
Uhasama wa kiutendaji kati ya vyombo vya habari
na vya ulinzi na usalama nchini Tanzania huenda ukapungua kwa kiasi
kubwa baada ya pande hizo kuanza kukaa pamoja na kujadili mambo
yanayokwamisha utekelezaji wa majukumu yao.
Baraza la Habari
Tanzania limeitisha mkutano wa mashauriano kati ya vyombo vya habari na
vyombo vya ulinzi, usalama na sheria ili kutambua kazi, haki na wajibu
wa kila upande kwa maslahi ya umma.
Kila upande umekuwa ukitetea
kuwa unatekeleza majukumu yake kwa maslahi ya umma. Hata hivyo vyombo
vya habari ndivyo ambavyo vimeelekeza lawama zaidi kwa vyombo vya ulinzi
na usalama kuwa vinakandamiza uhuru wa vyombo vya habari kupata na
kutoa taarifa zenye maslahi kwa umma.
Kwa upande wake vyombo vya
ulinzi na usalama vimekuwa vikivilaumu vyombo vya habari kwa kutoa
habari na hata kulazimisha kutoa habari zinazohatarisha usalama wa umma.
Akizungumza
katika mkutano huo Makamu wa Rais wa Tanzania Dokta Gharib Bilal
amesema katika ulimwengu wa sasa suala la habari limetanuka kiasi kwamba
sheria zilizopo kusimamia vyombo vya habari hazina budi kuangaliwa upya
ili kukidhi mazingira ya sasa.
“Si rahisi tena kudhibiti
mawasiliano ama taarifa kwa kutumia sharia tulizojiwekea kama nchi maana
jambo linaweza kudhibitiwa nchi moja na kutangazwa nchi nyingine na
likarejea kule kule lilikodhibitiwa.” Amesema.
Hata hivyo Dokta Bilal amesema kuna umuhimu wa kuangalia mbinu za kukabiliana na mawasiliano yenye kuhatarisha usalama wa umma.
Amesema vyombo vya habari na vyombo vya usalama vina mipaka ya utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.
Dokta
Bilal amesema mikwaruzano ya vyombo hivi inatokana na chombo kimoja
kutaka kupata habari hata katika mazingira ambayo vyombo vya usalama
vinaona ni hatari.
Kwa upande wake katibu mtendaji wa Baraza la
Habari Tanzania Mukajubi Mukajanga amesema,”vyombo vya usalama na sheria
na vyombo vya habari vina uhusiano wa mashaka.Kuna wakati ambao
wanadhani wanahitajiana wanakuja pamoja na kuna wakati ambapo kuna
uhasama mpaka watu wanapigwa….”
Bwana Mukajanga amesema kutokana
na umuhimu wa vyombo hivi kushirikiana katika masuala mbalimbali ya
kijamii, baraza lake likaamua kuwakutanisha pamoja ili kujenga moyo wa
kuaminiana.
Baraza la Habari Tanzania limewakutanisha waandishi wa
habari na vyombo vya ulinzi na usalama ili kujadili mambo
yanayokwamisha utekelezaji wa majukumu yao.