CHAMA CHA DEMOKRASIA NA MAENDELEO (CHADEMA)
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI JUU YA MAAZIMIO YA KIKAO CHA KAMATI NDOGO YA KAMATI KUU
1.0 UTANGULIZI
Kikao cha Kamati Ndogo ya Kamati Kuu cha dharura kilichoketi tarehe 14
Februari, 2017 Jijini Dar es Salaam katika Hoteli ya Bahari Beach
kilipata nafasi ya kujadiliana kwa kina kuhusu matukio mbalimbali
yanayoeendelea hapa nchini ikiwa ni pamoja na kutolewa kwa kauli
mbalimbali na viongozi wa kiserikali na ambazo zimeendelea
kuuthibitishia umma wa watanzania kuwa nchi yetu haiendeshwi kwa misingi
ya kuzingatia Katiba, Sheria na Kanuni tulizojiwekea kama Taifa .
Aidha Kamati hiyo ilipata muda wa kutafakari kwa kina zaidi juu ya
Operesheni UKUTA ambayo tumeendelea kufanikiwa katika kuitekeleza kwa
vitendo na pia watanzania wengi zaidi sasa wameona umuhimu wa kuendelea
na Operesheni UKUTA kwani Taifa linaelekea kwenye kutumbukia kwenye
utawala wa kutokufuata Katiba na Sheria za Nchi (Udikteta kamili).
Mwalimu Nyerere Julai 19, 1967 alisema hivi kuhusu udikteta “Udikteta
ni serikali ya mtu mmoja au kikundi cha watu wachache na wao ndiyo huwa
sheria.Anayepinga watakayo,basi huonyeshwa cha mtema kuni”
Kamati hiyo imejiridhisha bila shaka kuwa sasa Chama chetu kinawindwa na
watawala pamoja na Rais Mwenyewe na hii ni katika kuelekea kufikia
lengo la Rais alilolitangaza alipokuwa Singida mwezi Juni ,2016 ya
kuhakikisha kuwa upinzani unakufa ,ifikapo au kabla ya mwaka 2020.
Aidha Kamati hiyo imejiridhisha bila shaka ya kuwa sasa zinatengenezwa
chuki za makusudi baina ya vyombo vya dola na wananchi . Hii inatokana
na ukweli kuwa Amiri Jeshi Mkuu alisikika akiagiza Polisi wawe na
utaratibu unaofanana na Jeshi la Wananchi. Hii ina maana kwamba Polisi
lisiwe tena ni jeshi la kulinda wananchi na mali zao bali ni jeshi la
kuilinda serikali .
Tumeshaona tayari Polisi wamepiga marufuku (Tamko la Advera –msemaji wa
jeshi la Polisi) wananchi kwenda kuwatembelea ndugu , jamaa na marafiki
wanapokuwa katika vituo vya polisi bila hata kutaja kifungu cha sheria
kinachowapa mamlaka hayo.
2.0 KAMATAKAMATA NA FUNGAFUNGA YA WAPINZANI
Mara baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2015 viongozi na wanachama wa CHADEMA
wamekuwa wakikamatwa na kushtakiwa kwa makosa ya kubambikiziwa kwa
kisingizio cha uchochezi na mpaka sasa kuna jumla ya wanachama na
viongozi 215 ambao wamefunguliwa kesi zaidi ya 78 katika nchi nzima
.Wengi wao wamenyimwa dhamana bila sababu za msingi . Na wale ambao
walipatikana na hatia walipewa adhabu za vifungo bila ya kupewa fursa ya
faini.
Hivi sasa umekuwa ni mtindo kwa mahakama kuwakatalia dhamana wanachama
wa CHADEMA bila ya sababu za msingi.Pia imekuwa ni mtindo kuwahukumu
vifungo bila kuwapa fursa ya kulipa faini.
