Aliyekuwa Kamanda wa Polisi Kanda
Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna mstaafu Alfred Tibaigana amesema Rais
John Magufuli amepatikana wakati sahihi, kwa kuwa nchi inamhitaji
kiongozi ambaye akitoa amri inatekelezwa mara moja.
Kauli ya Tibaigana inakuja takribani
miezi 15 tangu aliposema anatamani kuiona Tanzania ikimpata rais dikteta
kwa kuwa nchi haiwezi kupiga hatua iwapo mkuu wa nchi hataweza kukemea
na kutoa amri watu wakatii.
Akizungumza katika mahojiano maalum na
gazeti hili nyumbani kwake katika Kijiji cha Katare, wilayani Muleba
Mkoa wa Kagera, hivi karibuni, Tibaigana alisema anaamini changamoto
nyingi zinazowakabili Watanzania zitatatuliwa na Rais Magufuli.
Akitolea mfano utaratibu wa Rais
Magufuli wa kufanya ziara za ghafla kwenye sekta mbalimbali za umma,
Tibaigana alisema: “Watu hawafanyi kazi na viongozi ni waoga wa kutoa
uamuzi, ziara ya Rais Magufuli (Hospitali ya) Muhimbili imesababisha
hospitali nyingi kuboresha huduma, siyo lazima afike kila mahali akitoa
kauli hatua ichukuliwe.”
Kamanda huyo mstaafu alisema hata uamuzi
wa Rais Magufuli wa kufuta safari za nje kwa viongozi wa umma mpaka kwa
kibali maalumu, umekuja wakati mwafaka kwa kuwa baadhi ya safari
hazikuwa na masilahi kwa taifa.
“Safari zinatumia pesa nyingi na
nyingine huwa siyo za lazima, kwa uzoefu wangu wa kukaa Serikalini hata
baadhi ya wafanyakazi wa ndani hulipwa kama waajiriwa kwa kufanyiwa
mipango na mabosi wao,’’ alisema.
Tibaigana ambaye aliwahi kugombea ubunge
Jimbo la Muleba Kusini miaka mitano iliyopita kupitia CCM na kushindwa
kwenye kura ya maoni, alipendekeza Bunge la 11 kufanyia marekebisho
baadhi ya sheria ili ziwe kali kwa watu wanaohujumu uchumi.
Maagizo yatekelezwa
Kauli ya Tibaigana imekuja wakati Rais
Magufuli ameanza kazi ya kutafuta na kuziba mianya ya upotevu wa fedha,
alianzia Hazina na kupiga marufuku safari zote za nje kwa viongozi na
kusema zitakuwa zinaruhusiwa kwa kibali maalumu.
Dk Magufuli pia aliamuru mashine za MRI
na CT-Scan katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) zitengenezwe na
kuagiza Sh3bilioni zitolewa kugharimia matengenezo kati ya Sh7bilioni
zilizokuwa zinahitajika.
Vilevile, aliagiza Sh4bilioni zilizokuwa
zitumike katika Maadhimisho ya Sherehe za Uhuru Desemba 9, kutumika
kupanua barabara ya Morocco kwenda Mwenge, kazi ambayo utekelezaji wake
unaendelea.
Rais huyo wa Awamu ya Tano na Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa kwa nyakati tofauti walitembelea maeneo muhimu kwa
uchumi wa nchi kama Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bandari na
Kampuni ya Reli Tanzania (TRL) na kuibua vitendo vya ufisadi na ukwepaji
wa kodi.
Akizungumzia hali hiyo, Mhadhiri
Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Benson Bana anasema
kinachoonekana ni uzembe au udhaifu kwa watumishi wa umma ambao mbali na
kuwa wazito katika kutoa uamuzi, lakini ni wazito katika kutambua uzito
wa tatizo.
Alisema lipo tatizo kubwa kwa viongozi
wengi kukosa uwajibikaji licha ya dhamana kubwa walizopewa na kusema
wakati umefika wa kuangalia upya mfumo wa uteuzi wa viongozi wa ngazi
mbalimbali nchini.
