Alhamisi, 12 Mei 2016

Viongozi Wakuu Wote wa Taifa Wako nje ya Nchi ..Nani Anaongoza Nchi Kwa Sasa?

Viongozi wakuu wote wa Taifa wako nje ya nchi katika ziara za kiserikali kwenye mataifa tofauti.
Rais John Magufuli aliwasili Uganda jana asubuhi kuhudhuria sherehe za kuapishwa kwa Rais mteule wa nchi hiyo, Yoweri Museveni zinazofanyika leo na Makamu wake, Samia Suluhu Hassan alikuwa Kigali, Rwanda kuhudhuria mkutano wa dunia wa uchumi.
Taarifa zilizopatikana na kuthibitishwa na Mwandishi wa Makamu wa Rais, Penzi Nyamngumi zimesema, Makamu wa Rais aliondoka nchini Jumanne akitokea Dodoma na angerejea kesho baada ya mkutano huo.
Kiongozi anayefuatia kwa wadhifa, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alisafiri juzi kwenda London, Uingereza kumwakilisha Rais Magufuli katika mkutano wa wakuu wa nchi kujadili mapambano dhidi ya rushwa.
Majaliwa katika ziara hiyo ameongozana na Jaji Mkuu, Mohamed Chande Othman.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju alipotakiwa kutoa ufafanuzi juu ya anayepaswa kukaimu urais, alisema Makamu wa Rais amekwisha rejea nchini na yuko Mwanza.
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya 37 (3), inaeleza kuwa endapo Rais atakuwa hayupo katika Jamhuri ya Muungano, kazi na shughuli za Rais zitatekelezwa na Makamu wa Rais, kama naye hayupo, yatatekelezwa na Waziri Mkuu.
Hata hivyo, Ibara ya 37 (6) (b) inasema Rais hatahesabiwa kwamba hayupo iwapo atakuwa nje ya Jamhuri ya Muungano kwa kipindi cha saa 24.


0 comments:

Chapisha Maoni