Jumamosi, 12 Desemba 2015

Baada ya Nape Kula Shavu la Uwaziri wa Habari, Utamaduni, Wasanii na Michezo.. TFF yatoa Tamko Hili



Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi amemtumia salamu za pongezi mbunge wa jimbo la Mtama, Nape Nnauye kufutia kuteuliwa kuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Wasanii na Michezo katika serikali ya awamu ya tano.
Katika salamu zake, Malinzi amempongeza Nape na kusema TFF ina imani nae katika nafasi hiyo, na kuahidi kushirikiana katika michezo na haswa katika kusukuma gurudumu la maendeleo ya mpira wa miguu nchini.
Aidha pia Malinzi amewapongeza Paschal Kihanga, Mwenyekiti wa chama cha soka moa Morogoro kwa kuchaguliwa kuwa Meya wa manispaa hiyo, na James Bwire mmiliki wa shule ya Alliance kwa kuchaguliwa meya wa manispaa ya Nyamgana.
Malinzi amewatakia kila la kheri katika nafasi hizo walizozipata za kuwatumikia watanzania, na kwa niaba ya familia ya mpira wa miguu nchini anawatakia kila la kheri na kuahidi kushirikiana nao.

Rais Magufuli Amwaga Mabilioni Bodi ya Mikopo Elimu ya Juu..Shirikisho la Wanafunzi wa vyuo vikuu Tanzania Wasema Haya



Shilingi billion 473 zimetengwa kwa ajili ya kutoa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu nchini kwa mwaka huu ikilinganishwa na Shilingi bilioni 341 zilizotolewa  mwaka jana ikiwa ni ongezeko la Tsh. bilioni 132 katika bajeti ya mwaka huu.
Hayo yalisemwa  jana jijini Dar es salaam na Mwenyekiti wa shirikisho la wanafunzi wa vyuo vikuu Tanzania(Tahliso)  bwn. Nzilanyingi  John  alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kuaandaa mdahalo kujadili hotuba ya Rais Dkt. John Magufuli aliyoisoma Dodoma wakati wa ufunguzi wa bunge la kumi na moja .
Alisema kuwa kwa kipindi kifupi kumekuwa na  mabadiliko ya haraka yaliyotokea katika sekta ya elimu nchini kwa mwaka huu  kwani kuna ongezeko la zaidi ya wanafunzi 1800 waliopata mkopo ikilinganishwa na mwaka uliopita ambapo ni wanafuzi 34128 pekee ndio waliofanikiwa kupata mkopo.
“Mpaka sasa jumla ya wanafunzi 51,675 wa mwaka wa kwanza wamepata mkopo na lengo ni kufikia 53,032, pia jumla ya wanafunzi 91 wa shahada ya uzamili  na wanafunzi 113 wanaosoma vyuo vya nje tayari wamepata mkopo” alisema John.

Aliongeza kuwa katika kipindi kifupi kijacho bodi ya mikopo imehakikisha kutoa mikopo kwa wanafunzi zaidi ya elfu moja wanaochukua Diploma maalumu ya ualimu Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) na hivyo kukamilisha adhma yao ya kutoa mikopo kwa wanafunzi 53,032.
Aidha shirikisho hilo ambalo ni umoja wa viongozi wa serikali za wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu nchini umeandaa mdahalo wenye lengo la kutoa fursa kwa watanzania wengi kujadili hotuba hiyo  na namna rais alivyoanza kutekeleza majukumu yake katika nafasi hiyo.
Mdahalo huo utafanyika jijini Dar es Salaam tarehe 13 mwezi huu katika ukumbi wa Nkurumah na wazungumzaji wakuu katika mdahalo ni Mtaalamu mbobevu wa uchumi kutoka chuo kikuu cha Mzumbe Prof.Honest Ngowi, Dkt. John Lingu kutoka Idara ya Sayansi ya Siasa ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Mwanadiplomasia Christopher Liundi.

Ijumaa, 11 Desemba 2015

Namba za Simu za Kuripoti Kero TRA na taarifa za siri za Watumishi Wabadhirifu

Dk Mpango ametaja namba za simu na kuomba wananchi waripoti taarifa zinazohusu watumishi wa ofisi ya Mamlaka na Mapato Tanzania (TRA), wanaojilimbikizia mali kinyume na kanuni za utumishi wa umma.

