WAZIRI
wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye jana alinusuru
kuvunjika kwa mdahalo ulioandaliwa na Jumuiya ya Taasisi za Elimu ya Juu
(TAHLISO), baada ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kuupinga.
Mdahalo
huo ulilenga kujadili hotuba ya Rais Dk. John Magufuli aliyosoma
bungeni Novemba 20, mwaka huu wakati akizindua Bunge la 11.
Dosari
hiyo ilijitokeza mapema kabla ya Nape kuwasili katika ukumbi wa
Nkurumah baadaya Rais wa Serikali ya Wanafunzi wa chuo hicho (DARUSO),
Kataponda Ahadi kusimama na kutoa hoja ya kuwataka wenzake wasusie
mdahalo huo kwa sababu haukubeba ajenda na lengo la TAHLISO.
Hata
hivyo, alikatishwa mazungumzo yake baada ya kuelezwa muda wa kujadili
mada ulikuwa haujaanza, kwa sababu wakati huo mdhamini wa mdahalo huo
ambao ni Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), alikuwa akielezea
faida za mfuko huo.
Baada
ya malumbano yaliyochukua muda kidogo, wanafunzi hao walikubaliana na
hoja ya kuendelea kumsikiliza mwakailishi wa NSSF aliyekuwa
akiwasilisha mada, hadi Nape alipowasili ukumbini hapo.
Katika
hotuba yake, Nape aliusifia mdahalo huo na kusema utasaidia wabunge
watakapo kwenda bungeni wawe na ajenda za wananchi, badala ya kwenda na
ajenda zao ambazo pengine si matatizo wanayopata wananchi.
Alisema
hotuba ya rais, imekuja kwa wakati na imeeleza changamoto nyingi, hivyo
ni muhimu vijana wakawa sehemu ya mabadiliko yanayotakiwa kwa staha na
uwazi.
Aliwataka
wananchi waache utaratibu wa kusikiza na kushangilia tu, bali
waichambue, waikosoe,washauri na kuwasisitiza kuwa wasiache suala la
mabadiliko liwe la Rais Dk. Magufuli tu.
“Lazima
tuhakikishe mabadiliko haya yanaingia kwenye mfumo na yasibaki kwa rais
peke yake ili siku tukimpata mtu mwingine afuate mfumo huo. Inapaswa
tuusukume mfumo ukubali mabadiliko hayo lakini mfumo ukigoma tutapata
matatizo,” alisema Nape.
Baada
ya hotuba hiyo, baadhi ya wanafunzi walinyoosha mikono kutaka kutoa
hoja ambapo mshereheshaji aliwataka wasubiri mada zitakapowasilizwa
wahusika ndiyo wapate muda wa kuzijadili.
Hata
hivyo, wanafunzi hao hawakukubaliana na mwongozo huo na walisimama na
kusema wana hoja ya kumweleza waziri kabla mada hazijawasilishwa na
ndipo mmoja alipopewa nafasi.
Mwanafunzi
huyo ambaye hakuweza kufahamika jina lake, alisimama na kuanza kutupa
lawama kwa TAHLISO kuwa wameshindwa kusikiliza na kujadili matatizo
yanayowakabili wanafunzi wa vyuo vikuu na badala yake wanajihusisha na
mijadala ya kisiasa.
“Tunashangaa
TAHLISO ambayo ni shirikisho la kuwatetea wanafunzi wa vyuo vikuu,
wamekaa kimya kila tunapofikisha matatizo ya wanafunzi, sasa wameona
bora wajadili hotuba ya Dk.Magufuli,” alisema mwanafunzi huyo ambaye
kabla hata hajamaliza kutoa hoja yake aliamriwa kuketi.
Kitendo
hicho kiliamsha hisia kwa wanafunzi wengine, ambao walisimama na kuanza
kupaza sauti wakipinga mdahalo huo kwa madai kuwa hauna maslahi ya
wanafunzi na kwamba ni wa kisiasa.
Hali
hiyo ilimlazimu mshereheshaji kuwaomba askari kuingia ndani ili kuwatoa
wanafunzi hao ambao hata hivyo waliamua kutoka wenyewe wakiongozwa na
rais wao huku wakiendelea kuituhumu jumuiya hiyo.
Walipofika
nje ya ukumbi waliendelea kupiga kelele ambapo iliwalazimu baadhi ya
viongozi wa TAHLISO kutoka nje na kuwataka waondoke katika eneo hilo.
Yaliibuka
mabishano baina ya viongozi wa pande hizo mbili na baadhi ya wanafunzi
ambapo Waziri Nape aliamua kutoka nje na kuacha mdahalo ukiendelea na
alipofika nje aliomba kusikiliza hoja zao.
