Bwana Taj Hargey anasema msikiti huo unawalenga watu wenye mawazo chanya
Msikiti ambao unasemekana kuunga
mkono watu wanaoshiriki mapenzi ya jinsia moja, na ambao pia wanawake
wataruhusiwa kuswali ndani,umefungwa.
Afisaa mmoja mjini Cape
Town, anasema kuwa msikiti huo umevunja sheria za baraza la jiji kwa
kukosa nafasi za kuegesha magari ya waumini.
Msikiti huo, ulifunguliwa rasmi siku ya Ijumaa wiki jana licha ya kukosolewa na waumini wa kiisilamu katika eneo uliko.
Mwanzilishi
wa msikiti huo, Taj Hargey, alisema kuwa msikiti huo utasaidia katika
kupambana na kuenezwa kwa itikadi kali za kidini.
''Tunafungua
msikiti huu kwa watu walio na muonekano chanya kwa baadhi ya mambo wala
sio wenye muonekano finyu,'' alisema bwana Hergey kabla ya ufunguzi wa
masikiti huo.
Kadhalika bwana Hargey alikana kwenda kinyume na mafunzo ya dini ya kiisilamu.
Maafisa wa baraza la jiji wamekanusha madai kuwa kufungwa kwa msikiti huo ni kwa nia mbaya.
Msikiti huu umefungwa kutokana na kukosa nafasi za kuegeshea magari
"swala hili linazua sana hisia, baadhi ya maafisa wa baraza la jiji,
ambao ni waisilamu wangeteka kuunga mkono kufungwa kwa msikiti huo,
lakini wasio waisilamu wangependa kuuona ukiwa wazi, lakini cha muhimu
hapa ni kwamba, tungetaka kuona sheria ikifuatwa, '' alisema afisa mmoja
wa baraza la jiji.
Inaarifiwa kuwa bwana Hargey hakuomba idhini
ya kuruhusu jengo lililokuwa likitumiwa kama sehemu ya kuweka vitu
kubadilishwa na kuwa msikiti.
Kuambatana na masharti ya baraza la
jiji, kila sehemu ya maombi inapaswa kuwa na sehemu ya kuegeshea magari
ya waumini lakini msikiti huo hauna sehemu hiyo.
Shughuli ya kuwasilisha maombo ya kuwezesha kuwepo sehemu ya kuegeshea magari huenda ikachukua hadi miezi sita.
Bwana Hargey aliambia BBC kwamba anaamini kuwa kila kitu kiko shwari.
Wanawake wataruhusiwa kuswali pamoja na wanaume na hata kuongoza maombi.