Ijumaa, 16 Juni 2017
Home »
» Simba Walimdaka Niyonzima Airport...Yanga Yaambulia Patupu
Simba Walimdaka Niyonzima Airport...Yanga Yaambulia Patupu
WAKATI Yanga wakimsubiria kiungo wao mchezeshaji, Haruna Niyonzima atue nchini kwa ajili ya kumuongezea mkataba watani wao wa Simba wenyewe hawakauki Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere ili wamsainishe. Hiyo, ikiwa ni siku chache tangu tetesi zienee kuwa kiungo huyo anayemudu kucheza namba nane tayari amesaini mkataba wa miaka miwili kuichezea Simba. Kiungo huyo, hivi sasa ni mchezaji huru anayeruhusiwa kufanya mazungumzo na klabu nyingine kutokana na mkataba wake kumalizika mwezi ujao kwa mujibu wa kanuni za Fifa.
Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Championi Ijumaa, kutoka kwa ndugu wa karibu wa Niyonzima viongozi wa Simba walikuwa tayari wapande ndege kumfuata kiungo huyo Rwanda, lakini ilishindikana kutokana na kukatishwa tamaa na meneja wake.
Mtoa taarifa huyo, mfanyabiashara maarufu nchini, Mohammed Dewji ‘Mo’ ndiye alikuwa anawasiliana na Niyonzima kwa ajili ya kwenda kumsainisha nchini Rwanda kwa dau la shilingi milioni 70. “Nikwambie ukweli tu, ni ngumu Niyonzima kwenda kusaini mkataba wa kuichezea Simba, kwani mpango wao wa kwanza walioupanga umeshindikana kwani walipanga wamfuate Rwanda alipokuwa kwenye majukumu yake ya timu ya taifa.
“Mipango hiyo ilishindikana ni baada ya meneja wake kuuzuia
uongozi wa Simba usiende huko na badala yake wamsubirie hadi ataporejea nchini na baada ya kuona wamekwama, viongozi hao wa Simba wakaanza kwenda kumwinda uwanja wa ndege kwa kukagua muda wa ndege wa Rwanda Air na mratibu wa hilo ni Mo.
“Lakini wakati wakipanga hayo, Bin Kleb (Abdallah), yeye aliwasiliana na Niyonzima na kumwambia mara baada ya kutua nchini asionane na yeyote zaidi yake yeye,” alisema mtoa taarifa huyo. Championi Ijumaa,lilimtafuta Niyonzima na kuzungumza naye moja kwa moja kutoka Rwanda kuhusiana na taarifa za yeye kusaini Simba alisema kuwa: “Hayo maneno tu wanaongea, nikuhakikishie mimi sijasaini Simba na kama unakumbuka mimi nilikwambia nimeichezea kwa amani Yanga miaka sita hivi sasa.”
0 comments:
Chapisha Maoni