UNAAMBIWA ukiona cha nini mwenzako anasema nitakipata lini, kwani baada
ya Yanga kuamua kumtema kocha wao za zamani, Hans van der Pluijm, nyota
ya Mholanzi huyo imezidi kung’aa na sasa ana ofa mbalimbali kutoka ndani
na nje ya nchi ambazo zimekuwa zikimiminika kila kukicha.
Pluijm alibadilishwa kutoka kuwa kocha mkuu wa klabu hiyo na kupewa cheo
cha ukurugenzi wa benchi la ufundi muda mfupi baada ya waajiri wake,
Yanga, kumwajiri kocha mwingine, George Lwandamina, aliyekuwa akiinoa
timu ya Zanaco ya Zambia, lakini hakudumu muda mrefu, baadaye
alitimuliwa kabisa kutokana na kile kilichodaiwa na uongozi kuwa ni
ukosefu wa fedha.
DIMBA Jumatano limezungumza na Pluijm kuhusu mustakabali wake ambapo
amesema anamshukuru Mungu kwa kuendelea kumpigania, kwani kwa sasa
amekuwa akipata ofa mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi ambazo
zinampa wakati mgumu wa kuamua aende wapi.
Alisema kwa sasa bado yupo Tanzania na wala hajaondoka kwenda kwao
Ghana, ambapo amedai kuwa, anafanya mambo yake kimyakimya na yakishakaa
sawa atawekakila kitu bayana ili Watanzania na wadau wanaomuunga mkono
wafahamu.
“Kama kuna watu wanauliza, kama nipo Tanzania au nimeshakwenda Ghana
waambie bado nipo hapa nchini, na kuhusu mustakabali wangu niseme kwamba
siwezi kuzungumza mengi kwa sasa ila kwa kifupi nimepata ofa mbalimbali
za hapa Tanzania na nje ya nchi.
“Kwa sasa nachukua muda kutafakari na kutuliza akili yangu halafu
nitafanya maamuzi sahihi,” alisema kocha huyo, aliyeiletea heshima Yanga
kutokana na kuwapa vikombe mbalimbali, huku pia akijenga mashikamano
ndani ya timu.
Taarifa zaidi kutoka vyanzo mbalimbali zinadai kuwa, moja ya timu ambazo
Pluijm anatajwa kujiunga nazo hapa nchini ni timu ya Taifa ya Tanzania
‘Taifa Stars’ ambayo kwa sasa ipo chini ya Jackson Mayanja.
0 comments:
Chapisha Maoni