Chama
cha Madaktari Tanzania (MAT) kimesema Chuo Kikuu cha Kimataifa cha
Matibabu na Teknolojia (IMTU) sanjari na hospitali iliyo chini yake,
vinastahili kufungiwa.
Tamko
hilo la chama limekuja huku mamlaka mbalimbali zinazohusika na
usimamizi wa karibu wa vyuo vikuu vya matibabu zikikiweka chuo hicho
kiporo, kusubiri uchunguzi wa tuhuma zinazokikabili za kutupa viungo
vya binadamu jalalani, ukamilike kabla ya kuchukua hatua zinazostahili.
Kitendo
hicho cha kutupa viungo vya binadamu jalalani kimetajwa na watu
mbalimbali, wakiwemo wataalamu kuwa ni cha ajabu kinachodhalilisha nchi
na utu wa binadamu.
Akizungumza
na mwandishi wa habari hizi, alisema taasisi hiyo isingetakiwa kutoa
mafunzo ya udaktari wala kufanya tafiti zozote, ikiwa ni pamoja na
kutoruhusiwa kutoa huduma za afya katika hospitali yake.
Mwingine
aliyezungumzia sakata hilo ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge
ya Huduma za Jamii, Margareth Sitta aliyepongeza taasisi za serikali kwa
hatua za haraka walizochukua kuhakikisha watu hao wanabainika mapema na
kukamatwa.
Hata
hivyo, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii pamoja na Tume ya Vyuo Vikuu
(TCU) kwa nyakati tofauti, walisisitiza nia yao ya kuchukua hatua dhidi
ya chuo hicho, mara jopo linalochunguza sakata hilo litakapokamilisha
kazi yake.
Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Kebwe Stephen alisema kwamba amesikitishwa na kitendo hicho ambacho si cha kawaida.
Alitaka upelelezi ufanyike haraka, adhabu stahiki ichukuliwe kutokana na kitendo hicho.
“Baada
ya kukamilika kwa upelelezi wa tukio hili na kupata taarifa za kwa nini
walifikia hatua hii, naahidi wizara yangu itachukua hatua kali,” alisema Kebwe.
Katika
mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, msemaji wa
wizara hiyo, Nsachris Mwamwaja alisema kutokana na kuwa jambo hilo ni
jipya, wataangalia uwezekano wa kuchukua hatua kwa mujibu wa sheria za
nchi.
Alisema
ingawa wizara yake haihusiki na usimamizi wa vyuo hivyo vinavyozalisha
madakatri na kutaka waulizwe TCU, kwa mujibu wa Mwamwaja, kitendo
walichofanya madaktari husika si cha kimaadili.
Alisema pamoja na kuwa kitendo hicho si cha maadili pia wanaangalia madhara ya kiafya kulingana na tukio hilo.
“Lakini
pia ni vema kuangalia na jiji (Dar es Salaam) ni jinsi gani wanasimamia
madampo yao, kwa nini inaruhusu kumwaga uchafu wowote bila kuwepo
wakaguzi au ni utaratibu gani wanatumia kulinda afya za wananchi,”alisema Mwamwaja.
Kwa
upande wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi yenye dhamana na vyuo
vikuu, Katibu Mkuu wake, Profesa Sifuni Mchome alisema pia wanasubiri
ripoti ya timu iliyoundwa kuchunguza suala hilo wachukue hatua za
haraka chini ya Tume ya Vyuo Vikuu (TCU).
“Kwa sasa uchunguzi unaendelea hivyo hatuwezi kuchukua hatua yoyote,” alisema Profesa Mchome. Katibu Mkuu alisema katika tume hiyo iliyoundwa na polisi, yumo mwakilishi wa elimu kutoka TCU.
Alisisitiza
wataangalia suala hilo na kupendekeza hatua za kuchukua kutokana na kwa
sasa hakuna sheria inayowabana kutokana na kuwa suala hilo ni jipya
nchini.
