Mwanasheria Mkuu wa Chadema na mbunge wa Singida Mashariki kupitia chama
 hicho, Tundu Lissu amezungumzia hatua yake ya kujitosa kuwania urais wa
 Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS).
Mosi, Lissu amesema amepata msukumo kutokana na kauli ya rais John 
Magufuli kuwa kuna kampeni zimeanza za kumuondoa rais wa sasa wa TLS na 
zinaendeshwa na chama fulani ambacho kimeweka mgombea wake.
Pili, akasema Lissu ni kauli kuwa mawakili wanaotetea wauza dawa za kulevya nao wakamatwe wawekwe ndani.
“Sikuwa na mpango wa kugombea lakini the moment (wakati) aliposema, nikasema sasa nitagombea urais wa TLS,” amesema mbunge huyo.
Rais alitoa matamko hayo katika sherehe za maadhimisho ya Siku ya Sheria
 iliyofanyika mapema mwezi huu kwenye uwanja wa Mahakama Kuu jijini Dar 
es Salaam.
Lissu amesema TLS imepoteza mwelekeo na nafasi yake katika jamii kwenye 
masuala ya kisheria, hasa kushindwa kukemea vitendo vya uvunjifu na 
ukiukaji wa Katiba na sheria unaofanywa na viongozi.
“Chama cha wanasheria kinatakiwa kiwe cha kwanza kupiga kelele sheria za
 hovyo zinapotungwa, kinatakiwa kuwa mstari wa mbele kukemea vitendo vya
 ukiukaji wa Katiba na sheria vinavyofanywa na watu wenye mamlaka lakini
 Law society ya kwetu imekaa kimya,” amesema.
Kuhusu msimamo wake wa kisiasa na chama hicho endapo atapata nafasi 
hiyo, Lissu amesema masuala ya kisheria hayana uhusiano na vyama vya 
kisiasa na kwamba chama hicho kipo kwa ajili ya kulinda na kusimamia 
utawala wa sheria.
Pia, amesema kama chama chake kitakuwa na msimamo sawa na misingi ya 
chama hicho katika kutetea utawala wa kisheria, si tatizo na kwamba, 
ikiwa kitakuwa na msimamo tofauti katika mambo ya msingi, hakina budi 
kukosolewa.
“Sigombei ili kuipeleka Chadema ndani ya TLS. Masuala haya yanatuhusu 
sisi wote kujua mambo yanapoharibika, kuona sheria zinapokiukwa na kuona
 sheria mbovu zinapotungwa,” alisema.
Ofisa Maboresho ya Sheria wa TLS, Mackphason Buberwa amesema mchakato wa
 kupata wagombea umeshakamilika na waliopitishwa na kamati ni watano.
“Taratibu zimekamilika, kilichobaki ni wagombea kuandaa kampeni zao 
kabla ya Machi 18 siku ambayo uchaguzi utafanyika mjini Arusha,” amesema
 Buberwa.
Wagombea wengine ni Francis Stola, Lawrance Masha, Victoria Mandali na 
Godwin Mwapongo. Uchaguzi huo umepangwa kufanyika Machi 18 jijini Arusha
 ambako zaidi ya mawakili 6,000 wanatarajiwa kuhudhuria.







 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
0 comments:
Chapisha Maoni