Wakati
Rais John Magufuli akitimiza siku 31 akiwa amejifungia Ikulu kutatua
kero za nchi bila kusafiri nje ya nchi, Rais mstaafu Jakaya Kikwete
(pichani) ameendelea kujumuika katika hafla za kimataifa baada ya
kuonekana nchini Afrika Kusini juzi akiwa mwalikwa wa Mkutano wa China
na Afrika.
Tangu
aingie madarakani Novemba 5, Rais Magufuli amepiga marufuku safari za
nje kwa watendaji wa serikali bila ya kibali maalumu cha Ikulu.
Alifikia
uamuzi huo baada ya kubainisha katika hotuba yake ya ufunguzi wa Bunge
la 11 mwezi uliopita kuwa safari za kimataifa zinatafuna mabilioni ya
fedha za walipa kodi.
Rais
Magufuli hajasafiri kwenda nje ya nchi mbali na kwenda Dodoma kwa ajili
ya kumwapisha Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na kuzindua Bunge.
Picha
zilizotumwa na Ofisi ya Makamu wa Rais jana, zilimwonyesha JK akiwa na
Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan, aliyemwakilisha Rais Magufuli kwenye
Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika na China, uliomalizika jana jijini
Johannesburg.
JK
ameonekana katika picha hizo akitembelea mabanda ya maonyesho ya
mkutano huo ulioandaliwa na China ili kujadili mikakati ya ushirikiano
baina yake na Afrika.
Ni
mara ya pili kwa Kikwete kwenda nje ya nchi tangu Rais Magufuli aingie
madarakani. Novemba alionekana katika Jiji la Addis Ababa Ethiopia.
Kwenye
utawala wake wa miaka 10, Rais mstaafu huyo alilaumiwa kusafiri mara
nyingi nje ya nchi akiwa na msururu wa viongozi na wasaidizi wake hivyo
kutumia gharama kubwa, lakini alijitetea kuwa huenda nje kutafuta fedha
za maendeleo.
Wakati
akihutubia Bunge mjini Dodoma mwezi uliopita Rais Magufuli alisema
safari za nje ziliigharamu nchi Sh. bilioni 356 kuanzia mwaka 2013 hadi
2015.
Alisema
kati ya kiasi hicho karibu Shilingi bilioni 200 zilitumiwa kwa tiketi
za ndege, kadhalika bilioni 68 zilitumiwa kwa mafunzo ya nje wakati
bilioni 104 ziliishia kwenye mifuko ya vigogo na maofisa kwa ajili ya
posho.
Rais
Magufuli alisema mabilioni hayo ya safari yangejenga kilometa 400 za
barabara kwa kiwango cha lami akitaja ile inayotoka Urambo Tabora hadi
Kigoma mjini.
Katika
kutimiza azma ya kupinga safari za nje , Rais Magufuli alikacha kwenda
kwenye mkutano wa wakuu wa nchi wa Jumuiya ya Madola, uliofanyika visiwa
vya Malta wiki mbili zilizopita.
Aliagiza
Balozi wa Tanzania jijini London Uingereza na maofisa wengine wanne
kuiwakilisha nchi kwenye mkutano huo hatua iliyookoa karibu Shilingi
milioni 700 ambazo zingegharamia safari hiyo.
0 comments:
Chapisha Maoni