Akizungumzia
tukio hilo, Ofisa Habari Mwandamizi wa TCU, Edward Mkaku alisema
wanasimamia ubora wa elimu ya juu na suala lililotokea ni kesi ya chuo
kwa asilimia 100.
Hata
hivyo, alisema kwa kuwa Mkurugenzi wa Ithibati wa Elimu ya Juu katika
tume hiyo yupo kwenye tume iliyoundwa, wataangalia hatua za kuchukua
baada ya uchunguzi kukamilika.
Alisema
TCU ni taasisi yenye utaratibu, hivyo itatoa uamuzi baada ya ripoti kwa
kuwa sasa IMTU bado ni watuhumiwa na haipaswi kuhukumiwa.
“Tunasubiri
tume imalize uchunguzi ndipo tutaona tutachukua hatua gani kulingana
na Sheria ya Vyuo Vikuu kwani kwa sasa sheria ya suala hilo haipo
kutokana na kwamba ni jipya kutokea nchini,”alisema.
Wakili
wa Kujitegemea kutoka MK Law Chambers, Karoli Mluge akizungumza nafasi
ya sheria katika suala hilo, alisema hakuna sheria inayozungumzia kwamba
kutupa viungo vya binadamu au mwili hadharani ni kosa.
Mluge
alisema jamii lazima itofautishe Sheria na suala zima la maadili na
ubinadamu. Alisema kibinadamu na maadili, utupaji wa viungo vya binadamu
si sahihi na ni jambo linaloshitua lakini kisheria, haimtii mtu
hatiani .
“Kimaadili si sawa, lakini suala hili ni la kiubinadamu halina sheria,” alisisitiza.
Alisema hata mtu anapokutwa na kiungo cha binadamu, hatiwi hatiani kwa
maana ya kukutwa na kiungo husika isipokuwa, kinachotafutwa ni
kujiridhisha ni kwamba amekipataje kutoka mwili wa binadamu.
“Si kosa kukutwa na kiungo cha binadamu…cha msingi, ni kuthibitisha umekipataje,” alisema.
Kumekuwepo
maswali juu ya ni namna gani vyuo vinapata miili ya kufanyia mafunzo
kwa vitendo na baada ya mafunzo inapaswa iteketezwe namna gani. Hata
hivyo katika kutafuta ufafanuzi wa maswali haya, taasisi hizo
zinazohusika na usimamizi wa vyuo hazikuwa tayari kuzungumzia kwa undani
suala hilo, kwa madai ya kusubiri matokeo ya tume iliyoundwa.
Tume
hiyo iliyoundwa, kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar
es Salaam, itahakikisha inakuja na majibu, ikiwa ni pamoja na kujua
idadi kamili ya watu wenye viungo hivyo.
Timu
hiyo ya wataalamu ya watu saba inayohusisha pia Mkemia Mkuu wa
serikali, itakuja na majibu viungo hivyo ni vya muda gani na zilitumika
kemikali gani kuvikausha.
Jopo
litabaini pia kama ipo sheria na ni ipi inavunjwa. Inalenga kubaini
pia kama upo uzembe katika kulinda viungo vya binadamu na vinapatikanaje
kwa ajili ya mazoezi.
Katika
sakata hilo lililovuta hisia za watu na kuzua mjadala mitaani na kwenye
mitandao ya kijamii, watu wanane wakiwemo Madaktari wa IMTU,
walikamatwa juzi na Polisi kwa mahojiano wakituhumiwa kuhusika katika
utupaji viungo vya binadamu jalalani.
Polisi
ilisema mifuko ipatayo 85 yenye vichwa, miguu, mikono, moyo, mapafu,
vifua na mifupa ya aina mbalimbali ya binadamu, ilikutwa maeneo ya bonde
la Mbweni Mpiji, eneo la Bunju jijini Dar es Salaam.
0 comments:
Chapisha Maoni