BAADHI ya baa zilizopo katika viwanja vya Legho, Ubungo jijini Dar, leo
zimevunjwa kufuatia agizo la mahakama kwa kile kilichodaiwa wamiliki
walivamia eneo ambalo siyo lao.
Akizungumza na mwandishi wetu, dalali wa mahakama kutoka katika kampuni
ya Mem Auctioneers and General Brokers Ltd, Elieza Mbwambo, alisema
mmiliki halali wa eneo hilo ni Dar Cool Makers Limited ambaye baada ya
kuvamiwa eneo lake alifungua kesi mahakamani mwaka 1993 ambapo
iliendelea mpaka ilipofikia leo.
Wavamizi wa eneo hilo ambao ni John Ondoro Chacha, Jumuiya ya Wazazi CCM
na mtu mwingine mmoja baada ya kuona mmiliki halali amepeleka kesi
mahakamani nao wakaenda kuweka zuio ambapo Mahakama ya Hakimu Mkazi
Kisutu iliamuru eneo hilo lirudi kwa mmliki halali ambapo wavamizi
walitakiwa wabomoe vibanda walivyokuwa wamejenga walikokuwa wakifanya
biashara ya baa.
“Januari 25 mwaka huu tulipewa oda na mahakama tuje kuwatoa hawa
wavamizi, tuliweka tangazo kama wiki moja iliyopita lakini hawakujali
hivyo leo ikawa ndiyo siku rasmi ya kuwaondoa na kama unavyoona ndiyo
tunabomoa hivi.
“Mwenye kesi ya msingi ambaye ni John Ondoro Chacha alitakiwa kuwaambia
wapangaji wake kwamba ameshindwa kesi lakini hakuwaambia ndiyo maana
hata tangazo lilipowekwa hawakushtuka, kwa mujibu wa mahakama huyu
Chacha ambaye kwa sasa ni marehemu na watoto wake ndiyo walikuwa
wakipokea kodi ya kila mwezi kwa wafanyabiashara waliowapangia wakati
eneo hili siyo lao,” alisema Mbwambo.
Watu mbalimbali walionekana wakiwa wamesimama huku wakishangaa eneo hilo
huku wengine wakilalamika kwamba watakuwa wanajiachia wapi wakati
walikuwa wamezoea viwanja hivyo.
Source-Global Publishers
Ijumaa, 5 Februari 2016
Home »
» Bomoa Bomoa Zaikumba Sinza...Baa za Uwanjani Legho Zavunjwa
0 comments:
Chapisha Maoni