Shilingi billion 473 zimetengwa kwa ajili ya kutoa mikopo
kwa wanafunzi wa elimu ya juu nchini kwa mwaka huu ikilinganishwa na
Shilingi bilioni 341 zilizotolewa mwaka jana ikiwa ni ongezeko la Tsh.
bilioni 132 katika bajeti ya mwaka huu.
Hayo yalisemwa jana jijini Dar es salaam na Mwenyekiti wa
shirikisho la wanafunzi wa vyuo vikuu Tanzania(Tahliso) bwn.
Nzilanyingi John alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu
kuaandaa mdahalo kujadili hotuba ya Rais Dkt. John Magufuli aliyoisoma
Dodoma wakati wa ufunguzi wa bunge la kumi na moja .
Alisema kuwa kwa kipindi kifupi kumekuwa na mabadiliko ya
haraka yaliyotokea katika sekta ya elimu nchini kwa mwaka huu kwani
kuna ongezeko la zaidi ya wanafunzi 1800 waliopata mkopo ikilinganishwa
na mwaka uliopita ambapo ni wanafuzi 34128 pekee ndio waliofanikiwa
kupata mkopo.
“Mpaka sasa jumla ya wanafunzi 51,675 wa mwaka wa kwanza
wamepata mkopo na lengo ni kufikia 53,032, pia jumla ya wanafunzi 91 wa
shahada ya uzamili na wanafunzi 113 wanaosoma vyuo vya nje tayari
wamepata mkopo” alisema John.
Aliongeza kuwa katika kipindi kifupi kijacho bodi ya mikopo
imehakikisha kutoa mikopo kwa wanafunzi zaidi ya elfu moja wanaochukua
Diploma maalumu ya ualimu Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) na hivyo
kukamilisha adhma yao ya kutoa mikopo kwa wanafunzi 53,032.
Aidha shirikisho hilo ambalo ni umoja wa viongozi wa
serikali za wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu nchini umeandaa mdahalo
wenye lengo la kutoa fursa kwa watanzania wengi kujadili hotuba hiyo na
namna rais alivyoanza kutekeleza majukumu yake katika nafasi hiyo.
Mdahalo huo utafanyika jijini Dar es Salaam tarehe 13 mwezi
huu katika ukumbi wa Nkurumah na wazungumzaji wakuu katika mdahalo ni
Mtaalamu mbobevu wa uchumi kutoka chuo kikuu cha Mzumbe Prof.Honest
Ngowi, Dkt. John Lingu kutoka Idara ya Sayansi ya Siasa ya Chuo Kikuu
cha Dar es Salaam na Mwanadiplomasia Christopher Liundi.
0 comments:
Chapisha Maoni