ALIYEKUWA Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila amelaani hatua ya Mkuu
wa Wilaya ya Hai, Gelasius Byakanwa kutumia mamlaka yake kuvamia na
kuharibu shamba la Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe.
Juzi, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya hiyo ikiongozwa na Mkuu wa
Wilaya walivamia shamba la Mbowe nyumbani kwake Machame na kuharibu
miundombinu, mali, mboga na mimea kadhaa.
Akizungumza Dar es Salaam juzi, Kafulila alisema amesoma na kusikia kuwa
Mkuu huyo alitumia mamlaka yake kufanya kitendo hicho, jambo ambalo
aliliita ni laana ya hali ya juu.
“Nimesoma na kusikia kuwa Mkuu wa Wilaya ametumia mamlaka yake kuvamia
na kuharibu shamba la Mwenyekiti wa Chadema ambalo ni uwekezaji wa
kilimo cha mboga kwa soko la ndani na nje ya nchi,” alisema.
Alisema kitendo hicho ni cha kushangaza, kwa kuwa shamba hilo lina
thamani ya mamilioni ya fedha, lakini mtu anatokea na kuharibu
miundombinu kwa kuwa ni kiongozi tena bila sababu za msingi jambo ambalo
halileti picha nzuri kwa jamii.
“Huu ni uamuzi unaoweza kufanywa na Serikali za kishenzi kama Somalia au
Sudani na Burundi. Nasita kuamini kama huko ndiko Rais John Magufuli
anataka kutupeleka,” alisema na kuongeza:
“Naamini atachukua hatua kali dhidi ya DC huyu, kwani ni doa lenye
viashiria vya chuki za kisiasa kwa kiwango cha unyama, chuki ambayo
hakika sidhani kama inaweza kuwa maelekezo ya kiongozi anayemtaja Mungu
na kuomba maombi siku zote.”
0 comments:
Chapisha Maoni