Pia ameomba namba hizo zitumike kutoa taarifa kuhusu kero wanazokumbana nazo wananchi katika ofisi za TPA.
Piga simu 0689 122 515
Tuma ujumbe mfupi wa maneno (sms) 0689 122 516
Pia ametoa namba yake kuwa ni 0787 570 714 na ya Naibu wake kuwa ni 0784 228 095

Profesa Lipumba, Lissu wapinga uteuzi wa Muhongo na Mwakyembe

Saa chache baada ya rais Magufuli kutangaza baraza lake la Mawaziri ambalo limekuwa baraza dogo kama alivyoahidi, aliyekuwa mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF) na mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu wamekosoa uteuzi wa Profesa Sospeter Muhongo na Dk. Harison Mwakyembe.

Dk. Mwakyembe alikuwa waziri wa Uchukuzi katika serikali ya awamu ya nne na hivi sasa ameteuliwa kuwa waziri wa Katiba na Sheria. Profesa Muhongo ambaye alijiuzulu kwa kashfa ya Escrow katika serikali ya awamu ya nne, amerudishwa katika wizara ya Nishati na Madini.

Profesa Lipumba amekosoa uteuzi wa profesa Muhongo kwa madai kuwa uteuzi wake umelitia doa baraza hilo.

“Kwa kitendo kama hiki, Rais Magufuli amejiwekea dosari kutokana na uteuzi huu. Maana yake ni kuwa katika kashfa ile Profesa Muhongo hakuwa na hatia,” Profesa Lipumba aliliambia gazeti la Mwananchi.

Profesa Lipumba aliongeza kuwa wananchi watapata ugumu kumuelewa Rais kutokana na ahadi zake kuwa atapambana na rushwa na ufisadi.

Naye Tundu Lissu aliliambia gazeti hilo kuwa uteuzi wa Dk. Harison Mwakyembe hakuwa sahihi kwa kuwa ndiye aliyekuwa waziri wa Uchukuzi na punde baada ya rais Magufuli kuingia ikulu, Mamlaka ya Bandari ikabainika kukumbwa na kashfa ya upotevu wa makontena.

“Juzi Rais Magufuli aliufumua uongozi wa Bandari ya Dar es Salaam kutokana na kashfa, miongoni mwa waziri waliokuwa wakisimamia sekta hiyo ni Dk. Harrison Mwakyembe, eti leo amemrudhisha kundini?” Lissu ananukuliwa.

Lissu aliongeza kuwa Muhongo pia hakufaa kuwa miongoni mwa mawaziri kwa kuwa alifukuzwa na Bunge kutokana na sakata la Escrow.

Hata hivyo, Profesa Lipumba alimpongeza rais kwa kutekeleza ahadi yake ya kuunda baraza dogo kwa lengo la kubana matumizi.

Home Shoppinga Center Yajitokeza Kujibu Tuhuma Za Kukwepa Kodi

Baada ya kusambaa kwa taarifa kwenye mitandao zikieleza kuwa kampuni ya Home Shopping Centre imefunga maduka yake kutokana na kukwepa kodi na kuhusika kwenye sakata la makontena yaliyopotea bandarini, uongozi wa kampuni hiyo umejitokeza na kupinga taarifa hizo.

Kupitia taarifa yake kwa vyombo vya habari, kampuni hiyo imeeleza kuwa habari hizo sio za kweli na kueleza kuwa haijawahi kukwepa kodi na haihusiki kwa namna yoyote na makontena yaliyopotea bandarini.

“Home Shopping Centre Co. Limited haihusiki kabisa kwa njia yoyote ile na wizi, ukwepaji kodi, au potevu wa makontena 349 na yale zaidi ya 2431 yaliyoibuliwa na Mheshimiwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na kamwe haijawahi kujihusisha na uhalifu huo wa kuiba makontena na kukwepa kodi,” ilieleza taarifa hiyo iliyosainiwa na Mfilisi wa kampuni hiyo, Yusufu Mohamed.

Mohamed alieleza kuwa kampuni hiyo ilifunga maduka yake kama ambavyo makampuni mengine hufanya na sio vinginevyo.

