Mtanzania anayefanya vizuri kwenye mchezo wa kickboxing Emmanuel Shija hivi karibuni ataipeperusha bendera ya Tanzania nchini Uganda wakati atakapopanda ulingoni kupambana na Mganda Moses Golola katika pambano la kuwania ubingwa wa Afrika Mashariki na Kati katika mchezo wa Kickboxing.
Pambano hilo linatarajiwa kufanyika nchini Uganda mwishoni mwa wiki hii huko Jinja kwenye ukumbi wa Hoteli ya Crested Crane ambapo bondia toka Uganda Moses Golola amekuwa akijitamba kumpiga Mtanzania huyo ambaye kwa upande wake amekuwa mkimya akichagua kutojisifia sana na badala yake kufanya mazoezi ya nguvu ili aonyeshe uwezo wake siku ya pambano .
Shija ana rekodi nzuri inayoonyesha kuwa katika mapambano 28 amefanikiwa kushinda mara 25 huku akipoteza mara tatu na hajatoka sare hata mara moja .
Moses Golola amekuwa na kawaida ya kujisifu kwa mbwembwe nyingi kabla ya mapambano yake hali ambayo mwenyewe anadai inamsaidia kuwatia hofu wapinzani wake na kumpa faida ya kupata ushindi hata kabla ya kupanda ulingoni kwa kuwafanya wapinzani wake wapoteze hali ya kujiamini .
Mganda huyo amepanda ulingoni mara 24 ambapo amefanikiwa kushinda katika mapambano 19 huku akipoteza mara 4 pekee na katika michezo hiyo amefanikiwa kushinda mara 11 kwa mtindo wa Knock-Out.
Mara ya mwisho katika pambano lake Moses Golola alichakazwa na Mmarekani Richard Abraham katika pambano lililofanyika nchini Uganda .
Emmanuel Shija ambaye hafahamiki sana miongoni mwa Watanzania , amekuwa akifanya vizuri katika mapmbano yake ambayo karibu yote yamekuwa yakifanyika nje ya nchi kwenye mataifa kama Falme za kiarabu na Hispania ambako amejijengea jina kubwa .
0 comments:
Chapisha Maoni