HALI ya taharuki imeibuka katika Halmashauri ya Moshi baada ya madiwani
kugomea mafunzo ya utaratibu ulioboreshwa wa uendeshaji ruzuku ya
maendeleo kwenye mamlaka za Serikali za mitaa (LGDG), wakishinikiza
kulipwa posho ya Sh 100,000 kila mmoja.
Mafunzo hayo yaliyokuwa yanasimamiwa na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa (TAMISEMI), yalihusisha madiwani wote na wakuu wa
idara jana katika ofisi za Halmashauri.
Taharuki iliibuka baada ya madiwani hao kuingia ukumbini na kabla ya
mafunzo kuanza, Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Michael Kilawila
aliwatangazia kuwa kutokana na mafunzo kutokuwa ya kisheria, Halmashauri
itapaswa kutoa posho zao kupitia makusanyo ya ndani.
Kilawila alisema kutokana na hali hiyo na mapato kuwa madogo, kila
diwani atalipwa Sh elfu 60,000 kama posho ya siku moja ambapo siku mbili
za mafunzo hayo kila mmoja angepokea Sh 120,000.
Baada ya tamko hilo hali iligeuka baada ya madiwani hao kuonesha
kutoridhishwa na kiwango hicho cha posho na kugonga meza wakishinikiza
kulipwa Sh 100,000 kwa siku kama wanavyolipwa kwa vikao vingine
vinavyotambulika.
Waliposhindwa kuelewana, madiwani hao walisusia mafunzo hayo na kuondoka
hali iliyowalazimu wakufunzi kutoka Tamisemi kufundisha wakuu wa idara
peke yao.
Akizungumzia sintofahamu hiyo, Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Butamo
Ndalahwa alisema lengo la mafunzo hayo ni kuhakikisha madiwani kwa
kushirikiana na wananchi, wanaibua miradi.
Ndalahwa alisema mafunzo hayo yanafanyika katika halmashauri zote nchini
na kuwa madiwani hao waligoma wakitaka posho kubwa bila kujali kuwa
mafunzo hayo yangenufaisha wananchia ambao ndio waliowachagua.
Mkurugenzi huyo akionesha masikitiko, alisema jambo hilo la kugomea
mafunzo litasababisha maendeleo ya Halmashauri kurudi nyuma kwa kukosa
elimu ya uibuaji miradi ambayo inakubalika.
“Nimesikitishwa kwa kiasi kikubwa, madiwani wameonesha kutangulia mbele
maslahi yao badala ya kutumikia wananchi waliowachagua, tumewaelimisha
kuhusu posho, kwa nini tunawapa Sh 60,000 lakini hawakutaka kuelewa na
badala yake waligonga meza ovyo na kutoka nje,” alisema Ndalahwa.
Kilawila alipotafutwa kwa njia ya simu kuzungumzia suala hilo na hatima
yake, alisema hawezi kuzungumzia jambo lolote mpaka kikao cha madiwani
kitakapokaa ili kutoa maazimio.
“Ninachoweza kusema sasa ni kwamba siwezi kuzungumza lolote, mtafute
Mkurugenzi, mimi nasubiri ni kikao cha madiwani ili kutoa maazimio ya
kilichotokea leo,” alisema Kilawila.
0 comments:
Chapisha Maoni