Wema Sepetu Kortini Kwa Uwizi wa Umeme..Tanesco Waeleza Makubwa

KIMENUKA! Baada ya Miss Tanzania 2006 aliye pia nyota wa sinema za Bongo, Wema Sepetu ‘Madam’ kunaswa na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) akidaiwa kutumia umeme wa shirika hilo kinyemela, kuna madai atapandishwa kortini.
Taarifa kutoka chanzo makini zinasema kuwa, mrembo huyo alifanya ‘manuva’ hayo katika nyumba anayoishi, Kijitonyama, Dar hivyo kuweza kuliingizia hasara shirika hilo hali ambayo shirika hilo haliwezi kumvumilia.


“Amefanya ile michezo ya kuchezea mita. Mita inakuwa inasoma umeme mdogo lakini mzigo unaotumika ndani mkubwa, haufanani na malipo halisi ambayo alistahili kulipia,” kilisema chanzo chetu na kuongeza:
“Maofisa wa Tanesco juzikati ndiyo wakampitia. Inasemekana Wema alikuwa ndani na Idris (yule mshindi wa Big Brother Africa). Idris ndiye alitoka lakini Madam hakuinua miguu yake kwenda nje, wakamng’olea mita na kuondoka nayo.”

Baada ya chanzo hicho kuvujisha ubuyu huo sambamba na picha zilizosemekana ni za siku ya tukio wakati maofisa hao walipofika nyumbani hapo na kufanya ‘ambushi’, paparazi wetu alimpigia simu Wema kwa muda mrefu lakini hakupatikana, akampigia mtu wa karibu na Madam, Ahmed Hasheem ‘Petit Man’ ambapo alipatikana na kusema:

“Unajua kaka mimi si msemaji wa Wema. Mimi ni msemaji wa wasanii walio kwenye lebo ya Wema ya Endless Fame. Kama unataka msemaji wake, cheki na Martin Kadinda.”
Alipotafutwa Martin, alijibu kwa kifupi: “Kaka hata mimi nazisikia hizo habari lakini sipo Dar, nikirudi nitakwenda kucheki halafu nitakupa taarifa kamili.”
Juzi Jumanne, paparazi wetu alifika nyumbani kwa Wema ili kujionea sakata hilo lakini hakufanikiwa kuingia getini baada ya kugonga geti kwa muda mrefu bila majibu.
Mmoja wa majirani wa mrembo huyo aliyeomba hifadhi ya jina, alipoulizwa kuhusu kufahamu sakata hilo, alisema:

“Kiukweli sisi wenyewe tulishangaa. Tunaamini Madam si mtu kuchezea mita. Ni mtu anayejiweza, anayejitambua sasa tumeshtuka kuona mita inatolewa.”
Paparazi wetu alifika Ofisi za Tanesco Mkoa wa Kinondoni Kaskazini (Mikocheni) ili kuzungumza na wahusika lakini akakosa ushirikiano.

Hata hivyo, mfanyakazi mmoja wa Kitengo cha Emergency (Dharura) aliyeomba kufichwa jina lake, alisema ni kweli zoezi hilo lilifanyika nyumbani kwa Wema, Jumatatu iliyopita na kukutana na kadhia hiyo ambapo alisema madam huyo atapandishwa mahakamani kujibu mashitaka ya kuiibia Tanesco.
GPL

Jumanne, 8 Desemba 2015

Maneno ya DC Paul Makonda kuhusu kufanikisha kutatua mgomo wa kiwanda cha URAFIKI Dar..


Siku chache zilizopita wafanyakazi wa kiwanda cha nguo cha urafiki walifanya mgomo kwa madai ya kutolipwa mishahara yao kwa muda mrefu kupelekea mkuu wa wilaya ya Kinondoni, DC Paul Makonda kuagiza shughuli zote za kiwanda hicho zisimame mpaka mgogoro wa kimaslahi kati ya wafanyakazi na wamiliki wa kiwanda hicho utakapotatuliwa.

Sasa leo kupitia kwenye ukurasa wa instagram DC Paul Makonda aliandika maneno kuhusu namna alivyotatua mgogoro huo na kufanikisha kile kiasi wanachotakiwa kulipwa wafanyakazi kiwanda cha nguo cha URAFIKI kilichopo eneo la Shekilango Dar es Salaam.
Asante Mungu kwa kuniwezesha kuwatetea wanyonge wenzangu na wafanyakazi wa kiwanda cha urafiki na kufikia kulipwa kiwango 150000 tofauti na hapo zamani walipokuwa wanalipwa 80000 kwa mwezi….Jambo ambalo wameliomba tangu 2007′>>>>Paul Makonda