Kikosi cha magwiji hao maarufu kama
`Real Madrid Legends` kitafanya ziara ya siku nne nchini kuanzia Agosti
22 mwaka huu na kitacheza mechi moja ya kirafiki dhidi ya kikosi maalumu
cha nyota wa Tanzania.
Akizungumza leo na waandishi wa
habari katika hoteli ya New Afrika, jijini Dar es salaam, meneja wa
ziara hiyo, Dennis Ssebo amesema mbali na Vodacom, wadhamini wengine ni
Fastjet, Tropical, Pembe Flower, Lake Gas, EFM Radio na Ladger Plaza
Bahari Beach.
Ziara hiyo ni mwaliko wa kampuni ya
Tanzania Sisi ni Nyumbani (TSN), chini ya mkurugenzi wake mkuu, Farough
Baghozah na meneja wa ziara hiyo ni Dennis Ssebo.
Wachezaji wa Real Madrid waliocheza
La Liga miaka ya nyuma, ligi ya mabingwa kombe la dunia kama vile
Mfaransa Zinedine Zidane, Mreno Luis Madeila Figo na Mbrazil Ronaldo de
Lima watakuwepo katika ziara hiyo.
Ssebo kabla ya mkutano wa leo,
aliuambia mtandao huu kuwa maandalizi ya ziara hiyo yanakwenda vizuri na
itakuwa fursa pekee kwa Watanzania kuiona Real Madrid kwa mara ya
kwanza barani Afrika.
“Ninaloweza Kusema ni kwamba,
Watanzania wakae tayari kupokea wachezaji 27 wa zamani wa timu ya Real
Madrid na mashabiki 23 kutoka Hispania wanaokuja kuwashangilia magwiji
wao. Kwahiyo jumla tunapokea watu 50 kutoka Hispania kwa ajili ya ziara
hii”. Alisema Ssebo.
“Ni ziara ambayo tulifikiria itakuwa
fupi, lakini wenzetu kumbe wameipenda nchi na wanaifahamu, kwahiyo ni
ziara ambayo itachukua takribani siku nne”. Aliongeza.
0 comments:
Chapisha Maoni