Jumamosi, 5 Desemba 2015

Wabunge: Magufuli Futa Wakuu wa Wilaya na Mikoa

BAADHI ya wabunge kutoka Chama cha Mapinduzi (CCM)  kutoka mkoa wa Dodoma wamemshauri Rais John Magufuli kuondoa nafasi za Ukuu wa Mikoa na Wilaya na badala yake kazi hizo zifanywe na Makatibu tawala wa mikoa na Wakurugenzi wa halmashauri husika. 

Wakizungumza  kwa masharti ya kutokutaka kutajwa majina wabunge hao walisema hakuna sababu yoyote ya kuwepo kwa Mkuu wa Mkoa wala Mkuu wa wilaya kwani hawana kazi na badala yake ni kuiogezea mzigo serikali.
Mmoja wa wabunge kutoka kati ya majimbo ya Nyanda za juu kusini,alisema ili kudhiilisha kuwa wakuu wa mikoa na wilaya hawana kazi ni hivi tu ambavyo wanaonekana kukurupika kwa kuwawajibisha watumishi waliopo chini yao.

“Inasikitisha kuona wakuu wa Wilaya na Mikoa wanavyokurupuka kwa sasa kuwawajibisha watendaji ambao wapo chini yao kwa kuwanasa vibao ama kuwasweka rumande.
“Hapo utajiuliza muda wao walikuwa wapi hata hivyo ukiangalia vizuri utagundua wazi kuwa wakuu wa
Mikoa na Wilaya hawana kazi yoyote ya kufanya na badala yake watendaji wakuu ni Makatibu tawala wa Mikoa au wakurugenzi wa Halmashauri husika” amesema Mbunge huyo.
Wabunge wakipendekeza hayo baadhi ya watumishi katika halmasauri ya Dodoma,nao kwa masharti ya kutokutaka kutajwa majina wamesema kwamba kutokana na kasi ya utendaji wa Rais Magufuli sasa wanasiasa wanalazimisha kuingilia masuala ambayo ni ya kitaalam.
“Tunashangaa zaidi kuona wanasiasa kama vile wakuu wa wilaya na wakuu wa Mikoa wakiwakaripia watumishi ambao ni wanataaluma.

“Na pale wanasiasa wanaposhauriwa juu ya utendaji wao wanakuwa wakali wakali zaidi kwa sasa kilichobaki ni watumishi kukaa kimya ili wawasikilize wanasiasa lakini matokeo yake kazi zitalala” alisema Mtumishi huyo.

Yapo mambo mengine kwa sasa ambayo uwezi kuyafanya kutokana na kuhitajika kwa vitendea kazi,wakati mwingine unatakiwa kutoa tiba wakati huo hakina vifaa.
Watumishi hao wanalazimika kutoa yao ya moyoni kutokana na taarifa mbalimbali zinaziripotiwa kuwa wapo baadhi ya wakuu wa Wilaya na wakuu wa Mikoa ambao wanawazaba watumishi vibao na kuwashweka ndani watumishi.

Wakati huohuo baadhi ya wanasheria mkoani Dodoma wamewataka baadhi viongozi wa serikali kuacha kutumia madaraka yao vibaya kwa kuwadhibu baadhi ya watumishi wanaochelewa kazini kwani kufanya hivyo ni kosa.

Siku za hivi karibuni vyombo vya habari kumezagaa taarifa za baadhi ya viongozi ndani ya serikali wamedaiwa kutumia nyadhifa zao vibaya kwa kuwapiga au kuwasweka lumande watumishi wa ngazi ya chini pindi wanapobainika kuchelewa kufika kazini.
Wanasheria hao kwa kuweka weka sawa suala la wakuu wa mikoa na wilaya au kiongozi yotote kumpiga mtumishi walisema kwa kufanya hivyo ni kosa la jinai.

Wakizungumza na MwanaHalisi online mjini hapa juzi, bila kumlenga kiongozi yeyote, Wanasheria hao  walisema ni kosa kwa mtumishi wakiwemo viongozi kupigana katika sehemu za kazi.
Mmoja  wa mawakili  wa Kituo cha Sheria cha Goldmac Attorneys Advocates, Modester Mganga, alisema watumishi wote wa Idara za serikali wanapaswa kuzingatia sheria sehemu za kazi pamoja na utawala bora na si vinginevyo.

Alisema kuwa endapo kama ni kweli kuna mfanyakazi ambaye amefanyiwa vitendo hivyo vya kupigwa au kuwekwa rumande anayo haki ya kwenda kushitaki kwenye vyombo vya sheria kwa vile sheria za kazi ziko wazi kwamba zina kataza watumishi kupigana sehemu za kazi.

0 comments:

Chapisha Maoni