Alhamisi, 9 Machi 2017

Ukweli Mchungu..Uwepo wa WCB; Bongo Fleva Inachungulia Kaburi...!!!

Hayo yote nayasema kuhusu nyota wa Bongo Fleva, Nasibu Adul Juma au maarufu zaidi kwa jina la Diamond. Siku za hivi karibuni, Diamond ameanzisha zoezi la kuwachukua wanamuziki na kuwaingiza kwenye kundi lake maarufu sana la Wasafi Classic Baby ‘WCB’ ambalo limetokea kupata jina kubwa katika Muziki wa Kizazi Kipya Bongo.
Lebo hii ya Wasafi kwa sasa inaundwa na watu wanne, Queen Darleen, Rayvanny, Rich Mavoko na Harmonize. Awali, alianza na akina Harmonize, Rayvanny, Rich Mavoko na mwisho ni Queen Darleen. Harmonize na Rayvanny walikuwa hawakutamba sana kabla ya kwenda Wasafi. Mimi kwa hao, naona ni sawa kabisa na wala sina tatizo nao.
ANAINUA VIPAJI
Katika mahojiano yake na vyombo mbalimbali vya habari hapa Bongo, Diamond amekuwa akisema kwamba, anafanya hivyo ili kukuza muziki na kuinua vipaji vya wanamuziki wachanga wa Tanzania. Mimi kwa hilo pia sina tatizo naye. Pia, watu au wadau mbalimbali wa muziki huo wakawa wanampongeza Diamond kwa kuwa, zoezi lake la kuwabeba akina Harmonize linaongeza ushindani mkubwa katika Muziki wa Kizazi Kipya, kwamba kama yeye anawainua hawa, wengine wakainuliwa kule, muziki utapaa. Na kwa hili pia mimi sina tatizo nalo hata kidogo.
NI HOJA ZA MSINGI SANA
Kuna hoja za msingi kwamba, kama si Diamond, hawa akina Rayvanny wasingekuwa hivi walivyo leo. Wasingejulikana kama wanavyojulikana wakiwa kwa Diamond. Hiyo ni hoja ya msingi sana, tena sana. Na kwa hilo mimi sina tatizo na hoja husika.
KUHUSU RICH MAVOKO
Katika zoezi lake la kuendelea kuchukua wasanii, Diamond akamchukua Mbongo Fleva, Rich Mavoko ndani ya kundi lake la Wasafi. Hapa kidogo baadhi ya watu wakahoji uhalali wa usahihi wake. Wengi waliamini kuwa, Diamond kumchukua msanii huyo ambaye alishajenga jina kubwa katika muziki huo ni sawa na kumpoteza njia kwani Rich Mavoko kuwa chini ya Wasafi kunaweza kumfanya afifie kama siyo kufa kabisa kisanii.
NINACHOKIONA
Sasa ninachokiona mimi ni kwamba, nia ya Diamond inaweza kuwa nzuri sana lakini kukatokea makosa madogomadogo kwenye kuchukua aina ya wasanii. Yapo madai ya chini kwa chini kwamba, pia ana mpango wa kumchukua msanii anayevuma sana kwa sasa, Darassa ambaye kibao chake cha Muziki kimeishika nchi kwa kupigwa maeneo mbalimbali. Kama kuna ukweli wa madai haya, naamini kuna siku tutakuja kusikia, hata Ali Kiba, Ommy Dimpoz nani sijui, wote wana mpango wa kujiunga Wasafi. Katika hili, ninatia shaka kwamba, lengo la Diamond kuwakusanya wasanii niliowataja na kumchukua pia Rich Mavoko ni njia moja kwake ya kuelekea kwenye kuudidimiza muziki wa Bongo Fleva.
Wasafi linajiimarisha kuwa kundi kubwa la muziki huo nchini. Sasa je, ikitokea hivyo, upinzani utatoka wapi? Ninavyojua mimi siku zote, palipo na ushindani ndipo panapokuza kitu. Ni sawa na timu za mpira wa miguu wa Tanzani, piga mahesabu kwamba, kuna siku Simba itashuka daraja. Je, Yanga atabaki na mshidani gani? Na kilele cha raha ya mpira wa Tanzania ni kucheza kwa Simba na Yanga.
Ndiyo maana, makocha wa timu hizo bora wafungwe na timu nyingine zote, lakini siyo Simba au Yanga. Hata shule wanazosoma watoto wetu siku hizi, ubora wake inatokana na kuwepo kwa shule bora nyingine. Kama ingekuwa shule moja tu ndiyo bora sifa yake isingekuwa na maana. Sifa  ya mtu mrefu duniani kote inatokana na kuwepo kwa mtu mfupi. Kama watu wote wangekuwa na kimo sawa isingejulikana kama urefu ni bora.
Kuwepo kwa Wasafi kusiwe sababu ya kuwakusanya wanamuziki wengine hawa wenye majina makubwa kwani na wao uwepo wao ndiyo changamoto ya kuwepo kwa Wasafi. Inawezekana nia ya Diamond ikawa nzuri sana lakini mimi naamini anakokwenda, kunaweza kuwa ndiyo kaburi la muziki wenyewe.

0 comments:

Chapisha Maoni