Jumanne, 3 Mei 2016

PROF MUHONGO: TATIZO LA UMEME KUISHA MWAKA HUU MWEZI SEPTEMBA

SERIKALI inatarajia kuzindua mradi mkubwa wa kuboresha miundombinu ya kusafirisha umeme Septemba mwaka huu, utakaomaliza tatizo la umeme kukatika.
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo alisema kwa sasa miundombinu ya kusafirishia umeme ni midogo na katika kuboresha hilo, kuna mradi mkubwa utazinduliwa Septemba mwaka huu wa kusafirisha umeme.
Alisema mradi huo ni wa kusafirisha umeme kutoka kilovoti 220 hadi 400 kutoka Dar es Salaam-Tanga hadi Arusha na Iringa-Dodoma-Shinyanga, hivyo tatizo la kukatika umeme litatatuliwa.
Waziri huyo alitoa maelezo hayo wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Korogwe Mjini, Mary Chatanda (CCM) aliyetaka kufahamu lini umeme utakoma kukatika wilayani Korogwe.
Akielezea hilo, Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dk Medard Kalemani alisema Serikali inafanya marekebisho ya transfoma na chanzo cha umeme cha Hale mkoani Tanga ili kumaliza tatizo la kukatika umeme mara kwa mara wilayani Korogwe na mkoani Tanga kiujumla.

0 comments:

Chapisha Maoni