Wakati vita dhidi ya madawa ya kulevya jijini Dar vikipanuka na kugeuka 
kuwa suala la kitaifa, kuna kila dalili kuwa usalama wa Mkuu wa Mkoa wa 
Dar es Salaam, Paul Makonda upo hatarini, Risasi Mchanganyiko limebaini.
Juzi Jumatatu, Paul Makonda alijitokeza tena hadharani na kutoa 
ufafanuzi wa mambo kadhaa yanayohusiana na vita alivyovianzisha, huku 
ikiwa ni mara yake ya tatu kutaja majina ya wanaojihusisha na madawa ya 
kulevya, safari hii, akitoa orodha ya watu 97.
HATARI YAKE IKOJE?
Biashara ya ‘unga’ ni moja kati ya biashara chache zenye fedha nyingi 
duniani, ambayo bahati mbaya inapigwa vita na serikali nyingi. Watu 
wanaojihusisha na shughuli hii, wana fedha nyingi na wako tayari kufanya
 lolote linalowezekana kuifanya biashara yao kuwa salama.
Kwa Paul Makonda kutangaza vita hadharani, tena akitaja majina ya watu 
na njia zinazotumika kuuleta, kuusambaza na kuusafirisha, anajiweka 
katika nafasi mbaya ya kuwa mlengwa wa wafanyabiashara hao, hasa kwa 
kuwa kukamatwa kwao siyo tu kutaharibu biashara yao hiyo, bali pia wao 
wenyewe watapotea.
Mfano mmojawapo wa jinsi watu wanaojihusisha na biashara hiyo walivyo na
 uwezo mkubwa, ni kesi ya bilionea wa unga wa Colombia, Pablo Escobar, 
aliyeuawa Disemba 2, 1993, baada ya mahakimu zaidi ya 30 waliosimamia 
shauri hilo kuuawa, licha ya kuendesha kesi hiyo wakiwa mafichoni, tena 
sauti zao zikiwa zimewekwa mawimbi ya kutofahamika.
MAADUI ZAKE WAMEONGEZEKA
Awali, ilionekana ni wauza madawa ya kulevya pekee ndiyo ambao wanaweza 
kusemwa kuwa ni maadui zake, lakini baada ya mazungumzo yake na vyombo 
vya habari Jumatatu iliyopita, watu ambao watafurahia kuona kiongozi 
huyo kijana anapatwa na matatizo, wameongezeka.
Watu hao ni pamoja na wamiliki wa maduka ya kubadilishia fedha maarufu 
kama Bureau de Change, wafanyabiashara wa mitungi ya gesi, wamiliki wa 
mahoteli na klabu za kamari (Casino), achilia mbali watoto wa viongozi 
wakubwa tokea serikali ya awamu ya tatu, chini ya Benjamin Mkapa.
KWA NINI HAWA?
Licha ya kushangazwa na wingi wa maduka ya kubadilishia fedha (alisema 
yapo zaidi ya 200 kwa Dar pekee), lakini pia aliyatuhumu kufanya miamala
 inayozidi kiwango kinachotakiwa kisheria, hivyo kuufanya mzunguko wa 
fedha zinazopitia hapo kuwa mkubwa.
Alisema wingi huo wa fedha, unatia shaka kuwa huenda unatumiwa na watu 
wa biashara ya madawa ya kulevya katika kutakatisha fedha. Kwa vyovyote,
 wenye maduka hawa hawajapendezwa na tuhuma dhidi yao na hivyo nao 
kuingia vitani kimyakimya.
Biashara ya mitungi ya gesi nayo ilitajwa kuwa ni mojawapo ya njia 
zinazotumiwa na wafanyabiashara hao kuficha madawa hayo wakati 
wakisafirisha kutoka au kwenda ughaibuni.
Aidha, alidai kuna hoteli kadhaa kubwa zenye wakazi wa kudumu, ambao 
wanatambuliwa na wamiliki wake, hivyo atahakikisha anawafanyia kazi, 
kitu ambacho kinaongeza idadi ya maadui, kama ilivyo kwa wamiliki wa 
nyumba 200 waliosemwa kuwa wanaruhusu biashara hiyo kufanywa ilhali 
wakijua ni kosa kisheria.
MBINU ZINAZODAIWA KUANDALIWA
Baadhi ya wanaharakati wanaopinga biashara ya madawa ya kulevya, ambao 
waliomba hifadhi ya majina yao, wamesema mbinu mbalimbali zinaweza 
kutumika ili kumdhuru kiongozi huyo, aliyewahi kuwa mkuu wa wilaya ya 
Kinondoni.
Mbinu hizo ni pamoja na kumwinda na kumuua kwa risasi, kitu ambacho ili 
kukidhibiti, wameomba kuimarishwa kwa ulinzi wake, nyumbani, kazini na 
hata awapo barabarani.
VIDOSHO, AJALI ZA KUTENGENEZWA
Eneo lingine alilotahadharishwa kujihadhari nalo ni pamoja na wasichana 
warembo, kwani wanaweza kutumiwa na maadui ili kumtia matatizoni, 
ikiwemo kumwekea sumu katika chakula, kinywaji au hata kumdhuru kwa 
namna nyingine.
Wadau hao wamelitaja eneo lingine la hatari linalopaswa kuangaliwa 
zaidi, ni kwa maadui zake hao kuweza kumtengenezea ajali ya kumdhuru, 
ili mradi wafanikiwe kuzima harakati zake za madawa ya kulevya 
alizoanzisha na kuungwa mkono na watu wengi.
KUHUSU ULINZI, HUYU HAPA SIRRO
Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Simon Sirro alizungumza na 
Risasi Mchanganyiko juu ya ulinzi wa kiongozi huyo. Akionyesha mshangao,
 alisema suala hilo siyo jambo la kuuliza kwa sababu wao wanaelewa nini 
kinapaswa kufanyika.
“Tunajua ukubwa wa vita hivi na madhara yake pia tunajua, huyu ndiye 
Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa, tunampatia ulinzi 
imara kabisa na kwa hili wala watu wasiwe na wasiwasi.”







0 comments:
Chapisha Maoni