Akielezea
malalamiko yao, Rais wa DARUSO Ahadi alisema TAHLISO imeshindwa
kusimamia maslahi ya wanafunzi hasa pale wanapoomba kukutana ili
kujadili masuala ya wanafunzi wamekuwa hawajitokezi.
“Hawa
kwenye mambo yanayohusu wanafunzi wanakaa kimya, mdahalo wameweza
kuandaa kujadili hotuba ya Rais Magufuli, zaidi hata huu mdahalo
unaofanyika hapa kwetu sisi viongozi wa DARUSO ambao pia ni wajumbe wake
hatujapewa taarifa, ndio maana tumeamua kuupinga,” alisema Ahadi.
Kwa
upande wake, Waziri wa Mikopo wa DARUSO, Shitindio Venance, alisema:
“Kutokana na kitendo cha jumuiya hii kushindwa kutatua matatizo yetu
tumeamua kuunda Kamati ya Taifa ya kufuatilia Mikopo ya wanafunzi nchi
nzima na hivi tunapozungumza hapa kuna wanafunzi wapatao 80 ambao
wanatakiwa wafungashe warudi nyumbani kwa kukosa mikopo na wengine wapo
Chuo cha Bagamoyo lakini tunashangaa TAHLISO ipo kimya,”alisema.
Naye
Makamu wa Rais wa DARUSO, Irene Ishengoma, alimweleza Nape kuwa pamoja
na kusumbuliwa kwa kunyimwa mikopo, bado Tume ya Vyuo Vikuu nchini (TCU)
imekuwa ikiwatoza sh 20,000 za kuiendesha suala ambalo ilitakiwa
yenyewe itafute mbinu za kujiendesha.
Akijibu
hoja hizo Nape aliwataka viongozi hao kuitisha vikao ili kuwaondoa
viongozi wa TAHLISO ambao wameonekana kushindwa kazi kwani wao ndio
waliowaweka na hivyo wana mamlaka ya kuwaondoa.
“Unajua
tatizo lenu ni dogo…hawa viongozi mmewaweka wenyewe na kwa kawaida
mwiba unapoingilia ndipo unapotokea hivyo nyie ndio wakuwatoa, tumbueni
majipu kama mnaona yapo,” alisema Nape.
Kuhusu
matatizo ya mkopo, Nape aliwaambia tayari yanajulikana na kwamba licha
ya kwamba yeye si waziri mwenye dhamana lakini ni kiongozi wa chama
kilichopo madarakani hivyo atahakikisha leo watahakikisha, tatizo hilo
linakoma.
“Naomba
niwahakikishie kuwa ikifika kesho (leo) wanaohusika tutakwenda
kuwashughulikia ili wakawajibike kwa sababu inaonekana kuna tatizo maana
wanafunzi wakigoma fedha zipo lakini wakikaa kimya hawapewi,” alisea
Nape.
Nape
alifanikiwa kumaliza dosari hiyo iliyodumu kwa dakika 20 baada ya
kuwaomba wanafunzi hao warudi ukumbini ili kuendelea na mdahalo
kwasababu kama ni matatizo yao yamefika sehemu husika ambapo walikubali
na kurudi ukumbini.
Ndani
ya ukumbi huo mada zilikuwa zinaendelea ambapo akichambua hotuba ya
Rais Magufuli, Mtaalamu wa Mambo ya Uchumi na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha
Mzumbe, Dk. Honest Ngowi alisema kiuchumi suala la elimu bure halipo
kwani elimu hiyo inalipiwa kwa ruzuku ya serikali kwa asilimia 100.
Alisema
ili kuweza kutekeleza hilo wananchi wanatakiwa kukubali kulipa kodi
zilizowekwa kwasababu ndizo zitakazotumika kuendesha sekta hiyo.
Naye
Mtaalamu wa Sayansi ya Siasa (UDSM), Dk. John Jingu alisema hotuba hiyo
ilijikita katika dira ya maendeleo ya Taifa ifikapo mwaka 2025 ya kuwa
na uchumi wa kati, kwani rais ameweza kuonesha njia na nia ya kutekeleza
dira hiyo.
Kwa
upande wake Mwanadiplomasia mkongwe, Balozi Christopher Liundi alisema
hotuba ya Rais Magufuli imekuwa mfano kwa viongozi wa chini yake, kwani
wanaonekana kutenda kwa kasi yake tangu aingie madarakani.
Jumatatu, 14 Desemba 2015
Home »
» Mdahalo Wa Tahliso Kujadili Hotuba ya Magufuli Waingia Dosari Baada Ya Wanafunzi wa UDSM Kuupinga
0 comments:
Chapisha Maoni