Jumanne, 5 Agosti 2014

Yaliyoikuta Yanga Kagame Cup baada ya kupeleka kikosi cha Pili

DSC_0082-1Baada ya jana usiku katibu mkuu wa Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) Nicholas Musonye kutoa onyo kwa Yanga kuwasilisha majina mapya ya wachezaji wa kikosi cha kwanza kwa ajili ya Kagame Cup, leo hii CECAFA wametoa uamuzi mpya dhidi ya Yanga.
Yanga SC sasa rasmi imeondolewa kwenye michuano ya Kagame kutokana na Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati kupinga kupeleka timu ya vijana.
Yanga ilitaka kupeleka timu yenye vijana wengi iliyochanganyika na wakongwe wachache.
Lakini Katibu Mkuu wa Cecafa, Nicholas Musonye akasema hizo ni dharau. Wanasema ni timu ina wachezaji wa timu ya kwanza, vipi Maximo abaki Dar es Salaam.
“Halafu timu isafiri kwenda kwenye mashindano makubwa kama ya Kagame. Huu ni utani, ndiyo maana sasa tumeipa nafasi Azam,”alisema jana.
Mabingwa wa Tanzania Bara, Azam FC, watapambana Kundi A lenye timu za Rayon Sport ya Rwanda, Coffee ya Ethiopia, Atlabara ya Sudan Kusini na KMKM ya Zanzibar.
Kundi B lina timu za APR ya Rwanda, KCC ya Uganda, Flambeau de L’Est ya Burundi, Gor Mahia ya Kenya na Telecom ya Djibouti wakati Kundi C linaongozwa na mabingwa watetezi, Vital’O ya Burundi, El Merreikh ya Sudan, Polisi ya Rwanda na Benadir ya Somalia.
Rais Paul Kagame wa Rwanda ndiye mlezi wa mashindano haya ambaye hutoa dola za Kimarekani 60,000 kila mwaka kwa ajili ya zawadi.
Kwa kuwa Azam imechukua nafasi ya Yanga, sasa itacheza mechi ya ufunguzi dhidi ya wenyeji Rayon Sport Uwanja wa Amahoro Agosti 8, mwaka huu.
Mechi ya saa 8 mchana itakuwa ni kati ya KMKM ya Zanzibar  dhidi ya  Atlabara ya Sudan Kusini. 
Mechi ya pili ya Azam FC itakuwa  Agosti 10 dhidi ya KMKM, kabla ya kuivaa Atlabara Agosti 12, halafu itamaliza makundi dhidi ya Coffee ya Ethiopia Agosti 16.

0 comments:

Chapisha Maoni