Ijumaa, 16 Septemba 2016

RUBBY ATANGAZA KUJISIMAMIA MWENYEWE BAADA YA KUTEMANA NA CLOUDS FM, ADAI SASA NI YEYE NA MASHABIKI WAKE


Msanii wa Bongo Fleva, mwanadada Ruby ambaye amewahi kutamba na wimbo wake wa “Na Yule’ amefunguka na kusema kwa sasa amebadili uongozi wake na kujisimamia yeye kwani anataka kusimama yeye pamoja na mashabiki zake.

Ruby alisema hayo kwenye kipindi cha eNewz na kudai kuwa yeye aliamua kubadili uongozi kwa sababu anataka kusimama yeye kama yeye kwenye muziki kwa kutegemea mashabiki wake, pia Ruby anadai Tanzania ukimchana mtu ukweli unaonekana wewe ni mkorofi au mgomvi.

“Unajua hata mtoto anapokuwa kwa wazazi inafika wakati anahitaji kuanza maisha yake mwenyewe, hivyo mtoto akiondoka kwa wazazi haina maana kuwa hauna wazazi ‘No’ wala haina maana kuwa umeondoka nyumbani kuna matatizo bali unakuwa umeanza maisha yako mwenyewe, ni sawa na mimi saizi nimebadili uongozi wangu na niko mimi kama mimi kwani nataka kusimama pamoja na mashabiki zangu. Watu wanasema sijui mimi ni mkorofi hao ni wao kwani mtu ukimchana ukweli unaonekana wewe ni mkorofi ni bora ukamwambia mtu ukweli kwani ukweli utakuweka huru” alisema Ruby

SERIKALI YAANZA MAZUNGUMZO YA KUWAOKOA MADEREVA 12 WALIOTEKWA CONGO

Serikali imeingilia kati na kuanza mazungumzo ya kuwaokoa madereva 12 wa malori kutoka Tanzania waliotekwa nchini Kongo (DRC) na kundi la waasi wa Mai Mai.
loritanzania

Waasi hao mbali na kuwateka madereva hao wametoa saa 24 kuanzia juzi saa 10 jioni walipwe fedha kiasi cha Dola za Marekani 4,000 kwa kila dereva ili waweze kuwaachia.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mindi Kasiga, alisema waasi hao wametishia kuwaua mateka hao endapo hawatalipwa kiasi hicho cha fedha hadi kufikia jana saa 10 jioni.

Mindi alisema katika tukio hilo, madereva wawili wa Kitanzania walifanikiwa kutoroka na ndiyo waliosaidia kutoa taarifa kuhusu tukio hilo.

“Serikali imepokea taarifa za kutekwa kwa malori 12 katika eneo la Namoyo Jimbo la Kivu Kusini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, jana (juzi) Septemba 14, 2016. Kati ya malori hayo manane yanamilikiwa na mfanyabiashara wa Kitanzania, Azim Dewji na mengine yanamilikiwa na wafanyabiashara kutoka Kenya.

“Kwa taarifa zilizopatikana watekaji ni kikundi cha waasi cha Mai Mai ambao baada ya kuyateka magari hayo, waliwashusha madereva na kuwapeleka porini na kisha kuteketeza kwa moto malori manne ambayo yote ni ya Dewji.

“Waasi hao wametoa saa 24 kuanzia jana saa 10 jioni walipwe fedha kiasi cha Dola za Kimarekani 4,000 kwa kila dereva ili waweze kuwaachia,” alisema Mindi.

Alisema Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imeshachukua hatua za awali za kuwasiliana na Serikali ya DRC ili kuhakikisha kuwa madereva hao wanaachiwa haraka iwezekanavyo wakiwa salama kabisa.

Alisema tukio la aina hiyo ni la pili kutokea ambapo katika mwaka jana masheikh kutoka Tanzania walitekwa nchini DRC lakini kwa ushirikiano wa Serikali hizo mbili juhudi ziliweza kuzaa matunda na masheikh hao kuachiwa huru bila madhara yoyote.

“Serikali ingependa kuushauri umma wa Watanzania hususan wafanyabiashara kuomba taarifa ya hali ya usalama kwa maeneo yenye matatizo ya kiusalama kama Mashariki ya Kongo hususan Kivu ya Kusini kabla ya kusafiri kwenda maeneo hayo,” alisema Mindi.

SAKATA LA REDIO KUFUNGWA MAGIC FM YATAKIWA KUOMBA RADHI SIKU TATU MFULULIZO, REDIO 5 ZAFUNGIWA MIEZI


August 29 2016 Waziri wa habari, utamaduni, sanaa na michezo Nape Nnauye alitangaza kuvifungia vituo viwili vya radio kwa muda usiojulikana ambavyo ni Magic Fm ya Dar es salaam na Radio 5 ya Arusha kwa makosa ya kutangaza na kutoa habari za kichochezi.