“Hii ni dalili ya kuwa na viongozi
wasiowajibika…maana haiwezekani mashine muhimu inaharibika na mkurugenzi
na madaktari wake wanakaa kimya tu kama vile hakuna kilichotokea… hii
inaonyesha kuwa tabia ya uwajibikaji haipo serikalini,” alisema Dk Bana.
Alisema kama ambavyo wafanyakazi wa
Serikali wanaweza kudai mishahara kwa kugoma, kunapotokea kukosekana kwa
vitendea kazi, watumie nguvu ileile kudai ili waweze kufanya kazi.
Alisema haiingii akilini kuona baadhi ya
watendaji wa Serikali wakiwamo wakuu wa mikoa, wilaya na hata makatibu
wakuu kukaa kimya licha ya Rais kuonyesha njia kipindi kifupi tangu
ashike nafasi hiyo.
Profesa George Shumbusho wa Chuo Kikuu
cha Mzumbe alisema uchapaji kazi wa viongozi katika eneo lolote
unategemea na umakini na ufuatiliaji wa kiongozi mkuu.
“Baba katika familia akiamua mambo
yaende yataenda tu… ni kawaida katika mabadiliko, binadamu kujaribu
wakiona huna mchezo watafanya kazi wakiona ni nguvu ya soda mtarudi kule
kule” alisema Profesa Shumbusho.
Alisema watendaji walio wengi
walionekana kulala na kufanya kazi kwa mazoea kutokana na wakuu wao na
akasema sasa wameanza kuamka kutokana na kasi ya mtendaji mpya na
akasema kasi ya utendaji inaweza ikawa kubwa zaidi endapo rais naye
ataendelea kuonyesha njia.
Jumapili, 6 Desemba 2015
Home »
» Tibaigana Afunguka...Huyu Ndiye Rais Niliyemtaka
Tibaigana Afunguka...Huyu Ndiye Rais Niliyemtaka
Related Posts:
EPL: Matokeo ya Chelsea vs Swansea City Mchaka mchaka wa ligi kuu ya England umeendelea tena jioni hii kwa mchezo uliowakutanisha vilabu viwili vilivyokuwa vikishika nafasi ya kwanza na ya pili katika msimamo wa ligi kuu ya England – Chelsea dhidi ya Swansea. … Read More
La Liga: Matokeo ya FC Barcelona dhidi ya Athletic Bilbao Ligi kuu ya Hispania maarufu kama La Liga imeendelea leo kwa michezo kadhaa kupigwa – FC Barcelona waliikaribisha Athletic Bilbao kwenye dimba la Nou Camp. Mchezo huo uliomalizika muda mfupi uliopita umeisha kwa matokeo y… Read More
EPL: Kilichoikuta Liverpool dhidi ya Aston Villa hiki hapa EPL: Kilichoikuta Liverpool dhidi ya Aston Villa hiki hapa Kwa mara ya nne mfululizo klabu ya Liverpool imekuwa ikikosa matokeo chanya kwenye uwanja wa nyumbani wa Anfield kila inapocheza na kikosi cha Paul Lambert – Aston Villa. Leo hii wakiwa nyumbani Liverpool huku ikiwacheze… Read More
EBOLA INAENEA KWA KASI NCHINI LIBERIA. Ugonjwa wa Ebola unaenea kwa kasi nchini Liberia huku maelfu ya watu wakiambukizwa upya na idadi hiyo inatarajiwa kuongezeka katika muda wa wiki tatu zijazo. Hii ni kwa mujibu wa shirika la afya duniani WHO. Shirika hilo … Read More
NYAMA YA KIBOKO YAWALETEA MAAFA. Watu kumi walikanyagwa na gari lililokuwa linakwenda kwa mwendo wa kasi walipokuwa wanajaribu kujipatia angalau kipande cha nyama ya Kiboko mwishoni mwa wiki. Taarifa hii ni kwa mujibu wa mtandao wa Daily Nation. Kiboko … Read More
0 comments:
Chapisha Maoni