Tumeamua na tunandaa orodha kamili itakayoainisha kesi zote za jinai
ambazo ziko mahakamani na kuonyesha aina ya mashtaka na vifungo
vilivyotolewa ambayo itawekwa wazi kwa vyombo vya habari na taasisi za
ndani na nje ya nchi kuthibitisha kuwa kuna mpango wa kuwafunga viongozi
wa upinzani kwa kusudi ili kuudhoofisha upinzani.
3.0 VITUKO VYA MKUU WA MKOA WA DAR ES SALAAM KUTANGAZA MAJINA YA WATU HADHARANI KUWA WANAHUSIKA NA DAWA ZA KULEVYA
Chama kinaunga mkono jitihada za dhati za kupambana na madawa ya kulevya
nchini, kama sheria na taratibu tulizojiwekea zitafuatwa kikamilifu
wakati wa mapambano hayo.
Kamati kuu inalaani kwa nguvu zote kitendo cha Mkuu wa Mkoa wa Dar es
Salaam (Paul Makonda) kutangaza majina ya watu mbele ya vyombo vya
habari na kuwatuhumu kuwa ama wanahusika katika kusambaza, kuuza au
kutumia madawa ya kulevya kwa lengo la kuwachafulia majina,
kuwadhalilisha,kuwafedhehesha na kuwaondolea heshima yao kwa umma
.Tunalaani kitendo hiki kwa sababu zifuatazo:
i. Mkuu wa Mkoa amekiuka masharti ya Katiba ibara ya 13(6) (b) na (e)
ambavyo vinaweka bayana kuwa mtu hatachukuliwa kuwa ametenda kosa la
jinai mpaka itakapothibitika kuwa anayo hatia ya kosa hilo na kuwa ni
marufuku kwa mtu kuteswa ,kuathibiwa kinyama au kupewa adhabu
zinazomtweza au kumdhalilisha
ii. Mkuu wa Mkoa amekiuka kifungu cha 54 cha Sheria ya Mwenendo wa Mashtaka ya Jinai
iii. Mkuu wa Mkoa hana mamlaka kwa mujibu wa sheria iliyotungwa na Bunge
inayompa kazi na majukumu yake yaani ‘sheria ya Tawala za Mikoa ya
1997’ kuwa ana wajibu wa kutaja majina ya watu anaowatuhumu kuhusika na
madawa ya kulevya .
iv. Mkuu wa Mkoa alikiuka ‘sheria ya Kuthibiti na kupambana na dawa za
Kulevya,2015’ ambayo haimpi mamlaka ya kutangaza na au kuwataka watu
ambao yeye anawatuhumu kujihusisha na usambazaji, uuzaji na au utumiaji
wa dawa za kulevya kufika katika vituo vya Polisi .
v. Mkuu wa Mkoa alienda kinyume kabisa na mila na desturi za Kitanzania
,kuwachafulia watu majina na kuwadhalilisha mbele ya jamii huku akijua
kuwa hawezi kuwasafisha na wengine ni viongozi wa dini ambao wanaaminiwa
na waumini wao .
4.0 HATUA
a. Kamati hiyo inaunga mkono hatua ya Mwenyekiti wetu Taifa
Mhe.Freeman Mbowe (MB) ya kumfungulia kesi ya Kikatiba na ya Madai Paulo
Makonda katika Mahakama Kuu ya Tanzania na itaungana naye katika kesi
hiyo kwa kumpatia mawakili wa Chama .
b. Aidha inatoa wito kwa wale wengine wote ambao walitajwa na wanaamini
kuwa walionewa,kuchafuliwa majina na au kudhalilishwa wafungue mashauri
mahakamani , kwani hii ndio njia pekee ya kuzuia wengine wasifanyiwe
uonevu kama huu siku zijazo.
c. Kamati hiyo inawapongeza kwa dhati kabisa wabunge wote wa Bunge la
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kukubaliana, kuungana na kuweka
itikadi za vyama vyao pembeni wakati wa mjadala wa kulinda hadhi na
madaraka ya Bunge. Inatoa rai kuwa waendeleze moyo huohuo kwa siku
zijazo kwa maslahi mapana ya Taifa letu.