Waziri Nape alielekeza kamati ya maudhui kuviita vyombo hivyo na kuwasikiliza kwa kina kisha kushauri hatua zaidi ya kuchukua.

Leo September 16 2017 kamati imetoa maamuzi ambapo Magic FM wamepewa onyo kali na kutakiwa kuomba radhi kwa siku tatu mfululizo kuanzia kesho September 17 2016, Redio 5 imepewa adhabu ya kulipa shilingi milioni 5, kufungiwa miezi 3 na kuwekwa chini ya uangalizi wa mwaka mmoja.

ZOMBE AACHIWA HURU, MSHIRIKA WAKE AHUKUMIWA KUNYONGWA HADI KUFA


Mahakama ya Rufaa imemhukumu aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi Wilaya ya Kinondoni, Christopher Bageni kunyongwa hadi kufa katika kesi ya vifo vya wafanyabiashara wa madini iliyokuwa ikimkabili yeye pamoja na aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Dar es Salaam (RCO) Kamishna Msaidizi wa Polisi Abdallah Zombe na maofisa wenzake wawili.

Katika hukumu hiyo, Zombe na maafisa wengine wawili wameachiwa baada ya kushinda rufani hiyo dhidi yao.

Hukumu hiyo imehitimisha mvutano wa muda mrefu wa kisheria kati ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) na maofisa hao kwani baada ya kimya kirefu hukumu hiyo imetolewa.

Watuhumiwa wengine katika kesi hiyo walikuwa ni, aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi wa Kituo cha Polisi Urafiki, Mratibu Msaidizi wa Polisi (ASP) Ahmed Makelle na Rajabu Bakari.

Hukumu hiyo imekuwa ikisubiriwa kwa muda mrefu, wakiwamo ndugu wa marehemu hao, wanasheria na jamii kwa jumla baada ya miezi minne, majuma mawili na siku mbili, tangu rufaa iliposikilizwa.

DPP alikata rufaa akipinga hukumu ya Mahakama Kuu iliyowaachia huru Zombe na wenzake wanane katika kesi ya mauaji ya wafanyabiashara wawili wa madini kutoka Mahenge, Morogoro na dereva wa teksi, mkazi wa Dar es Salaam.

Katika kesi ya msingi, Zombe na wenzake walidaiwa kuwaua kwa kukusudia wafanyabiashara Sabinus Chigumbi, maarufu Jongo na ndugu yake, Ephrahim Chigumbi, Mathias Lunkombe na Juma Ndugu, aliyekuwa dereva wa teksi wa Manzese.

Walidaiwa kutenda makosa hayo Januari 14, mwaka 2006, katika msitu wa Pande, uliopo wilayani Kinondoni baada ya kuwakamata wafanyabiashara hao Sinza, walipokuja Dar es Salaam kuuza madini.

Agosti 17, 2009, Mahakama Kuu iliwaachia huru washtakiwa hao ikisema baada ya kusikiliza ushahidi na hoja za mawakili wa pande zote iliridhika kuwa hawakuwa na hatia ya mashtaka yaliyokuwa yakiwakabili.

Badala ya kosa la mauaji ambalo adhabu yake ni kunyongwa hadi kufaa, DPP aliiomba Mahakama imtie hatiani Zombe kwa kosa la kuwalinda wahalifu, ambao adhabu yake ni kifungo kisichozidi miaka saba jela.

Wakili wa Serikali Mkuu (PSA), Timon Vitalis alidai DPP alifikia uamuzi huo baada ya kujiridhisha kuwa hakuna ushahidi wa kumtia hatiani Zombe kwa kosa la mauaji.

ALICHOKIZUNGUMZA WAZIRI WA MAMBO YA NDANI CONGO KUHUSU MADEREVA WALIOTEKWA


Jana ziliripotiwa habari za kutekwa kwa madereva wa malori kutoka Tanzania na Kenya kutekwa na kundi la waasi nchini Congo. Leo September 16 habari zilizoripotiwa na BBC Swahili zimedai kuwa watu wameokolewa na jeshi la nchi hiyo.

BBC imezungumza na waziri wa mambo ya ndani wa nchi hiyo ambapo kuwa madereva wote wameokolewa na vikosi vya jeshi la nchi hiyo na wako salama. BBC imesema utekaji wa madereva hao ulifanywa na watu wenye silaha katika kijiji cha Matete kuelekea Namoya kilichopo Mji wa Kivu Kusini Mkoa wa Manyema.

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Congo alipoongea na BBC kwa njia ya Simu, amesema ni magari saba ya kampuni ya Simba inayomilikiwa na mfanyabiashara Azim Dewji kutoka Tanzania ndio yaliyochomwa.

