa wakibainisha kuwa mawaziri wengi walishaondoka
katika makazi hayo.
Hata
hivyo, ofisa wa TBA anayeshughulikia makazi ya mawaziri Kanda ya
Masaki, Juma Hamis alisema mawaziri waliokuwa wamebakia kwenye eneo lake
ni Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Januari Makamba
na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Tamisemi, Hawa Ghasia.
“Kwa taarifa nilizonazo, hawa mawaziri wanahama leo (jana) kwani tayari wameanza kuhamisha baadhi ya vitu vyao,” alisema Juma.
Hata
hivyo, Makamba alipoulizwa alisema hajawahi kuishi kwenye nyumba ya
Serikali tangu aanze kuwatumikia wananchi kwa nafasi tofauti alizowahi
kuzitumikia.
Alisema, “Siku zote naishi kwenye nyumba yangu. Tangu nilipokuwa ikulu na hata nilipoondoka na kuwa waziri.”
0 comments:
Chapisha Maoni