5.0 HITIMISHO.
Kamati hiyo inatoa wito ufuatao kwa viongozi, asasi za Serikali,
wananchi wazalendo na wanachama wa CHADEMA, kufanya mambo yafuatayo;
1. Viongozi wana wajibu wa kuitetea ,
kuilinda na kuitekeleza Katiba ya Jamhuri ya Muungano na Sheria za Nchi.
Mwalimu Nyerere aliwahi kutuasa kuwa Rais asiyeweza kuilinda,kuitetea
na kuihifadhi Katiba hatufai.
2. Mahakama Itekeleze wajibu wake kwa
weledi uliotukuka kuhakikisha kuwa haki sio tu inatendeka bali
inaonekana kutendeka bila ya vitisho kwake kutoka kwa mtu yeyote.Iige
mfano wa uhuru wa mahakama na weledi wa Majaji wa Afrika ya Kusini,
Zimbabwe na Marekani ambao waliweza kutengua amri batili zilizotolewa na
Marais wa nchi zao.
3. Polisi na Jeshi la Wananchi wa Tanzania watekeleze
majukumu yao kwa weledi kwa mujibu wa sheria na taratibu
zilizowekwa.Wasikubali kuwaonea watu kwa misingi ya Vyama ,Itikadi au
misimamo yao.Polisi Wajibu wao Kisheria ni kulinda usalama wa raia na
mali zao , Jeshi la Wananchi wa Tanzania wajibu wao Kikatiba ni kulinda
mipaka ya Nchi.
4. Mawakili wana wajibu mkubwa kuisaidia
mahakama kutekeleza majukumu yake kwa weledi kuhakikisha haki
inatendeka bila woga ,vitisho au vishawishi .Wasikubali kutishwa na mtu
au asasi yeyote katika kuitetea ,kuilinda na kuitekeleza Katiba na
Sheria za Nchi.
5. Wasomi na wanataaluma wana wajibu wa
kutambua na kuitikia mwito wao wa kutetea ukweli na kulinda haki za
jamii hata kama kwa kufanya hivyo kutaathiri maslahi yao binafsi
6. Wanachama tuendelee kudai demokrasia
kwa nguvu zote bila woga kwa mujibu wa Katiba na sheria za
Nchi.Tushikamane kukikuza Chama kuanzia ngazi ya Misingi hadi Taifa
kuendelea na Operesheni UKUTA .
7. Wananchi nchi hii ni yetu sote ni
lazima tufaidike nayo kwa mujibu wa Katiba na Sheria za nchi bila
vitisho .Tuungane kudai demokrasia na uhuru wa kweli wa kisiasa na
kiuchumi. Wasikubali kuyumbishwa na mbinu ovu kama hizi ambazo zimelenga
kutupotezea lengo la kuhoji masuala ya msingi kama ufaulu hafifu wa
matokeo ya Kidato cha nne Mkoa wa Dar Es Salaam, hali ya chakula nchini
(njaa),zilipo milioni 50 za kila kijiji zilizoahidiwa , upatikanaji wa
Tume huru ya Uchaguzi,Katiba Mpya na hali mbaya ya kiuchumi kwa wananchi
.
Mwisho Kamati Ndogo ya Kamati Kuu inawashukuru watanzania wote kwa
kuendelea kuunga mkono jitihada za kupambana na udikteta nchini na
inawaomba waendelee kuwakumbuka kwa sala/dua viongozi mbalimbali wa
Chama waliopo kwenye mateso ya kesi, mahabusu na wengine wanatumikia
vifungo kutokana na kuonewa na watawala.
……………………
Prof. Abdalah Jumbe Safari
Makamu Mwenyekiti Taifa –Bara
16 Februari, 2017
Prof. Abdalah Jumbe Safari
Makamu Mwenyekiti Taifa –Bara
16 Februari, 2017
0 comments:
Chapisha Maoni