Ijumaa, 16 Septemba 2016

KUTOKA BUNGENI: RAISI MAGUFULI KUHAMIA DODOMA RASMIMWAKA 2020



Leo Septemba 16, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akisoma hotuba ya kuahirisha mkutano wa nne kwa Bunge la 11 uliodumu kwa muda wa wiki mbili, amesoma ratiba ya serikali kuhamia Dodoma.

“Ili kufanikisha azma ya Serikali kuhamia Dodoma, tayari imeandaliwa ratiba itakayowezesha Serikali kuhamia Dodoma kwa awamu, kuanzia mwezi Septemba, 2016 hadi mwaka 2020, bila ya kuathiri bajeti yetu ya mwaka 2016/2017 kama ifuatavyo”–


1. Septemba 2016 – Februari 2017.

Waziri Mkuu na Mawaziri wote, Makatibu Wakuu wote, Manaibu Makatibu Wakuu wote watahamia Dodoma katika Awamu ya Kwanza. Aidha, kila Wizara itatakiwa kuhamisha Watumishi wa Idara moja au mbili, na wakati huo huo kuendelea kuweka utaratibu wa kupeleka Watumishi wa Idara nyingine kuhamia Dodoma;

2. Machi 2017 – Agosti 2017.

Kipindi hiki kitawapa fursa watendaji wa wizara mbalimbali kuweka katika Bajeti zao za mwaka 2017/2018 gharama za kuendelea kuhamisha watumishi wake kuja Dodoma.

3. Septemba 2017 – Februari 2018.

Katika awamu hii, Wizara zitaendelea na uhamishaji wa Watumishi wa Idara zilizo ndani ya Wizara.

4. Machi 2018 – Agosti 2018.

Katika kipindi hiki, Wizara zinatakiwa kuendelea kuhamisha watumishi wake.

5. Septemba 2018 – Februari 2020.

Katika kipindi hiki, Wizara zinatakiwa kuendelea kuhamisha watumishi wake.

6. Machi 2020 – Juni 2020.

Katika kipindi hiki, Ofisi ya Rais ikiongozwa na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, watakuwa wanahamia Dodoma.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alitumia wasaa huu kuzishauri Wizara zote kuanzisha mifumo ya utunzaji kumbukumbu wa kielektroniki badala ya kuhama na mafaili kutoka Dar es Salaam kuja Dodoma, tunataka Dodoma iwe ya kielektroniki, alisisitiza Waziri Mkuu.

0 comments:

Chapisha Maoni