Waziri huyo amesema tukio hilo halijafanywa na waasi kama ilivyoanza kuripotiwa, ila ni majambazi tu ndio waliofanya tukio hilo.

>>>Ni majambazi tu wanatoka porini walipoona magari yanatembea wakayasimamisha katikati ya pori na kuangalia kama kuna pesa wanyang’anye lakini hawakukuta pesa wakaamua kuwachukua madereva na kukimbia nao porini kisha wakayachoma magari 6 na moja halikuteketea.:- Waziri Mambo ya Ndani Congo.

MAJAMBAZI, MALI ZA WIZI NA SILAHA VYAKAMATWA DAR



Kikosi maalum cha kupambana na ujambazi wa kutumia silaha cha Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam kimefanikiwa kuwakamata watuhumiwa 5 wa makosa ya ujambazi wa kutumia silaha katika maeneo mbalimbali.

Kamishna wa Polisi kanda maalum ya Dar es salaam Saimoni Sirro akionesha baadhi ya vifaa vilivyokamatwa.

Taarifa hiyo imetolewa na Kamanda wa Polisi Kanda maalum ya Dar es Salaam Kamishna Saimoni Sirro wakati akitoa taarifa ya kukamatwa majambazi wa 5 na kukutwa na silaha aina ya shotgun, bastola 3 na risasi 49.

Katika tukio lingine Polisi mnamo tarehe 5.9.2016 majira ya saa 8 usiku maeneo ya Magomeni mtaa wa Makumbusho waliokota begi lililokuwa na bastola mbili, sambamba na hilo wamefanikiwa kukamata magari 4 ya wizi, hati za magari na watuhumiwa wawili wa uhalifu huo wamekamatwa.
Jeshi hilo limetoa wito kwa viongozi wa serikali za mitaa kupitia kamati za ulinzi wa mitaa kuimarisha ulinzi na kuwataka wamiliki wa nyumba za kupanga kuhakikisha wanaweka kipengele cha kuwepo na picha katika mikataba ya kupangisha nyumba zao kutokana na uwepo wa wimbi la uhalifu.

Wakati huo huo Kamanda Sirro amesema Kanda Maalum ya Dar es Salaam kwa kipindi cha siku 11 wamefanikiwa kukusanya kiasi cha shilingi 882,570,000 ikiwa ni tozo za makosa ya usalama barabarani na makosa mengineyo.

KUTOKA BUNGENI: RAISI MAGUFULI KUHAMIA DODOMA RASMI MWAKA 2020



Leo Septemba 16, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akisoma hotuba ya kuahirisha mkutano wa nne kwa Bunge la 11 uliodumu kwa muda wa wiki mbili, amesoma ratiba ya serikali kuhamia Dodoma.

“Ili kufanikisha azma ya Serikali kuhamia Dodoma, tayari imeandaliwa ratiba itakayowezesha Serikali kuhamia Dodoma kwa awamu, kuanzia mwezi Septemba, 2016 hadi mwaka 2020, bila ya kuathiri bajeti yetu ya mwaka 2016/2017 kama ifuatavyo”–


1. Septemba 2016 – Februari 2017.

Waziri Mkuu na Mawaziri wote, Makatibu Wakuu wote, Manaibu Makatibu Wakuu wote watahamia Dodoma katika Awamu ya Kwanza. Aidha, kila Wizara itatakiwa kuhamisha Watumishi wa Idara moja au mbili, na wakati huo huo kuendelea kuweka utaratibu wa kupeleka Watumishi wa Idara nyingine kuhamia Dodoma;

2. Machi 2017 – Agosti 2017.

Kipindi hiki kitawapa fursa watendaji wa wizara mbalimbali kuweka katika Bajeti zao za mwaka 2017/2018 gharama za kuendelea kuhamisha watumishi wake kuja Dodoma.

3. Septemba 2017 – Februari 2018.

Katika awamu hii, Wizara zitaendelea na uhamishaji wa Watumishi wa Idara zilizo ndani ya Wizara.

4. Machi 2018 – Agosti 2018.

Katika kipindi hiki, Wizara zinatakiwa kuendelea kuhamisha watumishi wake.

5. Septemba 2018 – Februari 2020.

Katika kipindi hiki, Wizara zinatakiwa kuendelea kuhamisha watumishi wake.

6. Machi 2020 – Juni 2020.

Katika kipindi hiki, Ofisi ya Rais ikiongozwa na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, watakuwa wanahamia Dodoma.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alitumia wasaa huu kuzishauri Wizara zote kuanzisha mifumo ya utunzaji kumbukumbu wa kielektroniki badala ya kuhama na mafaili kutoka Dar es Salaam kuja Dodoma, tunataka Dodoma iwe ya kielektroniki, alisisitiza Waziri Mkuu.