MBUNGE wa Arusha Mjini, Godbless Lema ameendelea kusota katika mahabusu
ya Gereza la Kisongo mjini hapa akiingiza siku ya 22 leo baada ya jana
kukwama katika azma yake ya kutaka Mahakama Kuu Kanda ya Arusha kufanya
marejeo ya uamuzi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha uliomnyima dhamana.
Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, Sekela Moshi ndiye
aliyetupilia ombi la Lema, hivyo kumfanya arejee mahabusu huku mawakili
wake wakihaha kuhakikisha wanakata rufaa ili kuomba dhamana hiyo katika
ngazi nyingine ya kisheria.
Aidha, Jaji Moshi ameridhia ombi la Lema kupitia kwa mawakili wake Sheck
Mfinanga na Peter Kibatala la kukata rufaa mahakamani hapo ili kesi
hiyo isikilizwe na hatimaye Lema kupata dhamana baada ya kupitiwa na
jaji atakayepangiwa.
Akitoa uamuzi huo mahakamani hapo, Jaji Moshi alisema kimsingi hoja ya
mawakili wa Lema ya kutaka mahakama hiyo kuitisha faili na kulipitia
haina msingi wowote kisheria hivyo anaitupilia mbali hoja hiyo na kutoa
rai kwa mawakili hao kukata rufaa Mahakama ya Rufaa ili dhamana ya Lema
isikilizwe.
“Mahakama hii haiwezi kupitia faili la kesi hii ya Lema ya kupata
dhamana hivyo siwezi kupitia faili hili, bali nashauri mkate rufaa ili
iweze kusikilizwa,” alisema Jaji Moshi.
Awali Wakili wa Serikali, Paul Kadushi aliwasilisha pingamizi Mahakama
Kuu la kuitaka wasisikilize maombi ya Lema ya kutaka mahakama hiyo
iitishe faili la kesi namba 440/441 kwa madai yapo makosa ya kisheria
yaliyofanywa awali na Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha kwa lengo la
kumnyima dhamana mbunge huyo.
Akiwasilisha hoja zake mbele ya Jaji Moshi katika Mahakama Kuu Kanda ya
Arusha, Kadushi akisaidiana na Materu Marandu alisema anawasilisha hoja
mbili za pingamizi za mahakama hiyo kuendelea kusikiliza kesi hiyo.
Alisema kimsingi maombi hayo yaliwasilishwa mahakamani hapo kutaka
mahakama hiyo iitishe faili la kesi namba 440/441 yanakinzana na kifungu
cha 43 (2) cha sheria ya Mahakama ya Mahakimu. Katika kesi hiyo, Lema
anashitakiwa kwa kutoa maneno ya kumtusi Rais katika maeneo tofauti.
Kadushi alisema uamuzi unaopinga kufanywa na Mahakama ya Hakimu Mkazi
Arusha ya kukubali kutompa dhamana Lema ni uamuzi mdogo na haukuwa na
sababu za kukataa dhamana.
“Mahakama yako inafungwa mikono na kifungu hiki kufanya mapitio au
uamuzi mdogo, hivyo tunaomba mahakama itupilie mbali maombi
hayo,”alisema Kadushi ambaye wakati akiwasilisha hoja zake alikuwa
akinukuu mashauri mbalimbali ya kesi zinazofanana na hiyo.
Aidha, Kadushi alisisitiza kuwa wao wanatambua haki ya kukata rufaa ipo
wazi kwa mleta maombi ila itakuwa jambo geni kama mahakama itawapa
nafasi kusikiliza maombi yao. Alisema hoja ya pili ya pingamizi lake,
linatokana na mleta maombi kutokidhi matakwa ya kisheria ya mwenendo wa
makosa ya jinai.
Katika sheria ya makosa ya jinai, kifungu cha 359(1) ya mwaka 2002 kuwa
mtu asiporidhika na maamuzi ya mahakama ya chini kama ilivyo katika kesi
hiyo, kamwe hawezi kuwa na mbadala wa mapitio ya rufaa.
Akijibu hoja hizo Wakili anayemtetea Lema, Peter Kibatala akiwa na jopo
la mawakili wenzake, Adam Jabir, Sheck Mfinanga, John Mallya, Faraji
Mangula na Charles Adiel, alipinga kuwekewa pingamizi hilo na kuomba
mahakama isikilize maombi yao.
Alisema wao wamefungua maombi hayo kuiomba Mahakama Kuu kuitisha jalada
la kesi ya mahakama ya chini ili kuona uhalali wa kutotekelezwa kwa
uamuzi wa kutoa dhamana, kwani kilichokuwa kinasubiriwa ni masharti ya
dhamana.
“Huyu mshitakiwa alipewa dhamana , ila kabla ya mahakama haijatoa
masharti ya dhamana, upande wa serikali ukasimama kabla mahakama
haijaweka masharti ya dhamana ambayo lazima ifanye hivyo, wakasema
wameonesha nia ya kukata rufaa na mahakama ikakubaliana nao bila
kutekeleza amri yao,” alisema Kibatala.
Aliomba mahakama hiyo itupilie mbali pingamizi la serikali na kuiomba
kuendelea na kazi iliyokusudia kuifanya ya kupitia maombi yao ili kutoa
dhamana kwa mshtakiwa au iamuru mahakama ya chini kuendelea na uamuzi
wake.
Wakili wa mbunge huyo baada ya maombi yao kugonga mwamba, walikuwa
kwenye hekaheka ya kukamilisha kuandika rufaa ili kumnasua Lema atoke
mahabusu.
Baada ya kutoka nje ya Mahakama Kuu, Wakili Mfinanga alisema wanamalizia
kukamilisha taratibu za wao kukata rufaa Mahakama Kuu na wataomba rufaa
hiyo isikilizwe kwa hati ya dharura ili kumnasua Lema mahabusu.
Jumatano, 23 Novemba 2016
Home »
» MBUNGE Godbless Lema Aingia Siku ya 22 Mahabusu
0 comments:
Chapisha Maoni