MBUNGE wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe, amesema Serikali ya Awamu ya Tano imewahadaa wananchi kuhusu kuwapa Sh. milioni 50 kila kijiji/mtaa huku akiamini ahadi hiyo haitekelezeki.
Zitto alisema ahadi hiyo "kimahesabu, haitekelezeki."
"Kwanza kwenye bajeti ya Waziri Mkuu, fungu lililotajwa la Sh. bilioni 59 halipo. Na hata kama lipo Tamisemi wanakodai wao (Ofisi ya Waziri Mkuu), halitoshi kuvikopesha vijiji vyote Tanzania," Zitto alisema na kuongeza:
"Sh. bilioni 59 katika mwaka wa fedha 2016/17 maana yake vijini 1,000 tu vitapatiwa fedha. Kama serikali inatekeleza ahadi hiyo kwa vijini 1,000 kila mwaka, maana yake ni kwamba katika miaka mitano ya Rais Magufuli Ikulu, ahadi hiyo itatekelezwa katika vijiji 5,000 tu.
"Huku ni kuwahadaa wananchi. Tanzania ina zaidi ya vijiji 15,000. Kwa fungu linalotengwa, vijini zaidi ya 10,000 havitapata fedha hii."
MASHARTI MAGUMU
Wakati Zitto akitoa tahadhari hiyo, imebaini kuwepo kwa vigezo vya kupata fungu la Sh. milioni 50 za kila kijiji/mtaa ni vigumu.
Akihitimiha mjadala wa makadirio ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu katika mwaka wa fedha 2016/17 wiki iliyopita Majaliwa, alivitaja vigezo saba vitakavyotumika kugawa fedha za mradi huo, huku vyote vikionekana vitakuwa na ugumu kunufaisha wananchi wengi hasa katika maeneo ya vijijini.
Majaliwa alisema mradi huo unalenga kuwawezesha wananchi kiuchumi kwa njia ya kukopesha vikundi vya wajasiriamali kupitia ushirika wa kuweka na kukopa katika vijiji.
Alivitaja vigezo vya kukopeshwa fedha hizo kuwa ni kikundi cha kifedha kiwe kimesajiliwa na Halmashauri na Tume ya Ushirika, kikundi kiwe na Katiba, uongozi uliochaguliwa kidemokrasia na kupata mafunzo ya mikopo pamoja na kikundi hicho kuwa chini ya Asasi ya Kiraia inayotambulika na yenye uzoefu wa shughuli za mikopo.
Majaliwa alikitaja kigezo cha nne kuwa ni kikundi husika kionyeshe uzoefu wa kukopeshana kwa muda wa mwaka mmoja tangu kuanzishwa na historia ya urejeshaji mikopo ya asilimia 95 na cha tano ni kuwa dhamana ya serikali itakuwa kwenye kiasi cha msingi cha mkopo na si kwenye kiasi riba.
"Kigezo cha sita ni kikundi kuweka amana ya akiba ya fedha kwenye benki katika akaunti maalumu (Fixed Deposit) asilimia 10 ya mkopo," alisema.
Majaliwa alisema kigezo cha saba ni kuzingatiwa kwa Sheria ya Vyama vya Ushirika ya mwaka 2013 kuhusu mkopo kwa SACCOS.
Alisema serikali imeandaa mpango wa kutoa elimu kwa wananchi kuhusu suala hilo hususan masuala ya ujasiriamali na biashara
Chanzo: Siasahuru.com
Jumatatu, 2 Mei 2016
Home »
» Zitto: Millioni 50 za Magufuli Kila Kijiji ni Hadaa Kwa Wananchi.
0 comments:
Chapisha Maoni