Paul Makonda Afunguka Kuitwa na Bunge Kwa Ajili ya Kuhojiwa
MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amesema hawezi kufika mbele
ya Kamati ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge kuhojiwa kwa kuwa
hajapokea barua ya kuitwa.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Makonda alisema hatoweza kwenda
mbele ya kamati hiyo bila barua rasmi iliyomtaka kufanya hivyo.
Bunge lililokuwa likiendelea na vikao vyake Dodoma kabla ya kuahirishwa
juzi, lilipitisha uamuzi wa kuwataka Makonda na Mkuu wa Wilaya ya
Arumeru, Alaxander Mnyeti, kufika mbele ya kamati hiyo na kuhojiwa
kutokana na kauli walizozitoa, zinazodaiwa kuudharau mhimili huo wa
dola.
Lakini Makonda alisema jana “hilo suala la mimi kuitwa kwenye kamati nalisikia na kulisoma kwenye magazeti."
"Sina uhakika ni lini wamefikia uamuzi huu wa kuniita na hata kama wamefikia uamuzi huo, sijaletewa barua rasmi.”
Baada ya Bunge kupitisha uamuzi huo wa kuitaka Ofisi ya Bunge iwaandikie
barua viongozi hao, juzi baadhi ya wabunge walihoji kauli ya Katibu wa
Bunge, Dk. Thomas Kashililah, kwamba azimio la chombo hicho cha kutunga
sheria kumtaka Makonda kufika mbele ya kamati kujieleza kuhusu tuhuma za
kuudharau mhimili huo, halikufuata utaratibu.
Hatua hiyo iliamsha hasira kwa baadhi ya Wabunge na kuomba mwongozo
kuhoji kwa nini Katibu wa Bunge ametoa kauli ambayo inakinzana na
makubaliano ya Bunge.
Mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara na mwezake wa Iringa Mjini Mchungaji
Peter Msigwa (wote Chadema) walihoji kuhusu kauli ya Dk. Kashililah.
Waitara alisema, “Asubuhi ya leo ( juzi) nimetumiwa ‘clip’ ya sauti ya
Katibu wa Bunge akikosoa uamuzi wetu hapa na pia gazeti la Habari Leo,
Ukurasa wa 25, kuna habari imeandikwa.
Katika taarifa hii, Katibu wa Bunge anasema maazimio ya Bunge yalikosewa
na hayakufuata utaratibu,” alisema na kuongeza kuwa: “ Kwa maana
nyingine, hatatekeleza kile tulichokubaliana.”
Mchungaji Msigwa wakati akichangia taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge
ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, alieleza kuwa hajafurahishwa na
kauli ya Katibu wa Bunge.
Alisema Katibu wa Bunge amekosea kwenda katika vyombo vya habari na
kudai chombo hicho cha kutunga sheria kimekosea kwa kuwa anafanya kazi
ya Bunge na kwamba hajaajiri wabunge na anapaswa kufuata maagizo yao.
Hoja ya kutaka kina Makonda washughulikiwe iliwasilishwa na Mbunge wa
Ukonga, Mwita Waitara (Chadema) katikati ya wiki na ilijadiliwa na
kuungwa mkono na wabunge wote, wakiwamo mawaziri kwa kusema ‘ndiyo’.
0 comments:
Chapisha Maoni