Mamlaka ya Mapato Nchini (TRA) imetaja majina ya kampuni 43 na wamiliki
wa makontena 329 ambayo yalipitishwa bandarini bila kulipiwa na
kufichuliwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa wiki iliyopita.
Aidha, TRA imesema imesimamisha kazi watumishi wake 35 wanaofanya kazi
katika ngazi mbalimbali, wakiwemo 27 waliokamatwa wiki hii katika Geti
Namba Tano.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Kaimu
Kamishna Mkuu wa TRA, Dk. Philip Mpango alisema Mamlaka hiyo iliagizwa
na Waziri Mkuu Majaliwa kuchukua hatua mara moja kwa kufuatilia na
kubaini wamiliki wa Bandari Kavu (ICD) zilizohusika katika kashfa hiyo.
Alisema mbali na hilo walitakiwa kuwatambua wamiliki wa makontena hayo,
bidhaa zilizokuwemo, kuwalipisha wahusika kodi iliyokwepwa pamoja na
kuwachukulia hatua watumishi waliohusika na upotevu huo.
Dk. Mpango aliyataja makampuni hayo kuwa ni Lotai Steel Tanzania Ltd
iliyokuwa na makontena 100, Tuff Tryes Centre Company 58, Binslum Tyres
Company Ltd 33, Tifo Global Mart Company Limited 30, Ips Roofing Company
Limited 20, Rushywheel Tyre Centre Co Ltd 12 na Kiungani Trading Co Ltd
10.
Makampuni mengine yaliyotajwa ni Homing International Limited (9), Red
East Building Materials Company Ltd (7), Tybat Trading Co Limited (5),
Zing Ent Ltd (4), Juma Kassem Abdul (3), Salum Link Tyres (3), Ally
Masoud Dama (2), Cla Tokyo Limited (2), Farid Abdullah Salem (2), Salum
Continental Co (2), Zuleha Abbas Ali (2) na Snow Leopard Building (2).
Wamiliki wengine wa makampuni ambayo yalikuwa na kontena moja moja ni
Abdulaziz Mohamed Ally, Ahmed Saleh Tawred, Ali Amer, Ally Awes
Alhamdany, Awadhi Salim Saleh, Fahed Abdallah Said, Hani Said, Hassan
Husrin Suleyman, Humud Suleiman Humud, Kamil Hussein Ali na Libas
Fashion.
Wengine ni Nassir Salehe Mazrui, Ngiloi Ulomi Enterprises Co Ltd, Omar
Hussein Badawy, Said Ahmad Hamdan, Said Ahmed Said, Salumu Peculier
Tyres, Sapato N. Kyando, Simbo Yonah Kimaro, Strauss International Co.
Ltd na Swaleh Mohamed Swaleh.
Alisema kwa ujumla, makampuni hayo yalipitisha makontena 329 ambayo
yaliondolewa kinyume cha taratibu kutoka ICD ya Azam inayomilikiwa na
Said Salim Bakhresa And Company Limited.
Dk. Mpango alisema bidhaa zilizokuwemo ndani ya makontena hayo ni pamoja
na matairi ya magari, samani mbalimbali, betri za magari, vifaa vya
ujenzi, nguo na bidhaa zingine mchanganyiko.
27 WALIOKAMATWA
Aidha, Dk. Mpango alisema watumishi 35 wa Mamlaka hiyo wanaofanya kazi
katika vitengo mbalimbali wamesimamishwa kazi, wakiwemo 27 waliokamatwa
wiki hii katika geti namba tano.
Alisema watumishi hao wanashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa mahojiano
huku akisisitiza kuwa mtumishi yoyote wa TRA atakayebainika kuhusika
katika hujuma hiyo atachukuliwa hatua kali za kinidhamu kwa mujibu wa
sheria na kanuni za kazi kulingana na makosa atakayokutwa nayo.
Alisema TRA inaendelea kupanga safu ya watumishi wake ili kuthibiti
upotevu wa malipo ya kodi na kwamba wanapitia upya taratibu za utoaji
leseni kwa Bandari Kavu ili kuondoa mianya na kuweka udhibiti katika
uondoshaji wa mizigo katika bandari zote na bohari za forodha.
“Pamoja na hatua hizi, TRA inafuatilia kwa kina ili kubaini mawakala
wote wa forodha walioshiriki katika upotevu wa makontena hayo na
kuwachukulia hatua ikiwemo kuwafungia leseni pamoja na adhabu zingine
kwa mujibu wa sheria,” alisema Dk. Mpango
Mwishoni mwa wiki iliyopita serikali ya awamu tano chini ya Rais John
Magufuli ilibaini ukwepaji wa kodi kwa kutorosha makontena 329 ambayo
yamenyima serikali kodi ya Sh. bilioni 80.
Rais Magufuli alimsimamisha kazi Kamishna Mkuu wa TRA, Rished Bade huku
Jeshi la Polisi likiwashikilia maofisa kadhaa waandamizi wa Mamlaka hiyo
akiwemo Kamishina wa Forodha, Tiagi Masamaki.
Masamaki na wengine saba walifikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi wa Kisutu jana.
NIPASHE
Jumamosi, 5 Desemba 2015
Home »
» Watorosha Makontena Bandarini Bila Kulipia Ushuru Hawa Hapa...Majina Yatajwa
0 comments:
Chapisha Maoni